Deni la serikali la ndani lilipungua kwa mara ya kwanza mwaka jana katika kipindi cha miaka kumi kutokana na kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya ndani ambayo hivi sasa yamefikia Sh trilioni 1.6 kwa mwezi, JAMHURI limebaini.

Takwimu mpya za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa deni hilo liliongezeka mfululizo kutoka Sh bilioni 2,712.4 mwaka 2009 hadi Sh bilioni 14,631.4 mwaka 2018 kabla ya kupungua kwa Sh bilioni 196.2 mwaka uliofuata.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni ya hali ya uchumi nchini, taasisi hiyo ya fedha inasema sababu kubwa ya kupungua kwa deni la serikali la ndani ni kutokana na kuimarika kwa mapato kunakochangiwa kwa kiasi kikubwa na kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mafanikio haya ni matokeo ya jitihada za kudhibiti ukwepaji wa kodi ambao ulikuwa ni chanzo kikubwa cha kuikosesha serikali mapato na kuilazimisha kukopa kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi ili kugharamia bajeti zake na matumizi mengine.

“Deni la serikali la ndani lilikuwa Sh bilioni 14,435.2 mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2019, likiwa limepungua kwa kiasi cha Sh bilioni 12.3 kulinganisha na mwezi uliotangulia na pungufu ya Sh bilioni 196.2 kwenye kipindi kama hicho mwaka 2018,” Benki Kuu inasema katika Tathmini ya Hali ya Uchumi kwa Mwezi (MER) ya Januari mwaka 2020.

Zaidi ya makusanyo ya mapato ya ndani kuimarika na kuiwezesha serikali kutumia fedha zake yenyewe, BoT inasema kuwa kupungua kwa deni hilo pia kulitokana na kiasi kilicholipwa kuzidi pesa yote iliyokopwa katika kipindi hicho.

Kwa mwezi Disemba, mapato ya ndani yalikuwa Sh bilioni 2,112.5, kiasi ambacho ni asilimia 15.5 zaidi ya makusanyo ya mwezi Disemba mwaka 2018 huku sehemu kubwa ikiwa ni mapato yaliyokusanywa na serikali kuu. Mapato yatokanayo na kodi yaliongezeka kwa asilimia 20.2 hadi Sh bilioni 1,904.9 na kuvuka lengo la mwezi kutokana na kuimarika kwa juhudi za kusimamia na kukusanya kodi.

Kwa mujibu wa Muhtasari wa Tamko la Sera ya Fedha wa BoT, ukusanyaji wa mapato ulivuka malengo mwezi Septemba na Disemba katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka huu wa fedha.

“Mapato yaliyokusanywa na kuwekwa kwenye akaunti za serikali zilizoko Benki Kuu ya Tanzania yalikuwa Sh bilioni 9,810.8 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2019/20, sawa na wastani wa makusanyo ya Sh bilioni 1,635.1 kwa mwezi,” BoT inasema na kuongeza kuwa kiasi hicho ni sawa na asilimia 96.6 ya lengo la makusanyo kwa kipindi hicho.

“Kuongezeka kwa makusanyo ya mapato kwa sehemu kubwa kulitokana na jitihada kubwa za Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kuhakikisha ulipaji stahiki wa kodi unasimamiwa kwa dhati,” Benki Kuu inafafanua kwenye tamko hilo la mwezi Februari lililotolewa mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Chapisho hilo linalotoa tathmini ya hali ya uchumi wa nchi na dunia pamoja na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa sera ya fedha katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/20 linasema deni la serikali la ndani na nje limeendelea kuwa himilivu. Hii ni kutokana na ukuaji endelevu wa uchumi na maboresho ya sera na usimamizi thabiti wa taasisi.

Takwimu kwenye MER mpya zinaonyesha kuwa deni la ndani lilikuwa Sh bilioni 14,631.4 Disemba mwaka 2018 na Sh bilioni 13,411.2 kipindi kama hicho mwaka uliotangulia. Disemba mwaka 2016 deni hilo lilikuwa Sh bilioni 11,418.9 baada ya kupanda kutoka Sh bilioni 9,810.1 mwaka 2015.