Kwa karibu miezi sita sasa, siasa za Jimbo la Bukoba mjini zimegeuzwa siasa za chuki, kutishana, fitina, kuchambana, kulaumiana, kuonesha umwambwa, uwezo wa kifedha, dharau, ubaguzi na ujenzi wa matabaka yanayosigana katika jimbo hili.
Msuguano chanzo chake ni siasa za kutafuta ‘kula’ na ‘Uheshimiwa’ miongoni mwa wanasiasa hali inayodumaza maendeleo.
Wanasiasa wanaosuguana ndani ya CCM ni Mbunge wa Jimbo la Bukoba, Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Aman. Kila mmoja ana kundi lake.
Dk. Kagasheki si ‘mzawa’ wa jimbo hili. Anatajwa kuwa ni mtu wa kutoka nchini Uganda aliyehamia Tanzania na kujichimbia wilayani Karagwe, wakati wa ujana wake ambapo taarifa zinaeleza kwamba alipewa heshima ya kukimbiza Mwenge wa Uhuru nchini Tanzania akiwa bado kijana na huo ndiyo uliokuwa mwanzo wa kuingia katika siasa za Tanzania.
Dk. Amani aliwahi kuwa Mwenyekiti Vijana wa CCM Mkoa wa Kagera na baadaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera. CCM walimfukuza, akanyang’anywa uraia na akajichimbia kwenye biashara kwa kuanzisha shule za masomo kwa mchepuo wa Kiigereza ziitwazo Amani. Alianzisha pia biashara ya usafiri wa baiskeli, akiita ASECDO.
Alikuwa na utitiri wa baiskeli ambapo aliwagawia vijana baiskeli wasafirishe abiria kwa malipo na kila jioni wawasilishe ujira kwake. Kampuni hiyo ilikufa baada ya vijana kujua siri na kuachana na baiskeli za Amani alizokuwa amewanunulia wakanunua baiskeli zao na kufanya shughuli hiyo wao.
Dk. Amani alirejea katika siasa mwaka 2010 kwa kugombea udiwani kata ya Kagondo ambako amejenga shule ya mchepuo wa Kiingereza.
Balozi ni mzaliwa wa Bukoba Mjini, lakini ametumia muda mwingi nje ya nchi. Alikuwa mwakilishi wa Tanzania nchini Uswizi na alirejea nchini mwaka 2004 akiwa ‘ameitwa’ na wana-CCM kuanza maandalizi ya kumng’oa Lwakatare wa CUF.
Kabla ya kurejea nchini, Kagasheki alianza kufadhili miradi kadha wa kadha ikiwamo ujenzi wa vyumba vya madarasa, kulipia watoto ada, kufunga taa za barabarani na mingine kupitia kampuni ya Kananga Investment.
Kagasheki aliingia rasmi katika siasa za Bukoba mwaka 2005 wakati huo akiitwa ‘mkombozi’ na wana-CCM wenzake wakiongozwa na Mzee Pius Ngeze na Dk. Deodorus Kamala, aliyekuwa Mbunge wa Nkenge. Kagasheki alishinda ubunge kupitia CCM kwa kumwangusha Lwakatare wa CUF.
Akiwa mbunge kati ya 2005 na 2010, Kagasheki na wana-CCM wengine wakiwamo madiwani kutoka chama hicho, hawakuelewana vema na Meya wa Bukoba, Samuel Ntambala Luangisa, kwa jinsi alivyokuwa akitekeleza Ilani ya CCM, hivyo mipango ya kumwangusha ilianza.
Madiwani kwa kushirikiana na wana-CCM wengine waliamua kumtafuta Dk. Amani agombee udiwani kupitia Kata ya Kagondo hatimaye ‘wampitishe’ kuwa Mstahiki Meya. Nakumbuka madiwani wote walipelekwa Chato kupanga mbinu za kumng’oa Luangisa na kumwingiza Aman. Nyuma ya huu mchezo alikuwapo Kagasheki.
Hivyo, kauli ya Kagasheki ya kwamba ‘alimchonga’ Meya ni kweli kabisa wala hakuna ubishi katika hili labda kama mfumo wa uwasilishaji haukuwa sawa. Kwa nguvu ya Kagasheki, Dk. Amani alimwangusha Luangisa na kushinda umeya.
