Septemba 7, mwaka huu kwenye jengo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, kulifanyika Kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere –miaka 20 tangu alipofariki dunia. Wasomi na watu mashuhuri mbalimbali walitoa mada. Miongoni mwao ni Samuel Kasori aliyetoa mada hii iliyochapishwa hapa. Endelea…

“Hakuna mtu anayetaka kuwapenda wengine zaidi ya tunavyojipenda wenyewe; lakini kwa baadhi yetu tuliobahatika kupata elimu nzuri tunawajibika kuboresha ustawi wa jamii tunamoishi, ni sehemu ya kujipenda sisi wenyewe.”  Julius K. Nyerere.

Katika kongamano tajwa hapo juu, zipo mada kadhaa ambazo ziliwasilishwa na viongozi pamoja na wasomi kadhaa. Nililazimika kujituma kuchangia jitihada kubwa anazozifanya Rais John Magufuli katika kujenga na kuimarisha uchumi wa viwanda nchini Tanzania kwa yeye binafsi kuendelea kumuenzi kwa vitendo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hususan wakati huu ambao ni miaka 20 bila uwepo wa yeye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Miongoni mwa mada zilizokuwemo katiba ratiba ni juu ya uhusiano kimaendeleo kati ya mataifa ya Kaskazini na Kusini, yaani reflection on North – South, South – South economic relations and commodity trade and investment systems, ambapo mchangia hoja alikuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Dunia ya leo katika karne hii ya 21 ambayo kimsingi imeendeshwa kwa Sayansi na Teknolojia kabisa hatuwezi kwa yanayotokea duniani kupuuza kupiga darubini katika yale yanayotendeka huko katika mataifa ya Kaskazini ambapo kuna nguvu kubwa ya UCHUMI WA VIWANDA na sisi tuliobaki katika nchi za Kusini tunaoendelea kuonekana kuwa Bara letu la Afrika ni laana tupu.

 Sasa tujiulize:-

•Ni kweli kuwa sasa mataifa yetu ni nchi huru?

•Je, ni kwa nini wakulima, wafugaji, wavuvi na wengine wengi tu bado wanaendelea kukandamizwa katika lindi la umaskini, ujinga na maradhi?

•Je, ni kitu gani ambacho kinaweza kufungua haraka breki za uchumi wa nchi zetu zilizo nyuma?

•Je, tufanye nini ili tujitoe haraka pale tulipoganda na tutie kasi kubwa ya maendeleo yenye sura ya utu?

•Kwanini Bara la Afrika, Tanzania ikiwamo, tunaendelea kusimama pale pale tena bila matumaini katika karne hii ya 21?

•Kwanini maendeleo ya kilimo, uvuvi, mifugo na viwanda, yote ambayo ni muhimu kabisa yanaandamwa na vikwazo na kusitasita huku hali za raia zikiendelea kuambatana na hali mbovu za ustawi wa maisha yao? Je, ni kweli kuwa kujikwamua kwetu lazima tubebwe na mataifa ya Kaskazini?

Naweza nikakosolewa katika imani yangu; lakini ni ukweli usiopingika kuwa tofauti zetu za msingi na nchi za Kaskazini – industrialized nations katika “SUPERIORITY YA TEKNOLOJIA YA KASKAZINI”, huo ndio msingi mkuu unaotutofautisha sasa. Mengine yote nasisitiza kuwa ni matokeo tu.

Nasisitiza kuwa hatuwezi tukaelewa vizuri, kuwa changamoto ziko wapi katika uhusiano kati yetu na nchi za mataifa ya Kaskazini na nchi za Kusini bila kuelewa umuhimu na umbele wa teknolojia kama msingi wa uchumi wa viwanda.

Nasema kwa kujiamini na kwa ujasiri kuwa hapa nchini kwetu tulibahatika kuwa na kiongozi mwenye maono makubwa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alielewa sana suala hili na changamoto zake. Yeye Mwalimu aliona ulazima wa viwanda kuwa lazima vipewe nafasi ya kwanza katika vipaumbele vya maendeleo. Aidha, ustawi wa viwanda unategemea sayansi na teknolojia yenye kurutubishwa na ubunifu.

