Na Egbart Rwegasira, JamhuriMedia, Kagera

Ubalozi wa Japan nchini Tanzania kupitia naibu mkuu wa ujumbe wa Japan nchini Tanzania Bw. Shoich Ueda mapema Desemba 11, 2024 uliwasili Wilaya Misseny mkoani Kagera kwa lengo la kuzindua na kukabidhi bweni kubwa la wasichana lililojengwa kwa ufadhili wa chi hiyo.

Bweni hilo kubwa na la kisasa lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 120, likiwa na vitanda 60, kabati 30,Nyumba ya mlezi wa wanafunzi (matroni) Pamoja na vyoo na bafu limejengwa katika shule ya sekondari Kagera inayopatikana kata Kyaka Wilaya ya Misseny huku ikigharimu kiasi cha shilingi milioni 270,115,900 hadi kukamilika kwake na ikiwa ni wazo la Mwenyekiti wa Halmashauri ya Qilaya Missenyi Projestus Tegamaisho lililoratibiwa na kusimamiwa na shirika la Mapec kupitia mkurugenzi wake Dr George Buberwa.

Akizungumza na mwandishi wa Jamhuri Digital mkoani kagera Tegamaisho alisema ”Niliona uhitaji wa bweni katika shule hii na nikarejea maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hasan alipotutaka watumishi na viongozi kutumia akili ya kujiongeza kusaidia serikali kuleta maendeleo, nikiwa kama kiongozi anayeamini na kuheshimu taasisi binafsi nilimfuata mkurugenzi wa Mapec na kuomba atumie uzoefu wake kutafuta ufadhili wa haraka ili kufanikisha hilo, ni kweli Dr George aliandika andiko la kuomba mradi na sasa tumevuna tulichopanda.

Akizungumza kwa niaba ya Japan kaimu balozi Ueda alisema hili ni bweni la pili lililojengwa kwa ufadhili wa Japan Wilayani Misseny huku akitoa pongezi kwa shirika la Mapec ambao wamekuwa wasimamizi bora wa Miradi yao “ nawapongeza mapec kwa kusimamia vizuri miradi yetu, na tupo tayari kujenga bweni lingine la wavulana kama itaonekana kuna uhitaji” alisema Ueda.

Sambamba na hayo kaimu balozi wa Japan alisema anafurahi kufika Kagera wanapolima kahawa ikiwa Japan ni moja ya mataifa makubwa Duniani yanayotumia kahawa kutoka Tanzania hivyo anatamani kuona wanakagera wanaendelea kuuza kahawa yao nchini humo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Mapec ameiomba serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika binafsi na kutoa ushirikiano zaidi ili mashirika hayo yasaidie kupatikana kwa miradi mingi ambayo inaleta mabadiliko na maendeleo kwa wananchi wote.