Tangu kuanza kwa Ligi Kuu England, Manchester United ilipata ushindi wa pili katika mchezo wake wa Jumamosi iliyiopita dhidi ya West Ham United.
Kwa ushindi huo, United sasa imefikisha pointi nane baada ya kucheza mechi sita. Imetoka sare mechi mbili na kufungwa tatu hali ambayo ilianza kuwakatisha tamaa mashabiki wake.
Ushindi wa Jumamosi iliyopita si wa kuipa faraja moja kwa moja Manchester United kwani timu hiyo ukuta wake umemegeka kutokana  na kukabiliwa na majeruhi wengi.
Mabeki wanauguza majeruhi ni Chris Smalling beki huyo wakati alipata  maumivu ya bega katika mazoezi.
Mbali na  Smalling  majeruhi wengine ni Phil Jones mwenye maumivu ya goti Jonny Evans (kifundo cha mguu) na kinda Tyler Blacket anayetumikia adhabu.
Na itakumbukwa kwamba timu hiyo ilipoteza mabeki wake, Rio Ferdinand, Namanja Vidic na Patrice Evra mara baada ya msimu uliopita wa ligi hiyo ambayo mashetani hao wekundu walimaliza katika nafasi ya saba.
Pamoja na timu hiyo kupata mzuri na mwenye mafanikio ya hali ya juu Louis van Gaal lakini bado timu hiyo inasuasua katika msimu huu wa ligi hali inayowapa wasiwasi mashabiki na wapenzi hadi kuhoji tatizo ni nini.
Van Gaal ambaye ana uzoefu mkubwa wa kufundisha timu nyingi na rekodi yake ni nzuri. Pia wamesajili wachezaji wazuri na wenye majina makubwa.
Katika kipindi cha usajili wa dirisha kubwa la majira ya joto, Manchester united ilisajili wachezaji wengi tena kwa fedha nyingi.
Wachezaji waliosajiliwa ni pamoja na Luke Shaw, Ander Herrera, Angel Di Maria, Radamel Falcao, Daley Blind na Marcos Rojo.
Kwa pamoja wachezaji hao waliigharimu Manchester United kiasi cha paundi milioni 150  za Uingereza ikiwa ni sawa na Sh bilioni 300 za Tanzania.
Pamoja na hayo yote, msimu uliopita timu hiyo ikiwa chini ya Kocha David Moyes katika mechi zake tano za kwanza iliifikisha Manchester United katika nafasi ya saba huku ikiwa imetumia paundi milioni 64.
Pamoja na matumizi makubwa ya fedha hizo bado timu hiyo ikiwa na chini ya van Gaal hadi sasa ikiwa imecheza mechi zake sita ainashika nafasi ya saba ikiwa na pointi 8  na pia imetolewa nje katika mashindano ya Capital One Cup.
Kwa tathimini ndogo ya haraka haraka inaonesha kwamba Manchester United ina matatizo madogo madogo ambayo yanaweza kurekebishwa  na kupata matokeo bora katika msimu huu.
Matatizo ya Man U
Timu hiyo inasumbuliwa na mfumo ambao kocha  huyo anautumia kwa  kuchezesha mabeki watatu nyuma huku katikati akiweka viungo wengi, mfumo huu unaonekana kuwasumbua wachezaji ukizingatia mabeki wengi wa kati wa Man U bado hawana uzoefu wa kutosha katika mfumo huo.
Mfumo huo unaonekana kuzoewa na mabeki wake mahiri kama Nemanja Vidic na Rio Ferdinand, kwani mabeki hawa walikuwa wameishazoeana na wana uzoefu wa kutosha.
Lakini mabeki kama John Evans, Rafael na Blackett hawajazoeana  mfumo na pia hawana uzoefu wa kutosha.
Tatizo la pili lililofanywa na Kocha Van Gaal ni kusajili wachezaji wenye majina makubwa bila kuangalia uwezo wa mchezaji kwani ilimuacha Javier Hernández Balcázar ‘Chicharito’ ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kukaa katika nafasi na kufunga magoli na kumsajili  Falcao.

Chicharito amepelekwa Real Madrid kwa mkopo hadi sasa amefunga  magoli mawili katika mechi moja ambayo Madrid ilishinda mabao manane dhidi ya Deportivo La Coruna.
Tatu Man U ilimuacha beki wao mahiri mwenye kasi Patrice Evra na kumsajili kinda, Luke Shaw kwa fedha nyingi na kumuuza Evra katika timu ya As Monaco.
Luke Shaw hadi sasa hajashuka dimbani kuichezea timu hiyo hata mechi moja kwa kuwa ni majeruhi.
Hata hivyo usajili wa Di Maria ni moja kati ya usajili bora aliofanywa na Kocha Louis van Gaal katika hiyo kwani ameonesha uwezo mkubwa wa kupunguza mabeki.
Amekuwa akipiga krosi nzuri na pia ana kasi ya hatari na hata kufunga magoli, lakini mchezaji huyo anapata shida katika suala la nani wa kumpa pasi za mwisho.
Manchester united ikibadilisha mfumo wake wa kuacha mabeki watatu nyuma itafufuka na kuwa katika nafasi za kuwania kuingia katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
Pamoja na misukosuko ya vichapo anavyopokea nahodha  wa timu hiyo Wayne Rooney ameonekana kuwa na mtazamo chanya kwani amewaambia wachezaji wenzake ya kuwa timu itafufuka  na kufanya vizuri katika mechi zijazo.