Kipute cha Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) wiki hii kinaendelea na leo kutakuwa na mchezo mmoja, miamba ya Hispania, Real Madrid, ikikaribishwa na timu ya Ajax katika mchezo wa marudio utakaofanyika Uwanja wa Johan Cruijjf nchini Uholanzi.

Katika mchezo huo Real Madrid itamkosa beki wake kisiki, Sergio Ramos, baada ya kupata adhabu ya kadi mbili za njano katika mechi iliyopita, hivyo Kocha wa Real Madrid, Santiago Solari, atakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha anaimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo ili kuhakikisha wanatetea ubingwa wao waliobeba kwa misimu mitatu mfululizo chini ya kocha wao wa zamani, Zinedine Zidane.

Wapenzi wengi wa soka duniani wanawekeza fikra zao katika mechi ya kesho kwenye  mtanange mkali kati ya PSG watakaowakaribisha Manchester United (Mashetani Wekundu) katika dimba la Perc de Prince. Katika mechi ya awali ikumbukwe Manchester United walinyukwa magoli 2-0 kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Kutokana na matokeo ya ushindi waliopata PSG katika mechi ya ugenini, United wana kibarua kigumu katika kuhakikisha wanapindua matokeo ya mchezo huo ili kuingia katika hatua ya robo fainali.

Utawala wa United katika soka la Ulaya umekwisha baada ya kocha Sir Alex Ferguson kustaafu kuinoa timu hiyo, na mara kwa mara wamekuwa wakishindwa kufurukuta katika michuano hiyo hususan msimu uliokwisha timu hiyo ikitolewa na timu ya Seville katika hatua ya robo fainali baada ya kufungwa magoli 2-1 katika Uwanja wa nyumbani – Old Trafford, baada ya kutoka sare katika mechi ya kwanza iliyofanyika dimba la Ramon Sanchez-Pizjuan, nchini Hispania.

Katika mchezo huo Manchester United itawakosa nyota wake muhimu kama vile Anthony Martial, Ander Herrera, Juan Mata, Jesse Lingard na Paul Pogba – ambaye ataukosa mchezo huo kutokana na kupewa  adhabu ya kadi nyekundu katika mchezo uliopita baada ya kumchezea rafu Dan Alves katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha timu hizo.

Licha ya United kukabiliwa na majeruhi wengi, kwa upande mwingine PSG itaendelea kuwakosa wachezaji wake muhimu katika kikosi chao ambao ni pamoja na Neymar, Cavani na Adrien Rabiot, hali inayoweza kuwafanya United kupindua matokeo kutokana na kukosekana kwa wachezaji hao tishio katika mechi hiyo.

Lakini unaweza ukajiuliza, klabu za Uingereza nani kawaroga? Msingi wa swali hili unazingatia ukweli kwamba hivi karibuni timu za huko zimeshindwa kufua dafu katika mashindano hayo ya Ulaya, rekodi zikibainisha kuwa takriban miaka sita imepita klabu za  Hispania – Real Madrid na Barcelona zimebeba ubingwa wa Ulaya mara tano mfululizo.

Tangu mwaka 2012 Chelsea kubeba ubingwa wa Ulaya na Bayern Munich mwaka 2013, timu za Uingereza pamoja na klabu za Ujerumani zimeshindwa kutamba katika michuano hii ya Ulaya, licha ya kusajili wachezaji nyota, tena kwa bei ghali.

Licha ya United kutotabirika uwanjani, timu ya Liverpool nayo inakabiliwa na kibarua kigumu kutoka kwa Bayern Munich baada ya kupata sare tasa katika mechi iliyopita katika Uwanja wa Anfield. Kocha Jurgen Kllop naye anayo kazi ngumu kuhakikisha anaivusha timu yake katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya Ulaya katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Bayern Munich – Allianz Arena.

Timu ya Tottenham nayo inasongwa na kibarua kigumu mbele ya Borussia Dortmund katika kujihakikishia kutinga hatua ya robo fainali katika michuano hii ya Ulaya, licha ya kuwa na mtaji mzuri wa magoli matatu waliyoyapata katika mchezo wa nyumbani.

Kwa hiyo, katika mchezo wake wa marudio katika dimba la Westfalensadion, Ujerumani wanakabiliwa na shughuli pevu, hasa ikizingatiwa kuwa mpira wa miguu ni mchezo wa ‘maajabu’, lolote linaweza kutokea licha ya Spurs kuwa na mtaji mkubwa wa magoli.