QUITO
Ecuador
Walau watu 116 wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na mapigano yaliyozuka ndani ya jela moja nchini Ecuador kati ya mahabusu na wafungwa wa makundi mawili hasimu.
Taarifa rasmi zinataja vurugu hizo kuwa ndizo mbaya zaidi kuwahi kutokea ndani ya jela za serikali katika historia ya taifa hilo.
Mahabusu watano wanaripotiwa kuchinjwa wiki iliyopita ndani ya gereza lililopo jijini Guayaquil, wakati wengine wakiuawa kwa risasi.
Inadhaniwa kuwa mahabusu hao waliozuiwa ndani ya Gereza la Litoral, wana uhusiano na matajiri wa dawa za kulevya wa Mexico.
Litoral inachukuliwa kama gereza hatari zaidi nchini humo.
Kamanda wa Polisi, Fausto Buenaño, anasema kwamba mahabusu hao walitumia pia mabomu ya kutupa kwa mkono. Askari polisi 400 wametumika katika kudhibiti ghasia hizo.
Vyombo vya habari vinadai kuwa machafuko hayo yalifanyika kwa maelekezo ya makundi yenye nguvu ya wauza dawa za kulevya wa Mexico, ambao sasa wanafanya shughuli zao Ecuador.
Mkurugenzi wa Magereza wa Ecuador, Bolivar Garzón, amesema hali ilikuwa mbaya sana.
“Jana saa nane mchana, polisi walifanikiwa kudhibiti hali, lakini usiku kukasikika milio ya risasi, vurugu na milipuko, kabla ya kuidhibiti tena hali hiyo asubuhi. Tumeingia katika maeneo yaliyokuwa na fujo na kukuta miili mingi zaidi,” anasema.
Mara kwa mara makundi yanayomilikiwa na miamba wa biashara haramu ya dawa za kulevya hupambana katika harakati zao za kutawala gereza.
Februari mwaka huu, wafungwa 79 waliuawa katika mapigano kama haya.
Buenaño anasema mahabusu kutoka upande mmoja wa gereza walitambaa kupita kwenye tundu moja na kuingia upande wa pili, kisha wakawashambulia mahasimu wao kutoka kundi jingine.
Zaidi ya mahabusu 80 wamejeruhiwa.
Wapishi sita waliojikuta katika ya mapigano hayo waliokolewa na polisi.
Rais Guillermo Lasso ametangaza hali ya hatari katika mfumo mzima wa magereza.
Gereza la Litoral linatunza mahabusu kutoka Los Choneros, genge la Ecuador linalodhaniwa kuwa na uhusiano na Sinaloa, kundi lenye nguvu la Mexico.
Lakini kundi linalojiita la kizazi kipya, Jalisco New Generation cartel (CJNG), pia kutoka Mexico, lipo katika jitihada za kushawishi ushirikiano na makundi ya Ecuador katika biashara ya magendo ya dawa za kulevya kutoka Ecuador kuelekea Amerika ya Kati; njia inayomilikiwa kwa sasa na Sinaloa.
Julai mwaka huu, Rais Lasso alisema magereza nchini humo yamefurika kwa zaidi ya asilimia 30.