Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetaja mafanikio ambayo imeyapata katika kipindi cha miaka 61 ya uhuru wa Tanzania Bara huku ikiahidi kushirikiana na wizara nyingine katika kuhakikisha amani, usalama wa raia na mali zao vinalindwa ili kuiwezesha nchi kupiga hatua zaidi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika kikao kazi kilichoshirikisha Wakuu wa Vitengo na wasaidizi wake, Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Maduhu Kazi amesema hali ya ulinzi na usalama nchini imeimarika na kuwataka wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za kimaendeleo bila hofu yoyote.
“Tunatimiza miaka 61 ya uhuru tukiongozwa na kauli mbiu inayosema Miaka 61 ya Uhuru, Amani na Umoja ni Nguzo ya Maendeleo Yetu na sisi wizara tuna mafanikio mengi na makubwa ambayo tunapenda watanzania waweze kuyafahamu” alisema Dkt. Kazi
Ameyataja mafanikio hayo ikiwemo mabadiliko ya muundo kwa baadhi ya idara zake ikiwemo kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Uhamiaji kupewa hadhi ya kuwa majeshi ambayo itawapelekea kuboresha zaidi shughuli zao na kuwahudumia wananchi katika namna bora zaidi.
Ameyataja mafanikio mengine ambayo yamejumuisha ujenzi wa ofisi pamoja na makazi ya askari kutoka katika majeshi ya Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto na Uokoaji sambamba na ujenzi wa vituo vya polisi na zimamoto.
“Tumekua pia na uendelezaji wa taaluma katika vyuo vya kijeshi, sasa hivi katika miaka 61 tumekua na vyuo mbalimbali na tukiendelea kuboresha vyuo hivyo na mpaka sasa hivi tumekua na Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi, Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Chuo cha Polisi Zanzibar, Chuo cha Polisi Kidatu, Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza,Chuo cha Zimamoto na Uokoaji Chogo, Chuo cha Mafunzo ya Uhamiaji cha Kikanda Moshi pamoja na Chuo cha Uhamiaji Raphael Kubaga kilichopo Tanga” aliongeza Dkt. Kazi
Wizara pia imefanikiwa katika uanzishwaji wa uhamiaji mtandao, ujenzi wa viwanda katika vyombo vya usalama, uboreshaji wa huduma za zimamoto na uokozi, uanzishwaji wa madawati ya jinsia, uanzishwaji wa mashirika ya uzalishaji mali katika vyombo vya ulinzi na usalama, kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu, kuendelea kusajili taasisi za kidini na kuongeza ujenzi wa magereza ambao umesaidia kupunguza msongano wa mahabusu na wafungwa katika magereza ikienda sambamba na huduma za uangalizi na uboreshaji wa huduma hizo ili wawe raia bora wanapomaliza vifungo vyao na kuanzisha mfumo wa kushughulikia malalamiko.