KIGALI, RWANDA
Unapaswa kuwa na upendo ili upone; ndivyo anavyoamini mwanamke huyu ambaye si tu kwamba amekwisha kumsamehe mtu aliyemuua mumewe miaka 28 iliyopita, lakini pia amekubali kijana wake kumuoa binti wa aliyekuwa ‘mbaya wake’!
Mwanamke huyu, Bernadette Mukakabera, amekuwa akihadithia yaliyomkuta kama sehemu za juhudi za Kanisa Katoliki kutafuta upatanishi miongoni mwa jamii iliyosambaratika mwaka 1994 pale watu 800,000 walipouawa ndani ya siku 100 tu.
“Watoto wetu hawana chochote cha kufanya kwa yaliyotokea. Wamejikuta wakipendana na hakuna kitu kinachoweza kuzuia watu kuanguka katika mapenzi,” anasema Bernadette akizungumza na BBC.
Yeye na mumewe, Kabera Vedaste, wanatoka katika jamii ya Kitutsi, waliokuwa walengwa wa mauaji makubwa yaliyofuatia baada ya ndege iliyombeba aliyekuwa Rais wa Rwanda, Juvenali Habyarimana, kutunguliwa Aprili 6, 1994.
Habyarimana anatoka katika jamii ya Wahutu na saa chache tu baada ya kuuawa, maelfu ya Wahutu waliokuwa na chuki kwa miaka mingi, wakaanzisha mauaji ya kupangwa – wakiwalenga majirani zao Watutsi nchi nzima.
Mmoja wa Wahutu walioshiriki mauaji haya ni Gratien Nyaminani, aliyekuwa akiishi na familia yake jirani kabisa na Bernadette huko Mushaka, magharibi mwa Rwanda. Wote walikuwa wakulima.
Baada ya mauaji kusitishwa na ‘waasi’ wa Kitutsi kushika madaraka, maelfu ya watu waliotuhumiwa kushiriki kwenye mauaji wakakamatwa na kuwekwa kizuizini.
Mmoja wao ni Gratien, aliyekamatwa na kushitakiwa mbele ya moja ya mahakama za kijamii, ‘gacaca’, zilizoandaliwa kwa makusudi hayo.
Wakati wa kusikilizwa kwa mashauri hayo ya kila wiki, jamii ilipewa nafasi ya kukutana ana kwa ana na watuhumiwa na kutoa ushahidi kuhusu ni nini hasa kilichotokea na namna ilivyokuwa.
Mwaka 2004, Gratien alimweleza Bernadette namna alivyomuua mume wake, kisha akamuomba msamaha na papo hapo, mama huyu akaamua kumsamehe.
Hii maana yake ni kwamba hakuwa tena na sababu ya kutumikia kifungo cha miaka 19 jela; isipokuwa kifungo cha nje cha miaka miwili kuitumikia jamii.
‘Nilitaka kusaidia’
Kwa miaka 10 aliyokuwa kizuizini kabla ya kuomba radhi hadharani, familia ya Gratien ilikuwa ikitafuta namna ya kutibu majeraha na suluhu kwa Bernadette na mwanaye, Alfred, aliyekuwa na umri wa miaka 14 baba yake alipouawa.
Binti wa Gratien, Yankurije Donata, aliyekuwa na umri wa miaka tisa wakati wa mauaji ya kimbari, akawa akienda nyumbani kwa Bernadette kusaidia kazi zilizopo nyumbani.
“Niliamua kuwa ninakwenda kumsaidia mama yake Alfred kazi za nyumbani na hata za shambani, kwa kuwa hakuwa na mwingine wa kumsaidia, ukizingatia kuwa ni baba yangu aliyehusika na mauaji ya mume wake,” anasema Donata na kuongeza: “Ninadhani ni wakati huu nilipokuwa ninamsaidia mama yake kazi ndipo Alfred aliponipenda.”
