Wiki kadhaa zilizopita nilikuwa miongoni mwa waalikwa kwenye mkutano wa mwaka unaoandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na kuwakutanisha wahariri na waandishi wa habari waandamizi kutoka pande zote nchini.

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TANAPA wameweka utaratibu huu kwa kutambua kuwa wanahabari wana nafasi ya kipekee kwenye uhifadhi. Kwa kutumia magazeti, majarida, redio, televisheni na mitandao ya kijamii, wanahabari wamefanya kazi kubwa iliyotukuka kwa kuelimisha wananchi umuhimu wa kulinda rasilimali wanyamapori, misitu na mali kale kwa ajili ya manufaa ya taifa letu.

Mkutano wa mwaka huu ulikuwa na mada nyingi. Zote zilikuwa motomoto. Miongoni mwa yaliyojadiliwa na ambalo ninapenda kuwashirikisha wadau wengine wa uhifadhi ni mpango unaopigiwa debe na baadhi ya ‘wakubwa’ wa kuwapo matumizi ya viberenge (cable car) vinavyoendeshwa kwa umeme ili kupandisha na kuwashusha watalii Mlima Kilimanjaro.

Wapigia debe mpango huu wanataja sababu kadhaa japo kubwa ni mbili. Mosi, ni kusaidia kuongeza idadi ya watalii, hivyo kukuza mapato kwa kuvutia makundi mapya ya watalii – walemavu na vikongwe. Pili, ni kuwapa fursa watalii wa makundi yaliyokosa fursa ya kukwea Mlima Kilimanjaro, ili yaweze ‘kutendewa haki’ hiyo. Makundi hayo ni ya wazee na walemavu ambao kwa sababu za maumbile au kiafya hawawezi kutembea kwa takriban wiki moja kufaidi uzuri wa mlima huu mzuri. Hizi ndizo sababu kubwa zinazotajwa na watetezi wa mpango huu. Nitajitahidi kurejea kwa ufupi mno yale niliyoyasema Mwanza. Kwanza, tutambue kuwa Mlima Kilimanjaro hauna mpinzani kama ilivyo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mbuga ya Maasai Mara nchini Kenya.

Kwa sifa za kuwa ndiyo mlima mrefu barani Afrika, mlima uliosimama peke yake ambao ni mrefu kuliko mlima wowote wa aina hiyo duniani, mlima unaotoa theluji licha ya kuwa ukanda wa Ikweta, na mlima ambao una aina zote za uoto wa asili; Mlima Kilimanjaro hauna mshindani. Kwa sababu hiyo, aina yoyote ya kuufaidi mlima huu isihusishwe na ushindani.

Kitu kizuri hakipatikani kirahisi. Tanzanite ingekuwa inapatikana kama tunavyookota kokoto kando ya barabara, sidhani serikali ingejenga uzio kuzunguka machimbo hayo Mirerani. Almasi ingekuwa inapatikana kwa wepesi isingekuwa na thamani sokoni. Thamani ya tanzanite, almasi na madini mengine inachagizwa na ukweli kwamba upatikanaji wake ni mgumu.

Mojawapo ya sifa ya Mlima Kilimanjaro ni ugumu kwa mkweaji kufika kileleni. Ndiyo maana wengi huanza safari, lakini si wote wanaohitimisha na kurejea salama. Sifa hiyo pekee inaufanya Mlima Kilimanjaro uwe wa kipekee.

Kwa wale wanaojua siri ya uhifadhi Tanzania, wanatambua kuwa dhima ya kwanza kabisa ni UHIFADHI, na kwamba mapato ni matokeo au ni ziada tu ya kazi kubwa ya uhifadhi. Ni kwa sababu hiyo Tanzania kwa miaka mingi imezingatia mapato na si wingi wa wageni. Unaweza kushusha ada kwa wageni wanaozuru maeneo yetu ya hifadhi na matokeo yake yakawa kulemewa na kuvuruga kabisa rasilimali hizi.

Tunahitaji kuongeza idadi ya watalii na mapato, lakini sidhani kama kuna umuhimu wa kuondoa uhalisia na ladha ya ukweaji mlima huu kwa kuleta cable car. Wala sidhani kama suala la ‘haki za binadamu’ linapaswa kuingizwa kwenye jambo hili kwa kigezo cha kufurahisha kila kundi. Mlima Kilimanjaro uachwe kwenye uhalisia wake ili kuendelea kuupa heshima na umaarufu. Zipo sababu nyingi za kuendelea na mfumo wa sasa. Kwa mfano, utaratibu wa sasa unawafanya watalii wakae siku nyingi nchini. Kukaa kwako ndiyo faraja kwa wananchi na nchi kimapato. Tukiruhusu cable car maana yake tunafupisha muda wa watalii kukaa nchini. Tutawaumiza maelfu ya wapagazi ambao maisha yao yananawiri kutokana na kazi wanazofanya sasa.

Watetezi wa viberenge hivi wanasema hakutakuwa na athari kimazingira. Hili si kweli. Athari zitakuwapo hata kama si kwa kiwango ambacho wengi wetu tunakifikiria.

Kuanzisha utaratibu huu mpya kutavunja au kupunguza hadhi ya vyeti wanavyotunukiwa wale waliofanikiwa kufika hatua mbalimbali za mlima huu.

Kweli tunahitaji mapato yaongezeke, lakini tuwe makini sana kuhakikisha kiu ya fedha haiondoi uhondo wa rasilimali zetu. Mlima Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo machache mno katika sayari hii ambayo mwanadamu anaweza kufika na kufaidi uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Tusiondoe ladha hii na kubaki na mlima artificial.

Bahati nzuri ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii wahifadhi wengi, kama si wote, hawaukubali mpango huu. Swali la kujiuliza ni kwanini mradi huu umeshupaliwa? Kwanini hao wanaotaka kuwekeza wasijitokeze hadharani wajibu maswali?

Nirejee kusisitiza kuwa Mlima Kilimanjaro hauna mpinzani. Hakuna kilele kingine Afrika kinachopiku kilele cha mlima huu. Utajiri huu tunao sisi wenyewe. Kama ni mchuzi, basi huu umeshajiunga! Kuongeza vikorombwezo vingine ni kupoteza thamani na ladha yake. Lililo muhimu ni kwa wadau wote kuendelea kuutangaza Mlima Kilimanjaro na vivutio vingine ili watalii malaki kwa malaki wamiminike nchini mwetu. Kiu ya mapato isituongoze kuharibu urithi wetu.