Na Eleuteri Mangi, WUSM
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameipongeza Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kufuzu katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON, 2023 zitakazofanyika mapema mwaka 2024 nchini Ivory Coast.
Waziri Dkt. Ndumbaro ametoa pongezi hizo Septemba 8, 2023 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa kwa Wabunge na watanzania wote kufuatia hatua hiyo ya Taifa Stars kwenye mashindano ya Afrika.
Katika salamu zake, Waziri Dkt. Ndumbaro amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono mapana aliyonayo kwa Sekta ya Michezo kwa kutoa miongozo ambayo imekuwa na tija na kupelekea mapinduzi makubwa katika ya sekta ya michezo nchini.
“Kupitia maono yake, tasnia ya Michezo nchini inaendelea kuthaminiwa na matunda yake yanaonekana hasa timu zetu za Taifa na hii ya Taifa Stars ikiwa kinara kwa kutuheshimisha jana nchini Algeria” amesisitiza Waziri Dkt. Ndumbaro.
Waziri Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa maandalizi ya timu ya Taifa katika ushiriki wa michezo ya Kimataifa yanajumuisha malipo ya malazi, chakula, usafiri na malipo ya mshahara wa kocha wa timu ya Taifa Bw. Adel Amrouche ambaye analipwa mshahara na Serikali na ameiongoza timu ya Taifa kufuzu katika fainali za AFCON katika Uwanja wa ugenini nchini Algeria mafanikio ambayo yanatokana na maamuzi sahihi yanayodhihirika kwa vitendo.
Tanzania ilifika hatua ya Fainali Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2023 ambayo ndiyo mashindano makubwa Barani Afrika kuliko mashindano yoyote, Taifa Stars imefanikiwa kuingia kwa mara ya tatu katika zitakazofanyika nchini Ivory Coast kuanzia Januari 13, hadi Februari 11, 2024 yakiwa ni mafanikio kubwa ya tasnia ya Michezo nchini.
Kwa mara ya kwanza Tanzania ilifika hatua ya Fainali ya mashindano hayo mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria ambapo timu nane zilishiriki mashindano, mara ya pili ilikuwa mwaka 2019 katika nchini Misri na Tanzania ilikuwa moja kati ya timu 24 zilizofanikiwa kufuzu.
Aidha, Waziri Dkt. Ndumbaro amesema kuwa timu Taifa Stars itakaporejea itakabidhiwa nchini itakabidhiwa kiasi cha Shilingi 500,000,000/= ambazo zilikuwa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iwapo timu hiyo itafuzu katika Fainali za AFCON.