Pamoja na Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kujitahidi kujenga viwanda na kukazana kujenga uwezo wa teknolojia katika Taifa la Tanzania; sasa kwa kuangalia yanayotokea hapa nchini kwetu Tanzania, huo ndio msingi mkuu mimi kujituma kuzungumza na taifa ili tuelewe chanzo cha udumavu wa maendeleo yetu nchini Tanzania.

Nasema, tusipojituma kujua nafasi ya LAZIMA NA YA MSINGI YA KITU TEKNOLOJIA KATIKA UCHUMI WA VIWANDA, basi tutakuwa hatujaelewa maana halisi ya ujenzi na ustawi wa viwanda ‘Industrialization’!

Uhalali wangu katika kusema hivyo ni pamoja na kujiuliza maswali ya nyongeza ya msingi yafuatayo:-

Chukua taifa la Japan; je, wao wana nini? Je, wana chuma, makaa ya mawe, wanazalisha mpira, wana mafuta au gesi asilia? Kwa ujumla tujiulize tena, je, wanazo malighafi za viwandani? Jibu ni hapana!

Kwanini viwanda vyao vinaendelea kukua tena kwa kasi kubwa?

Naomba tujiulize kwa umakini mkubwa kuwa, je, sisi hapa Tanzania, kwa nini tumeendelea kubaki nyuma?

Bila kupepesa macho, jibu sahihi ni kuwa Japan wamewekeza sana katika teknolojia. Korea Kusini pia wameendelea kuwekeza katika teknolojia.

Hapa nchini kwetu Tanzania, ni muhimu tujivune kuwa tulibahatika kuwa na Mtanzania mzalendo, mwadilifu na mwenye utaifa usiotiliwa shaka; si mwingine, bali Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa taifa letu.

Juni 6, 2019, katika hotuba yake ya ufunguzi wa jengo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Rais Magufuli alifafanua vizuri wasifu wa Baba wa Taifa. Maelezo yake yaliungwa mkono vizuri na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yeye aliona vizuri sana umuhimu wa kupanga upya kabisa taratibu zitakazotumika katika kutayarisha na kuhimiza uwekezaji mkubwa katika sayansi na teknolojia.

Alihimiza viongozi wenzake wote washirikiane kuliandaa taifa kuwa na utayari wa kuwekeza katika Sayansi na Teknolojia. Kwamba lazima kama taifa tujinyime kwa kutumia vizuri rasilimali zilizopo.

Ushuhuda katika hilo ni kuwa Mwalimu Julius K. Nyerere, alianzisha Tanzania Industrial Research and Development Organization (TIRDO), Tanzania Engineering Manufacturing and Design Organization (TEMDO), Centre for Agricultural Mechanization Technology (CARMATEC) – Arusha.

Mwalimu Nyerere alikwenda hatua moja kubwa zaidi. Alianzisha mradi wa NYUMBU – ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa sababu maalumu tu, kuwa jeshini ndiko kwa uhakika kuna uwezo mkubwa wa kuanzisha, kukuza na kulea kwa kuendeleza ubunifu wa uhakika.

Huko Nyumbu, wanajeshi wetu baada ya kuhitimu Ireland – kupitia mikononi mwa Profesa Timoney hapa nchini walianza kushughulika na UBUNIFU, USANIFU NA KUUNDA MAGARI NA MITAMBO mingi/mengi – kupitia mazingira duni kabisa – from scratch!

Lengo kuu la kuanzisha hiyo miradi maalumu ya kukuza teknolojia nchini Tanzania lilikuwa ni taifa letu likatae kabisa kuwa la watwana, liwe lenye kutimiza maagizo ya wakubwa wa nchi za Kaskazini; kwa sisi kuendelea kuwa wazalishaji wa malighafi tu na kuishia kuwapelekea milima ya tani lukuki za hizo malighafi zetu.

Kwa huzuni kubwa sana, leo hii tunapozungumza juu ya Uchumi wa Viwanda, na taasisi nilizozitaja na nyinginezo; sasa tujiulize; je, taasisi hizo zinapewa vipaumbele sitahiki?

Nasema hata Institute of Productivity (IPI); iliyoanzishwa wakati wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati mmoja na Kitivo cha Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kujenga uwezo, nadharia na vitendo kwa sasa ni kama imeshazikwa.

Sina hakika kabisa kama hapa nyumbani Tanzania leo, tunayo IPI ya maana. Je, tunatembea kwa vitendo juu ya yale aliyoyakusudia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere? Nashauri kwa dhati kabisa kuwa “tuachilie mbali ulevi wa kujisifu. Sifa hazijawahi kuongeza shibe. Wewe, kama rais anaposema “Hapa Kazi Tu” wateule wake muhimu wajue kuwa mapambano ya uchumi wa viwanda sasa ndiyo yameanza.

Nasema pia kwa huzuni kubwa kuwa kama kweli uchumi wa viwanda hapa Tanzania ungejengwa kwa kutegemea uwepo wa malighafi na nishati pekee, basi Bara la Afrika na Tanzania kama sehemu ya Bara la Afrika, sisi tungeongoza sana kuliko Japan na Korea Kusini. Hilo halina ubishi tukidhamiria tu.

Pia kama uchumi wa viwanda ungetegemea fedha, basi Saudi Arabia, Dubai, Kuwait na Nigeria zingeongoza.

Wakati Rais Magufuli akitoa hotuba yake ya kupokea nafasi ya Mwenyekiti wa SADC, aliwakumbusha ma-rais wenzake, Viongozi Wakuu wa Nchi za SADC; kwamba: “Fedha si msingi wa maendeleo, bali ni matokeo.”

Kupitia Mradi wa Nyumbu, Mwalimu Nyerere alitufikisha katika hatua ya kuunda/kuzalisha magari  Nyumbu mjini Kibaha! Magari mawili ya Nyumbu yalitumika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam. Je, uwezo huo bado tunao?

Naomba Watanzania tujiulize, leo hii ndani ya karne hii ya 21 ya Sayansi na Teknolojia, ninaomba tuwe wakweli na tujiulize kwa kutambua utukufu wa ukweli kuwa; je, tunamuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuendeleza teknolojia za kujenga uchumi wa viwanda au, tunajenga uchumi wa viwanda kwa kuendelea kuwa vibarua tu na mafundi mchundo wenye kutumikia wale watakokuja kutoka nchi za nje, wao wakiwa wanamiliki mitaji na teknolojia na kuhodhi masoko?

Muda si mrefu, Rais Magufuli, kwa kujiamini na kwa ujasiri mkubwa na kwa kuwapenda Watanzania, alitamka kwa hekima na busara kubwa kuwa: “Nyumbu na Mang’ula Machine Tools lazima viwanda hivyo vifufuliwe.”

Tafadhali sasa tuongeze Kilimanjaro Machine Tools, MUTEX, MWATEX, Mwanza Tanneries, kadhalika vyuo vya ufundi, Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) n.k. vyote hivyo ni muhimu vipewe upendeleo maalumu.

Ninamuona na ninamwamini Dk. Magufuli kuwa ni Rais ajuaye thamani ya kusema na kutenda. Tafadhali tunaomba aendelee kujiweka katika mikono salama ya Mungu wetu ili kiuhalisia abarikiwe kujenga kwa uhakika uchumi endelevu wa viwanda.

Hiyo ndiyo njia sahihi ya kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hususan katika mwaka huu wa 20 bila yeye – yaani tangu afariki dunia.

•Kupitia kwake Rais Magufuli, basi; Watanzania wote tuungane katika kumwombea Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (ambaye Mungu alitupatia zawadi kwa yeye kuzaliwa Tanzania). Mungu wetu aendelee kumpa pumziko la amani, milele. Amina.

Mwandishi wa mada hii, mzee Samuel Kasori, ni Katibu Myeka mstaafu wa Mwalimu Julius K. Nyerere. Anaishi Arusha. Anapatikana kwa simu 0716267879 au 072545818.