Wazaramo wana misemo mingi katika lugha yao. Kati ya hiyo ni msemo usemao “Wose tozenga ing’anda imwe, habali tugombele lumango?” Katika tafasii sahihi ya Kiswahili “Wote tunajenga nyumba moja, kwa nini tugombee fito?” Nyumba ninayo kusudia kuizungumzia ni nchi yetu Tanzania.
Ndani ya nyumba hiyo wamo wananchi wakulima na wafanyakazi, wasomi na wasio wasomi, matajiri na masikini, viongozi na wanaoongozwa, wanasiasa na wasio wanasiasa na wengine kadhalika. Wote wana haki moja ya kuishi huru ndani ya nyumba hiyo na kutumia rasilimali iliyoko, kwa mujibu wa sheria na kanuni walizojiwekea; lau kama nyumba yenyewe haijakamilika ujenzi.
Haki hii ina mwenza wake Uhuru. Wote wanatawaliwa na kulindwa na sheria. Uhuru usio na mipaka ya sheria ni sawa na uwenda wazimu, ambao ni sawa na Haki isiyo na sheria ni ghasia, vurugu na mifarakano.
Niliyosema si mapya. Bali naweka msisitizo kuhusu thamani ya haki na uhuru wa kila mtu katika kuishi, kufanyakazi, kucheza, kuzungumza hata kulala usingizi na kula chakula. Hapo ndipo tunapopata utu wa mtu ndani ya mamlaka na madaraka aliyenayo.
Hivi sasa Wananchi tunashuhudia mtikisiko wa kisiasa na kiuongozi ndani ya nyumba yetu tunayojenga kati ya chama cha siasa – CHADEMA na chama cha siasa – CCM, pamoja na Serkali yake. Mtikisiko huu una dalili ya kutenguka amani, utulivu na mshikamano wa ujenzi wa nyumba salama kuwekwa rehani au ahera. Kutokana na kauli za viongozi wajenzi wa nyumba.
Kauli iliyotolewa na CHADEMA ya kufanya maandamano na mikutano ya hadhara nchini kote, kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu, kuelezea na kupinga kauli na vitendo vya Serikali vya kuminya demokrasia, kuzuia mikutano ya hadhara na kusimika udikiteta nchini, inagonganisha vichwa vya wananchi.
Kauli na msimamo huo usio na kikomo, umejibiwa na CCM kuwa haukubaliki na kupingwa kufanyika kwa sababu si kweli demokrasia inaminywa. Chadema wanahofu tu na hawapendi kuona rushwa na ufisadi unaangamizwa nyumbani. VIchwa vya Wananchi vinazunguka.
Serikali nayo imejibu huu si wakati wa kupiga siasa. Ni wakati wa kufanya kazi na kujenga uchumi. Taifa kwanza chama baadaye. Si wakati wa kujaribu nguvu za Serikali. Dhana hiyo iondolewe. Atakaye jaribu atakiona. Hapo tena vichwa vya wananchi vimevurugika.
Mtikisiko huo unayumbisha ujenzi wa nyumba tunayojenga kwa sababu kila mtu anajiona ana haki ya kujenga na mwenzake hana uwezo na haki ya kujenga. Mgongano wa mawazo hayo unafungua mlango wa kugombea fito na mijengo na kila mtu ataingia uwajani kuchukua kiasi cha fito anachoweza kujengea na kuhodhi nafasi ya ujenzi.
Septemba Mosi, haiko mbali iko kwa jirani. Wakati wa kuepuka kugombea fito ni sasa. Kama wasemavyo Wavuvi; “Maagano ni nchi kavu, baharini ni kuvua.” Baharini (majini ) si mahali tena pakugawana chambo, mishipi au nyavu na kupanga nani wa kupiga makasia, uvuta nyavu, au kutega dema.
Huu ni wakati wa viongozi wote wa Chadema, CCM na Serikali kutafakari upya kauli zao ili tusiingie katika zoezi la “ kugombela lumango “ Utakuwa si uamuzi wa hekima na busara kwa watu kama sisi wenye sifa za upendo, udugu na umoja. Kelele zinazopigwa sasa hazijengi zina bomoa utu wetu.
Ushauri wangu nawaomba, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Jumbe Safari na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee wetu Phillip Mangula mkutane pamoja wenyewe, si wasaidizi au wakilishi wenu kuzungumzia sakata hili.
Naamini na nina uhakika usio na mashaka, uzoefu wenu katika sheria na siasa, uongozi na hekima, uzalendo na uadilifu mlio nao mnaweza pasi na shaka kuepusha shari iliyoko mbele yetu. Msinogezwe na sauti tamu zitolewazo na viongozi wanao shabikia kugombea fito.
Namalizia kwa kusema nyumba yetu bado yahitaji kukandikwa na kupauliwa kabla ya kuwekwa milango na madirisha. Hatuwezi kukandika udongo wala kupwaua nyasi/ makuti/ mabati kama mijengo na pau hazijafungwa fito.
Fito ni muhimu kuhimilisha kuta na paa. Ndipo nasi tunaweza kuishi ndani ya nyumba hii katika hali ya amani na usalama. KUTANENI INAWEZEKANA.