Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Maandalizi ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mkoani Pwani yamefikia asilimia ili kufanikisha kufanya tukio hili kuwa kubwa la kihistoria.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, tarehe 2 Aprili 2025.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaji Abubakar Kunenge, alipokagua ukarabati wa uwanja huo alieleza kuwa hatua iliyopo sasa ni umaliziaji wa kazi na kuanza mapambo.
“Sisi ngazi ya mkoa, tukishirikiana na wenzetu kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, tumetembelea na kukagua, na tumeridhishwa na maendeleo, matayarisho yako tayari na uwanja umekamilika,” alisema Kunenge.
Aliongeza kuwa, “Kuna matenti ya kutosha, miundombinu ya maji na umeme vimekamilika, jukwaa kubwa lipo tayari, na sehemu za viongozi VIP I, II, na III pia zimekamilika.
Kunenge alieleza, kunatarajia kuwa na wananchi 16,000, na maeneo ya haraiki tayari yako vizuri.”

Hata hivyo, Kunenge alibainisha kuwa ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2025 unalenga kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura kwa amani na utulivu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Ujumbe huo pia utaendelea kupambana dhidi ya rushwa, kutoa kipaumbele kwa utunzaji wa afya, na kukuza kilimo, huku ukisisitiza mshikamano wa kitaifa.
“Ninawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi na tuitendee haki heshima tuliyopewa,” alisisitiza Kunenge.


