Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza Manchester City, baada ya kufanikiwa kumbakiza kocha wao Pep Guardiaola kwa msimu mmoja zaidi, Sasa wana nia ya kumbakiza mshambuliaji wao Erling Haaland (24), kwa misimu mingine mitano.

Manchester City wamempa ofa ya mkataba wa miaka mitano nyota huyo raia wa Norway, mkataba wenye ofa ya Pauni 500,000 ambazo ni sawa na Bilioni 1.67 za kitanzania kwa wiki, kiasi kitakachomfanya kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi Uingereza akimpita mchezaji mwenzake Kevin de Bruyne anayejikusanyia Pauni 400,000 kwa wiki.

Hii inakuaa baada ya nyota huyo kuhusishwa na klabu kubwa za Hispania, Real Madrid pamoja na Barcelona, hivyo Manchester City wanataka kuzima maslahi yoyote kwa mshambuliaji wao nyota.

Erling Halaand alijiunga na Manchester City misimu miwili iliyopita, na hivi Sasa amebakiza miaka miwili na nusu katika mkataba wake wa kwanza, ambao alisaini kuitumikia klabu hiyo kwa miaka mitano.

Mpaka sasa Haaland ameshinda tuzo ya Golden Boot katika misimu yake miwili ya kwanza kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, na sasa yuko njiani kushinda tena tuzo hiyo baada ya kufunga mabao 12 katika mechi zake 11 za mwanzo za ligi msimu wa 2024-25.