Siku chache zilizopita Tanzania imekumbwa na taharuki baada ya kutangazwa rasmi kuwapo kwa mgawo wa umeme na maji katika miji na majiji kadhaa.
Taarifa hii ya kushitusha imetokana na ukosefu wa mvua za vuli na za msimu zilizotarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi kuanzia mwezi uliopita.
Hali hiyo sasa imesababisha kupungua kwa kina cha maji katika mito mingi nchini; ambayo mbali na kuwa chanzo kikuu cha maji yanayotumiwa viwandani na majumbani, pia ndicho chanzo kikuu na muhimu cha umeme.
Kwa kuwa tayari taifa limeingia katika hali hiyo, tunaamini kuwa hakuna haja ya kunyosheana vidole, badala yake tujipange ili hali hii isiwe ya kudumu na isijirudie siku za usoni.
Miongoni mwa hatua za haraka ni kuwaondoa watu wote wanaoharibu vyanzo vya maji katika mito na chemchemi zote nchini; kuanzia kwenye milima ya Makete, vijito vinavyoingiza maji Mto Ruvu hadi yanakomwagika katika Bahari ya Hindi kupitia Mto Rufiji.
Hatua nyingine ya muda mrefu ni kuweka mikakati ya kuongeza matumizi ya gesi majumbani kwa kuimarisha mradi ulioasisiwa miaka kadhaa iliyopita wa kusambaza gesi hiyo katika mfumo sawa na wa DAWASCO au TANESCO.
Hilo tayari limesemwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inayotaka suala la usambazaji gesi majumbani lipewe kipaumbele kama ilivyokuwa kwa umeme vijijini.
Wito huo umetolewa na Naghenjwa Kaboyoka (MB) ambaye ni Mwenyekiti wa PAC, baada ya ziara waliyoifanya kutembelea miundombinu ya gesi katika mikoa ya Mtwara, Pwani na Dar es Salaam.
Kwa hakika matumizi ya gesi yataokoa misitu inayokatwa kwa ajili ya kupata mkaa wa matumizi ya majumbani. Misitu ndiyo inayohifadhi ikolojia ya mito na maziwa nchini na kuondoa ukame.
Mpango wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) wa kushirikisha sekta binafsi kutaka kusambaza gesi hiyo usiishie kwenye makabrasha ndani ya ofisi zao, bali unapaswa kuhamishiwa mitaani kwa vitendo.
Jamii iwe tayari kushiriki katika mapinduzi ya matumizi ya nishati mbadala, hasa gesi, kwa ari na mali, hata kama tutalazimika kufunga mikanda ili kuhakikisha kizazi kijacho hakikumbani na adha kama hii tunayoishuhudia kwa sasa.