Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mtendaji Mkuu Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse amesema kuwa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba ni fursa ya kunadi fursa zinazopatikana katika Sekta ya Madini

Amesema hayo, leo Julai 3, 2024 alipotembelea na kukagua Banda la Wizara ya Madini sambamba na Taasisi zake katika Maonesho hayo ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa zipo fursa nyingi katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na Uwekezaji katika Utafiti na Uchimbaji wa Madini sambamba na fursa za utoaji huduma katika maeneo mbalimbali ambayo kuna miradi ya madini ikiwemo vyakula na usafiri.

Ametoa rai kwa wawekezaji na wananchi kutembelea mabanda ya Wizara ya Madini na Taasisi zake ili wapate kujifunza fursa zilizopo katika Sekta sambamba na kujifunza kuhusu mnyororo mzima wa shughuli za uchimbaji madini.

Wizara ya Madini na Taasisi zake ikiwemo STAMICO, Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST),Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) kwa pamoja wanashiriki katika Maonesho hayo.

Maonesho hayo yamezinduliwa leo na Rais wa Msumbiji, Felipe Nyusi akiambatana na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkuu huyo wa nchi ya Msumbiji yuko nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku 4.

Maonyesho hayo yameanza tangu Juni 28 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2024.