Maneno hayo ya kutoka kwa Donata, yalimgusa sana Bernadette, na anasema: “Alikuwa akinisaidia huku akifahamu kabisa kuwa ni baba yake ndiye aliyemuua mume wangu. Alijua kwamba sikuwa na mtu wa kunisaidia, kwa kuwa Alfred alikuwa akisoma shule ya bweni.
“Nilipendezwa sana na upendo wake pamoja na tabia yake – na ndiyo sababu wala sikupinga yeye kuwa mkwe wangu.”
Lakini kwa upande wa Gratien, haikuwa rahisi namna hiyo – kwanza alisita na kuogopa alipoelezwa kuhusu mapendekezo ya ndoa.
“Alikuwa akihoji mara kwa mara ni namna gani na kwa nini familia aliyoikosea kwa kiwango kikubwa namna ile; ni nini inakitaka kutoka kwa binti yake?” anasema Donata.
Hata hivyo, juhudi zikafanyika hadi wakafanikiwa kumshawishi na yeye kutoa baraka zake, hasa kwa kuwa Bernadette aliweka wazi kwamba hana kinyongo wala nia mbaya dhidi ya Donata.
“Sikuwa na chuki ya aina yoyote kwa mkwe wangu kutokana na matendo ya baba yake,” anasema Bernadette na kuongeza:
“Niliona kabisa kwamba atakuwa mke mwema kwa mwanangu na mkwe mwema kwangu, kwa kuwa ananifahamu kuliko mwingine yeyote. Nikamshawishi mwanangu amuoe.”
Wawili hawa wakafunga ndoa mwaka 2008 katika Kanisa Katoliki karibu na kwao.
Ni hapo ndipo Gratien alipokiri na kutubu mbele ya waamini baada ya miaka miwili nyuma, kumaliza adhabu yake ya kuitumikia jamii; akaomba asamehewe.
‘Hakuna mapatano, hakuna Komunio Takatifu’
Kanisa lilikuwa likifanya juhudi kubwa ya kuziunganisha jamii zilizotengana kwa chuki kwenye eneo hilo.
Padri Ngoboka Theogene wa Jimbo la Cyangugu, anasema watu wengi walikubaliana na mpango wake wa upatanisho hivyo kufanya madhehebu mengine nayo kuiga juhudi hizo.
Makanisa haya yanafahamu kwamba watu hawana chaguo, ila kuishi pamoja; na kwamba ni muhimu kufanya hivyo kwa amani na uelewano mkubwa.
“Wale waliokuwa wakituhumiwa kushiriki mauaji ya kimbari hawaruhusiwi kushiriki sakramenti hadi pale watakapofanya upatanisho na familia zilizoathirika,” anasema Padri Ngoboka.
Mapatano ya mwisho hufanyika hadharani kwa wahusika wawili kusimama pamoja.
“Waathirika huwapa mikono watuhumiwa kama ishara ya msamaha,” anasema.
Majuzi, watu walikusanyika Mushaka kufanya kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya kimbari na kujifunza namna ya kuishi pamoja, miaka michache baada ya kifo cha Gratien.
“Tunapozungumzia mabadiliko, hatuna maana ya kubadili rangi ya ngozi, bali kubadilisha tabia mbaya,” anasema mmoja wa wawezeshaji wa tukio hilo, Apiane Nangwahabo, kutoka Parokia ya Mushaka.
“Mabadiliko ya moyo ni muhimu kabla ya kuamua kuishi maisha matakatifu.”
Ni hapa ndipo Bernadette alipozungumzia ndoa ya mwanaye na binti wa muuaji wa mume wake.
“Ninampenda sana mkwe wangu, wala sijui ningeishi vipi bila yeye kuja kunisaidia baada ya kifo cha mume wangu,” anasema.
Anasema anatamani kuyaona maisha ya Alfred na Donata yakiwatia moyo watu wengine wa kutafuta na kutoa msamaha.