Kama ilivyotarajiwa, manabii wa vurugu za Loliondo na Ngorongoro kwa ujumla wao wamejitokeza kupaza sauti za uchonganishi wakijitahidi kuhalalisha uongo.
Kwa wanaojua habari ya eneo hili hawashangai, maana kelele za ‘tunaonewa, tunapokwa ardhi yetu, tunapigwa nk’ ni filimbi nzuri sana inayoamsha masikio na mifuko ya wafadhili.
Ukiona Ngorongoro kumetulia, ujue akaunti za NGOs bado zina salio la kutosha. Salio likipungua kutatafutwa namna yoyote ya kuhalalisha maombi ya fedha kutoka kwa wafadhili. Haya yanajulikana kuanzia kwenye vyombo vya usalama vya nchi hadi kwa wananchi wa kawaida.
Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) imeshatoa taarifa ya kifo cha eneo hili ambalo ni moja kati ya maeneo ya Urithi wa Dunia. Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenye ripoti zake imeshaonya kutoweka kwa Ngorongoro.
Wataalamu wa uhifadhi wa ndani na nje ya Tanzania wameshaona kifo cha Ngorongoro kimeshawadia. Watalii ambao nchi inatumia rasilimali nyingi kuwavuta waje kutalii nchini, wakifika Ngorongoro wanakutana na kondoo, punda vihongwe, ng’ombe waliodhoofu na mamia ya watoto wasiokwenda shule. Sasa wanajiuliza kama kweli bado wana sababu ya kuwashawishi wenzao kuja kuangalia vituko hivi.
Shirika la UNESCO kwa sababu ya kuona Ngorongoro inaelekea kukata roho, linanuia kuifuta kutoka kwenye orodha ya maeneo ya Urithi wa Dunia. Mhifadhi Mkuu Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan, tangu akiwa Makamu wa Rais, alishaona Ngorongoro iko kwenye machela ikielekezwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu. Ametamka bayana kwamba Ngorongoro lazima ilindwe. Sisi wajibu wetu ni kumkumbusha na kumpa moyo.
Hawa wote tukijumuisha mitazamo yao inayofanana, tunabaki kuhitahji ushahidi gani mwingine wa kutufanya tuamini kuwa Ngorongoro inakufa? Tutakuwa kizazi cha ajabu endapo tutaruhusu kifo cha kizembe cha Ngorongoro.
Tunapozungumza Ngorongoro, tusisahau kuzungumzia Pori Tengefu la Loliondo ambako bila kujali asilimia 48 ya maji yote yanayowatunza wanyampori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inatoka hapo, na sasa vyanzo vyote vinaelekea kuharibiwa.
Idadi ya mifugo ni kubwa mno, na mingi inaingizwa kutoka Kenya. Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa takriban kilometa za mraba 4,000 nalo linakufa.
Wanaojiita wanaharakati waliitisha serikali, nayo ikasalimu amri na kushindwa kumega eneo la kilometa 1,500 za mraba kati ya hizo 4,000 ili ziwe eneo la uhifadhi na ushoroba wa wanyamapori. Waliopendekeza jambo hilo walitambua kuwa bila Loliondo, Serengeti inakufa. Loliondo imeshavurugwa, matokeo yake wafugaji wamekuwa wakiingia hadi kilometa 20 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kwa mujibu wa takwimu za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro za mwaka 2016, idadi ya ng’ombe ilikuwa 227,000; mbuzi 418,000 na kondoo 417,000 wanaomilikiwa na wananchi wa tarafa mbili za Sale na Loliondo. Idadi hii haijumuishi maelfu ya mifugo kutoka Kenya.
Mifugo imekuwa ikichungwa na kupoteza kabisa vyanzo vya maji vilivyokuwa vikionekana miaka ya nyuma.
Pori Tengefu la Loliondo sasa ni la mashamba. Wanyamapori wamekimbia.
Wanyamapori wamekimbia kutokana na shughuli za kibinadamu. Mnyama ataishi vipi mahali ambako vyanzo vya maji vimekauka, au vile vilivyopo vimewekwa ili maji yatumiwe na ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda-vihongwe?
Wanyamapori watabaki vipi katika Pori Tengefu ambalo kilimo kinachofanywa si cha kujikimu, bali cha kibiashara huku matrekta yanayofanya kazi hiyo yakitoka Kenya kuja kuvuruga nchi yetu?
