Habari kaka Jackton,

Nimebahatika kusoma makala yako katika Gazeti la JAMHURI toleo Na. 106 la tarehe 22 hadi 28 Oktoba. Makala hayo yana kichwa cha habari “Rais dikteta atatutoa hapa tulipo”. Katika makala hiyo umeitendea haki heading yako na nakupongeza kwa hilo.

Lakini katika makala hayo kuna sehemu umeandika “Tunao mahakimu na majaji wanaofanya kazi katika mazingira magumu, lakini wanatenda haki”.

Ndugu, hapa umeongea ukweli usiopingika kabisa, lakini umekosea sana kuweka neno ‘jaji’ hapo. Hivi unajua tofauti ya maslahi anayopata jaji na yale anayopata hakimu ndugu yangu? Hapo ulitakiwa tu kusema “tunao mahakimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu lakini wanatenda haki”.

 

Jaji hana maisha magumu katika nchi hii ndugu. Na kumlinganisha hakimu na jaji katika utendaji kazi mgumu, unamkosea sana hakimu huyu.

Kama ulikuwa hujui, hakimu anafanya kazi katika mazingira magumu sana na ukiona katenda haki, basi ujue Mungu ameingilia kati yaani utu umemjia. Hakimu huyu hana posho yoyote zaidi ya kutegemea mshahara wake, halipiwi chochote — iwe nyumba, usafiri, ulinzi wake, umeme, maji nk.

Hivi vyote jaji anapata na ziada pamoja na mshahara mnono ambao ni zaidi ya mara kumi ya basic salary ya hakimu mkazi, na zaidi ya mara 16 ya take home ya hakimu huyo.

Hivi, katika mazingira ya kukosekana kwa usawa baina yao, unatarajia hakimu asichukue rushwa kaka? Unatarajia hakimu awasilishe maduhuli ya Serikali serikalini kama sheria inavyosema?

Majaji wametengenezewa hadi sheria kwa ajili ya kuhakikisha maslahi yao. Soma Sheria namba 16/2007, Judges (Remuneration and Terminal benefits) Act.

Hebu pitia sehemu ya pili ya sheria hii, uone jinsi jaji anavyopendelewa huku hakimu akionekana kama takataka katika utumishi wa Mahakama.

Lakini jiulize, ni kazi ipi kubwa anayoifanya jaji ambayo hakimu haifanyi? Kuna utofauti gani mkubwa wa kimajukumu kati ya hakimu na jaji? Kwa nini hakimu hatendewi haki kiasi hiki na bado jamii inamtarajia atende haki?

Mahakimu wamebakia ni watu wa kuomba Mungu walau itokee safari tu ili walipwe hizo posho kukidhi mahitaji yao. Wakati huo, jaji akienda kwenye session analipwa si chini ya shilingi laki nane, kiasi hiki ni zaidi ya mshahara (basic salary) wa Hakimu Mkazi. Sasa katika mazingira haya jaji anafanya kazi katika mazingira yepi magumu? Lakini nani wa kumtetea hakimu katika hili? Ni nani atakayemzuia hakimu asichukue rushwa kama hali yenyewe ndiyo ipo hivi?

Katika hili hatuwezi kuilaumu Serikali Kuu wala Bunge, majaji ndiyo wanaotuumiza mahakimu, wanachoangalia wao ni maslahi yao tu, hakuna jaji hata mmoja anayemtetea hakimu.

Mahakama ni moja ya mihimili ya Taifa na bahati nzuri ina wafanyakazi wachache, kiasi kwamba kama majaji wangekuwa wapo kwa maslahi ya wote, mahakimu wangekuwa katika hali nzuri tu.

Jiulize, askari polisi hadi yule mwenye cheo cha chini kabisa, analipwa posho katikati ya mwezi, lakini hakimu anayetoa amri za kuwafunga na kuwaadhibu wauza unga, majambazi, wabakaji, mafisadi, nk, hana hata posho ya kulipia maji huku jaji akipata kila kitu pamoja na ulinzi wa uhakika na usafiri pia.

Ninaongea hivi si kwa kusimuliwa, ninayaishi haya maisha. Napenda kutenda haki na naitenda haki hiyo, lakini nina kinyongo moyoni kwa kuwa ndani ya taasisi hii inayotakiwa kuaminiwa, sitendewi haki hata kidogo.

Wakubwa wameshiba tayari, hawanioni mimi huku, na wakati huo huo wanasisitiza niwe mwadilifu. Nitakuwaje mwadilifu wakati ninyi hamnijali? Napenda kazi yangu, tena sana, lakini nakwazwa na waliyo juu yangu.

Napenda haya yafahamike kwa umma labda tutatendewa haki, ili na sisi tuirejeshe haki hiyo kwa jamii kupitia uamuzi wetu. Mimi ni hakimu, kama nilivyosema, waweza fanya uchunguzi huko juu ili ujiridhishe na jinsi majaji wanavyoishi peponi huku hakimu anayetekeleza wajibu ule ule akipata taabu kama vile si mtu muhimu katika mhimili huu.

Wengi wapo kimya si kwa kuridhika, bali kuogopa kufukuzwa kazi, maana tunaambiwa huku hakuna migomo na tunatakiwa kuwa na maadili kaka. Huku ni maumivu makali kwa mahakimu na chanzo cha maumivu hayo ni majaji na ndiyo maana Mahakama haitakuja kubadilika kamwe, na rushwa haitaisha.

Na napenda ishike nafasi ya kwanza kwa rushwa nchini kwa kuwa mahakimu wanajengewa mazingira hayo. Kuhusu makarani, wahudumu, walinzi na madereva, nenda kawaulize mwenyewe kaka.

Hakimu Mkazi

Kwa sababu za kitaaluma, mwandishi wa makala hay ameomba jina lake lihifadhiwe.