Kagasheki, Amani na mipango ya maendeleo
Kupitia kampeni za 2010 na ilani ya CCM wanasiasa hawa kwa pamoja walipanga kuifanya Bukoba kuwa Jiji kabla ya 2020 na pia kupitia vipaumbele vya halmashauri, ahadi za mbunge, ahadi za rais za 2010 na Ilani ya CCM walibuni miradi kadhaa ambayo waliamini ikitekelezwa, Bukoba ingepiga hatua kimaendeleo na ikaongeza mapato ya halmshauri.
Miradi waliyopanga kutekeleza ni ujenzi wa kitegauchumi, upimaji wa viwanja 5,000, ujenzi wa stendi ya mabasi Nyanga, mradi wa kuosha magari, ujenzi wa soko kuu, uendelezaji makazi Kashai na Miembeni, ujenzi wa chuo cha ualimu, ujenzi wa kituo cha maarifa na ujenzi wa bwawa la maji kwa ajili ya utalii.
Katika utekelezaji wa miradi hii, wanasiasa hawa walikuwa pamoja na kati yao hakuna asiyejua faida za kutekeleza miradi hiyo kwa maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.
Halmashauri ilianza utekelezaji wa miradi hasa miradi ya ujenzi wa soko kwa kubomoa lililopo na upimaji wa viwanja 5,000 ambapo mpango huu ulipanuliwa kupima viwanja vya kutosheleza watu 40,000 yaani sawa na viwanja 8,000 katika kata saba.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Khamis Kaputa, anasema katika hatua hii halmshauri iliandaa andiko la mradi wa viwanja kwa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, kupata fedha kwa ajili hiyo lakini hawakupata, hali iliyowafanya kutafuta wabia.
“Tuliamua kuwapata Mfuko wa Dhamana Tanzania (UTT) ambao tuliingia makubaliano nao watoe fedha zipatazo bilioni 2.6 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo na mkataba tulioingia Juni 20, 2011 upo katika mfumo wa ushirikiano (joint venture),” anasema Kaputa.
Kwa mujibu wa Kaputa, viwanja vingeendelea kuuzwa hadi Februari 2013 ambapo watafunga mradi na kugawana faida kwa uwiano wa asilimia 60 kwa UTT na asilimia 40 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba. Halmashauri inatarajia kupata gawio la sh bilioni 2.
Halmashauri ilizungumza na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) kuhusu kufadhili ujenzi wa soko ambapo Aprili 16, 2012 waliingia mkataba.
Kaputa kabla ya kubomoa soko la sasa ilikuwa ni lazima kuwatafutia maeneo mbadala wafanyabiashara walioko katika soko la sasa. Maeneo yaliyopendekezwa ni jengo la CCM Mkoa, soko la Nyakanyasi, machinjio ya zamani na eneo la CCM Miembeni. Hii ilikuwa itekelezwe kabla ya Agosti 2012.
Malalamiko juu ya miradi
Kabla ya malalamiko kuanza, tulishangaa kuona kila diwani wa Manispaa akiendesha gari na tulipouliza wakadai kwamba meya ‘amewafanyia’ mpango wa mkopo wa Sh milioni 10 kila mmoja ili wapate usafiri.
Baadaye madiwani wote wakapelekwa kutalii Dodoma kwa gharama za meya. Hapa tukasema mambo si ndiyo hayo! Wapiga kura wanasota, wapigiwa kura wanakula bata!
Lakini punde madiwani wakaanza kulalama kwamba meya sasa amekuwa ‘jabali’ kwamba ameanza kuwatambia kuwa ‘Yeye ni halmashauri na halmashauri ni yeye’ na wengine wakaenda mbali zaidi kwamba ‘anakula’ peke yake.
Hazikupita siku meya akafanya mahojiano na Redio Kasibante ya mjini hapa, Mei 18, 2012 na kumdhalilisha mbunge kupitia Chadema, Conchester Lwamlaza, kwa kumwita malaya, baadaye katika kikao cha Julai 2011 akamdhalilisha Samuel Luangisa kwa kumwamuru kama mtoto akisema “kaa chini wewe”.