Mnyama gani aliyezoea miti na majani ataendelea kuishi mahali kunakokatwa miti kila uchao kwa kigezo cha kujenga maboma? Wanyama waendelee kuishi na watu ambao awali waliaminika kuwa ni marafiki zao, lakini sasa baadhi yao ni majangili?
Na kwanini mifugo isiwe mingi kama kuna NGOs zinazonufaika kwa ujio wa mifugo hiyo kutoka Kenya?
Mapato mengi na makubwa Ngorongoro hayatokani na mifugo, isipokuwa utalii. Utalii hauwezi kuwapo bila wanyamapori. Wanyamapori hawawezi kuwapo kama miti na vyanzo vya maji vinauawa. Uhifadhi hauwezi kustawi kama NGOs zitaendelea kuhamasisha wananchi kupinga mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Tume na kamati nyingi vimeshaundwa. Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Balozi Khamis Kagasheki, alifuata sheria alipotoa tamko kuhusu kupunguza eneo la Pori Tangefu la Loliondo kutoka kilomita za mraba 4,000 hadi 1,500 na kuliacha eneo la kilomita za mraba 2,500 litumiwe na wananchi kadiri wapendavyo.
Alifanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009, Sehemu ya 16, Vifungu Na. 4, 5 na 6. Sheria hiyo inampatia waziri mwenye dhamana uwezo wa kupitia upya mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali muhimu kwa manufaa ya wananchi bila kuathiri uhifadhi.
Waziri alifanya uamuzi huo kwa kuzingatia taarifa mbalimbali za utafiti na uchunguzi zilizotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), na alizingatia mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa. Mojawapo ya tume hizo ni Tume ya Waziri Mkuu ya mwaka 2010 ambayo ilijumuisha wajumbe kutoka wizara 9, Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro.
Pamoja na mambo mengine, tume hiyo ya Waziri Mkuu ilipendekeza kuwa kuna umuhimu wa kupunguza eneo la Pori Tengefu la Loliondo bila kuathiri mapito ya wanyamapori, na vyanzo vya maji. Leo ni mwaka 2022 ni hatua gani zimechukuliwa?
Loliondo na Ngorongoro kwa ujumla wake ni za Watanzania, hivyo sote tuna wajibu wa kuona ikiendelea kuwapo ili iwe na manufaa kwa Watanzania na walimwengu wote.
Haiwezekani kabila moja katika nchi likatae kutii mipango ya serikali, hasa ikizingatiwa kuwa kinachofanywa na dola kina manufaa makubwa kwa umma na kwa nchi.
Ukaidi wa aina hii usipodhibitiwa haitashangaza kusikia kuna watu hawataki Mlima Kilimanjaro uwe hifadhi. Wapo watakaosema dhahabu ni mali yao, kwa hiyo wasihamishwe. Tukilegea kuna siku sisi wa mbali na mito, maziwa na bahari tutazuiwa kuvua samaki, maana si wetu!
Hatushangilii wananchi kuonewa, la hasha! Watendewe haki kadiri ya sheria za nchi. Viongozi wa serikali wawe imara kusimamia masuala yenye manufaa kwa nchi.
Ngorongoro na Loliondo zimezungumzwa sana. Muda umewadia wa kumaliza kadhia hii ili tuendelee na mengine ya kimaendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameanza kushambuliwa na NGOs. Namsihi awe na roho ngumu. Wakuu wake wa kazi wasimwache peke yake. Atakuwa anapambana na magenge ya watu wenye ukwasi wakisaidiwa na baadhi ya waliokuwa viongozi wa mkoa huo na hata taifa.
Hao walishikamana kupinga mipango ya serikali kuu licha ya wao kuwa wamo serikalini. Bado wapo, tena wakiwa na nguvu. Hawa ndio wachochezi wakubwa wasiotaka kuona Ngorongoro na Loliondo zikitulia.
Kwa ndugu zangu wanahabari, nawasihi tuisaidie nchi kwa kwenda kuyashuhudia haya ninayoyasema. Wanahabari wasipende kupokea habari za ‘kusikia’ hasa kama eneo zinapopatikana hizo habari linafikika. Tunao wajibu wa kikatiba wa kulinda rasilimali za nchi yetu kwa faida yetu na kwa vizazi vijavyo. Tuwe radhi kusimamia hilo hata kama tutapewa majina yasiyofaa. Ukweli utatuweka huru.