Hatimaye Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amewasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Ubelgiji na kupokelewa na wafuasi wa chama hicho.
Mwanasiasa huyo nguli wa upinzani ambaye awali alikuwa Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki na mwanasheria nguli, amerejea baada ya miaka mitano kuishi nje ya nchi.
Lissu aliwahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amepokelewa na viongozi na wanachama wa Chadema.
Mamia ya wafuasi wa CHADEMA wamekusanyika nje ya lango hilo wakiimba na kucheza huku ngoma pamoja na mavuvuzela.
Hata hivyo Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi na kuhakikisha wafuasi hao hawaingii ndani ya eneo la uwanja na badala yake wanabaki nje ya lango kuu pembezoni mwa barabara ya Nyerere.
Pia hali ya ulinzi na usalama iliimarishwa ili kuhakikisha kuwa shamrashamra hizo zinamalizika bila ya kuwepo kwa fujo.