Kwa kuwa madiwani wote walikuwa kitu kimoja katika uibuaji, upangaji na utekelezaji wa miradi husika taratibu wakaanza kutengeneza makundi. Yakawapo makundi yanayofaidika na yasiyofaidika na utekelezaji wa miradi. Kundi linalodaiwa kufaidika ni lile lililomo katika Kamati ya Uchumi na Fedha. Hapa madiwani bila kujali vyama wanakotoka wengi wakasaliti kambi! Wakaasi!
Malalamiko ya wananchi juu ya miradi
Kwa kuwa madiwani hawa ndiyo waliokuwa ‘jikoni’, walijua kila kitu hivyo waliwandaa wapiga kura wao kulalamikia baadhi ya miradi na vipengele kadhaa ambavyo wao pasipo kuwa na shaka, walijua vilifanywa kinyume na taratibu za uendeshaji wa halmashauri kwani walishiriki kufanya hivyo lakini wakijua ikitokea tatizo wataruka.
Katika mradi wa soko, walijitokeza madiwani wanaolalamika kwamba hakuna zabuni iliyotangazwa kuipatia kandarasai kampuni ya OGM kuwa mkadarasi mshauri na kulipwa Sh milioni 522 iandae andiko la mradi. Kwamba OGM haikushindanishwa na kampuni nyingine kama taratibu zilivyo bali ililetwa na Meya.
Kumbuka wamiliki wa vibanda sokoni asilimia kubwa ni madiwani wale wale na taarifa za wafanyabiashara kufungua kesi mahakamani kupinga soko lao kuvunjwa bila kupewa sehemu mbadala nyuma yao kulikuwa na madiwani hawa. Mkurugenzi Kaputa amekiri kwamba watawajengea maeneo mbadala.
Madiwani wanamwomba Kagasheki amuonye meya
Baadhi ya madiwani kwa kutazama mwenendo wa meya na ‘kufifia’ kwa mazingira yao kufaidika na miradi waliamua ‘kumshtaki’ kwa ‘mkubwa’ wake Kagasheki na taarifa zilizopo ni kwamba meya aliwahi kwenda kwa Kagasheki kuungama. Taarifa zinasema meya baadaye aliona ni dharau sana kuungama kila wakati.
Akaona ni bora ajitoe mhanga kwa kufanya kazi bila kuingiliwa na ama madiwani au Kagasheki. Kwamba nani amweheshimu mwenzake katika lipi na wapi! Wote si wanasiasa? Huu ndiyo uliokuwa mwanzo wa unamwaga mboga nami namwaga ugali!
Kagasheki anaongea wazi wazi kwenye mikutano, huku meya akiwasaka viongozi wa juu ya chama na mkoa kuomba msaada.
Kagasheki pia anatumia Redio yake ya Kasibante FM kuelezea mipango ya kuendeleza mji, meya anatumia Redio Vision FM kuelezea mipango hiyo hiyo na wakati mwingine wanatofautiana kwa lengo la kupata ‘wafuasi’. Katika hili redio hizi zinasaidia kukuza mgogoro.
Pia kupitia vijiwe zikajitokeza tetesi kuwa meya anataka kugombea ubunge 2015 ‘kumpora’ jimbo Kagasheki kwa sababu anatekeleza miradi ya maendeleo hasa ujenzi wa soko. Inadaiwa Dk. Amani hakuwahi kutamka popote maneno haya.
Mipango ya kumg’oa meya
Baada ya meya kuwa ‘ngangari’ kwa kukataa kuungama kila wakati kwa ‘aliyemchonga’ na kukataa kukubali baadhi ya matakwa ya madiwani anaowaongoza. Hapa inadaiwa kuna walioonekana kufaidi zaidi ya wenzao. Sasa wale wasiofaidika sana waliandaa mipango ya kummaliza kisiasa. Walimtumia Kagasheki kama kamanda mkuu wa ‘Operation Ondoa Meya’ (OOM).
