DAR ES SALAAM
Na Anna Julia Chiduo – Mwansasu
Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia tena kuandika kwenye Gazeti letu la JAMHURI katika kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kilichotokea miaka 22 iliyopita, Oktoba 14, 1999.
Awali ya yote, ninapenda kumpongeza Rais Mama Samia Suluhu Hassan, mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa miongoni mwa wanawake 10 waliowahi kukalia kiti cha urais barani Afrika.
Wanawake wengine waliowahi kushika nafasi hiyo ni Slyvie Kiningi wa Burundi (Februari – Oktoba 1993), Ivy Matsepe-Cassaburi wa Afrika Kusini (Septemba 2005), Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia (Januari 2006 – Januari 2018) na Rose Francine Rogombe wa Gabon (Juni 2009 – Oktoba 2009).
Wengine ni Agnes Monique Ohsan Bellepeau, wa Mauritius (Machi – Julai 2012 na Mei – Juni 2015), Joyce Hilda Banda wa Malawi (Aprili 2012 – Mei 2014), Catherine Samba wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (Januari 2014 – Machi 2016), Ameenah Gurib – Fakim wa Mauritius (Juni 2015 – Machi 2018) na Sahle-Work Zewde wa Ethiopia (Oktoba 2018 hadi sasa).
Kwa Samia kushika wadhifa huu wa juu ni hatua kubwa kwa maendeleo na uhuru wa wanawake nchini na Bara la Afrika kwa ujumla. Hongera sana Rais Mama Samia.
Mwaka 1944 Mwalimu Nyerere akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, aliandika rasimu ya kitabu aliyoipa jina la ‘Uhuru wa Wanawake’.
Mwanzo wa rasimu hiyo ambayo baadaye ilichapishwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kuwa kitabu, Mwalimu anaandika: “Ikiwa ‘Uhuru wa Wanawake’ kitaamsha mioyoni mwa Waafrika wenzangu hali ya kuwaheshimu wanawake na kupenda kuzungumza jinsi watakavyofanya ili wawasaidie kutoka katika hali ya kitumwa waliyomo siku hizi, kusudi langu la kuandika kitabu hiki litakuwa limetimia, hasa tukijitahidi wote kwa vitendo kuwafanya wanawake wawe sawa na sisi wanaume katika maisha yetu ya kila siku.”
Vitabu vya dini vinasema binadamu ni uzao wa Adamu na Hawa. Mwenyezi Mungu baada ya kumuumba Adamu aliamua kumfanyizia mwenziwe aliyeitwa Hawa.
Adamu alipotoka kwenye usingizi mzito aliolazwa ili Mungu atoe ubavu wa Adamu na kumuumba Hawa,
Adamu alishangaa kumuona Hawa; akanena: “Huyu ndiyo mfupa wangu, ndiyo nyama yangu.”
Mwalimu Nyerere anasema: “Kwa maneno hayo Adamu alimuungama mke kuwa ni mwenziwe, wala si mtumwa.”
Kilichotokea baada ya hapo, shetani aliingia na kuwadanganya Adamu na Hawa, dhambi ikaingia na dhambi hiyo ndiyo iliyosababisha mwanamke kudhalilishwa na kuonekana si lolote, si chochote mbele ya mwanamume.
Katika kitabu chake hicho ambacho alikiandika miaka 77 iliyopita, anauliza: “Kuna Waafrika wangapi ambao wanaweza kusema kuwa katika mazungumzo na mawazo yao ya kila siku, huwafikiria wanawake kuwa ni sawa nao?”
Anaendelea kusema: “Kwa kawaida sisi wanaume huwatendea wanawake kana kwamba hawana akili kama zetu, na kana kwamba walikusudiwa wakae katika hali hiyo siku zote.”
Mawazo hayo aliyoyazungumzia Mwalimu Nyerere ni dhahiri hadi sasa yameendelea kuwapo ndani ya vichwa vya baadhi ya wanaume kwamba wanawake hawawezi kuwa sawa na wanaume, wala hawawezi kufanya yanayofanywa na wanaume.
Lakini, jinsi miaka ilivyokwenda, wanawake duniani kote wamedhihirisha kwamba mawazo hayo ni potofu.
Hilo la uwezo wa mwanamke, Mwalimu alilikubali tangu wakati huo na aliandika hivi: “Katika mambo yanayotegemea akili hakuna tofauti inayojulikana kuwapo kati ya wanawake na wanaume.
“Mwanamke kama Malkia Victoria wa Uingereza aliweza kutawala vizuri na kwa akili sawa na mwanamume mwingine yeyote. Mwanamke kama Joan Austin wa Uingereza aliweza kuwa mwandishi mashuhuri kama mwanamume yeyote. Mwanamke kama Joan wa Arc wa Ufaransa ni shujaa kama mwingine yeyote.”
Tangu wakati huo wa enzi za Mwalimu akiwa chuoni, na kiongozi baada ya nchi yetu kupata Uhuru tumeshuhudia wanawake wengi duniani na nchini mwetu wakionyesha uwezo mkubwa walionao katika nyanja tofauti.
Kwenye vyama vya siasa, serikalini, kwenye anga za kimataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, shuleni, hospitalini na hata majumbani wamekuwapo wanawake shupavu walioonyesha uwezo sawa na uwezo walionao wanaume na hata kuwazidi.
Ingawa wapo wanawake ambao wameonyesha kuwa hakuna kazi ya kutumia akili aifanyayo mwanamume ambayo itamshinda mwanamke, wapo wanaume ambao bado wamekuwa wakifumba macho na masikio yao na kuamini kuwa wanaume ndio wenye akili zaidi kuliko wanawake.
Pia, wapo ambao wanaendelea kuamini kwamba kwa kuwa Mungu alianza kumuumba Adamu, basi kwa ajili hiyo tu wanaume lazima wawe juu ya wanawake.
Wengine wenye mawazo finyu huamini kwamba mwanamke lazima awe chini ya mwanamume kwa sababu ya wanawake kutolewa mahari wakiolewa, na sababu nyingine wanazofikiria wao zisizo na mashiko!
Kwenye rasimu ya Uhuru wa Wanawake, akielezea juu ya jambo la mahari, Mwalimu aliona kwamba utoaji wa mahari ulikuwa ukirudisha nyuma uhuru na maendeleo ya wanawake. Aliamini kwamba kutoa mahari ilikuwa ni sawa na kumnunua mwanamke na kuzidi kumdhalilisha.
Mwalimu anaandika: “Wazungu walipoanza kuichunguza desturi hii ya kutoa mahari hawakupata neno moja katika lugha zao la kuweza kutafsiri ‘mahari’ na kupata maana yake hasa. Kwa hiyo, walilitafsiri kwa maneno mawili ambayo yanapata tafsiri hasa ya ‘mahari’. Maneno hayo ni ‘Bride-Price’ yaani ‘Bei-ya-Bibi-Arusi’.
Mwalimu aliamini kwamba mahari ni bei ya mwanamke, alistaajabu kuona watu wengi wanavyokazana kukana ukweli huu. Alisema, mahari ni bei sawasawa na bei ya kitu kingine chochote uwezacho kufikiri.
Zipo desturi nyingine ambazo Mwalimu aliona zilikuwa zikirudisha nyuma uhuru wa mwanamke na kupunguza heshima ya mwanamke kama vile ndoa ya wake wengi; kupiga wanawake; kulipa ugoni; na kadhalika.
Kwa msingi huo uwezo wa wanawake na maendeleo yao yamekuwa yakiathiriwa na mila na desturi za aina hiyo.
Pamoja na hayo, Mwalimu alikiri kwamba uovu waliokuwa wakitendewa wanawake haukutokana na ubora na uwezo wowote walionao wanaume kuwazidi wanawake.
Akasema kuwazidi nguvu wanawake kusiwafanye wanaume kuwanyima wanawake nafasi katika kazi kubwa zinazohusu maisha yetu.
Akasisitiza kwamba kazi iliyo kubwa sana katika maisha yetu ni kazi ya utawala. Ikiwa wanawake hawapewi nafasi ya kutawala, tutaendelea kuishi nusu huru na nusu watumwa – kwa maana hiyo hatutaendelea.
Mwalimu kama kawaida yake, akaasa: “….Mawazo kwamba mwanamke hawezi kwa sababu ya kuwa mwanamke na si mwanamume, tuyaondoe…”
Naam! Mwalimu Nyerere katika kipindi chote cha uongozi wa taifa letu na hata baadaye alizingatia imani aliyokuwanayo kuhusu uwezo wa wanawake.
Na ndiyo maana hadi leo harakati zinaendelea kisiasa na kijamii kuwafanya wanaume na hata wanawake wasioamini juu ya usawa wa wanawake na wanaume, wafute mawazo hayo potofu.
Kwa miaka yote tangu tupate Uhuru, maono ya Mwalimu Julius Nyerere kuhusu uwezo wa wanawake yametufikisha hapa tulipo, ambapo tuna Rais mwanamke na idadi kubwa ya wanawake katika ngazi mbalimbali serikalini, kwenye mashirika ya umma/binafsi, shuleni, hospitalini, akina mama/bibi-ntilie na akina mama walio majumbani, wakifanya kazi nzuri ya kujenga taifa letu.
Tutaendelea kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kufanya kazi kubwa kuhakikisha kuwapo kwa uhuru wa wanawake na kuthibitisha pasipo shaka kwamba wanawake wanaweza!
0655774967