Meya naye aliandaa majeshi yake kwa kuunda kikosi cha ‘Operation Bakisha Meya (OBM) kwa kusaidiana na Chief Kalumuna, Diwani wa kata ya Kahororo (CCM).
Awali walikuwa ni CCM pekee waliopanga kumng’oa lakini hawa wanawashawishi wengine wa upinzani kutoka CUF. Madiwani wa Chadema hawakusaini kwa sababu ambazo bado hazijulikani kwani hawakuwa upande wowote ingawa katika dakika za mwisho walishajiunga na kundi la OOM katika hatua ya mwisho ya kupiga kura za kumuondoa.
CCM Mkoa, Taifa inaingilia kati
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa kupitia Kamati ya Siasa ya Mkoa, imefanya vikao zaidi ya vitatu kujadili ‘siasa’ za watu hawa na mara zote wakidai kuwa mgogoro umalizwe ndani ya vikao vya wilaya na kuwa haina tija kwa chama.
Lakini nao nguvu ya OOM inawazidi kimo kwani dalili za meya kuondolewa zinaonekana wazi. Wanahofia Halmashauri kwenda Chadema au CUF. Wanaamua kuomba msaada kutoka CCM Taifa ambako nao wamemtuma Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Philip Mangula, kutafuta suluhu.
Makosa aliyofanya Mangula
Mangula baada ya kusikiliza pande mbili ameshindwa kujua chanzo ni nini. Viongozi wa mkoa ama walimficha chanzo au hawajui. Naye hakufanya jitihada kujua chanzo cha mtafuruku huu. Yeye akawatuhumu Kagasheki, meya na madiwani kwa mipango ya kuua chama. Analalama kwamba mipango ya kumuondoa meya haina tija kwani itasababisha CCM ipoteze halmashauri.
Yeye katika hili anajikita kwenye chama kwanza mengine baadaye. Alipowauliza madiwani wote walikiri kufahamu utekelezaji wa miradi lakini hakutaka kujua waligota wapi kwa kumsaliti meya.
Akatangaza rasmi kwamba meya hataondolewa na kwamba madiwani wa CCM waliotia saini za kumkataa meya wakishirikiana na wapinzani wafute mara moja na kama hawataki warejeshe kadi zao kwake mara moja. Kambi ya OBM inashangilia ushindi! Kambi ya OOM inasononeka, inarudi msituni kujipanga! Itarejea na mbinu ipi hatujui.
Hapa Mangula hakutazama maslahi ya wananchi na hatima ya miradi husika kwani tangu aondoke hali ni mbaya kuliko mwanzo. Uhasama umekuwa mkubwa katika makundi haya yanayosigana. Utekelezaji wa miradi umekwama. Watendaji kila siku wanajadili ‘siasa’ hizi.
Madiwani wanaumbuana kwa tuhuma mbalimbali. Hali ni mbaya kwa CCM katika jimbo hili kuliko wakati wowote. Mangula alikata matawi ya mti katika harakati za kuondoa mti wenyewe, badala ya kuchimba mizizi na sasa matawi yanaanza kuchipuka tena. Kwa ufupi, Mangula amezima moto kwa petrol Bukoba.
Namna ya kumaliza mgogoro
Ikumbukwe viongozi hawa hawagombei madaraka wala fedha hapana, wanachogombania ni heashima! Nani amuheshimu nani katika lipi, vipi na wapi basi! Taarifa zilizopo ni kwamba meya amemdharau Kagasheki. Tatizo liko hapo. La msingi hapa ni je, Kagasheki anataka heshima kutoka kwa meya iweje na akiipata atafaidikaje, hakuna anayejua.
Katika mji tumekuwa na ‘majogoo’wawili. Bila jogoo moja kukubali kushindwa mgogoro huu hautakwisha kamwe. Hata meya akiondolewa wananchi wataendelea kusota tu.
Suluhu pekee ya kumaliza mgogoro huu ni CCM Taifa au viongozi wa juu wenye heshima zao kuwaita viongozi hawa wawili – Kagasheki na Dk. Amani – na kuwapatanisha, vinginevyo Wakurya wanasema ‘amang’ana gasarikile’ (mambo yameharibika).
Mwandishi wa makala haya anapatikana kupitia: