KILIMANJARO

Na Nassoro Kitunda

Kumekuwa na hoja kutoka kwa wanasiasa na wadau wa siasa kuhusu kutaka maridhiano kutoka pande zote; wa upinzani na chama tawala, na hadi inaingia Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na madai hayo ya wanasiasa kutaka kuonana na rais na kuzungumzia masuala ya maridhiano ya kisiasa, kwa madai kwamba watu wamegawanyika, hasa wanasiasa. 

Na hoja hii imezungumzwa pia na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), Zitto Kabwe, kuwa nchi imegawanyika na wanasiasa wakutane na rais wairejeshe nchi ilipokuwa na ibaki kwenye mstari.

Katika mjadala huo, Msajili wa Vyama vya Siasa, akatoka hadharani na kuitisha kikao na watu wa usalama na wanasiasa ili kujadili masuala yao, hasa ya kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa. 

Kuna baadhi ya vyama vya upinzani vimeitikia kauli hiyo, lakini baadhi ya vyama vimekataa wito huu na kusema msajili hana mamlaka hayo, suala la muhimu kwao ni watu kutimiza wajibu wao na kufuata sheria ya vyama vya siasa ambayo inaruhusu wanasiasa kufanya mikutano ya hadhara. 

Lakini wakati wa kikao kile cha wanasiasa, Mwenyekiti wa TCD, Zitto, aliomba kuweko na mazungumzo ya wanasiasa kama sehemu ya kutafuta mwafaka, lakini Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na NCCR-Mageuzi wakapinga mawazo ya Zitto kuwa suala si kuomba mazungumzo, ni kuachiwa kwa viongozi wao wa kisiasa, kuachiwa kwa mikutano ya kisiasa na uhuru wa kisiasa. 

Lakini vyama vyote vya upinzani vinakubaliana katika kutafuta maridhiano katika kurekebisha na kupata tume huru ya uchaguzi na Katiba mpya. 

Mimi sitajihusisha na upande wowote, lakini kwa hoja hizo hapo juu ndio muktadha wa kuja kwa hoja ya maridhiano, ndiyo inaanzia hapo. Lakini makala hii inahoji dhana ya maridhiano, nini ni maridhiano? Na yanalenga nini? Mambo yapi hayazungumzwi kwenye suala la maridhiano? 

Na uzoefu unaonyesha nini kwenye siasa za Afrika na ulimwengu juu ya kinachoitwa siasa za maridhiano? Na nini maridhiano yanapaswa yaguse? Maswali haya yatatusaidia kujua maridhiano hasa yanapaswa yaweje.

Kuundwa kwa kikosi kazi cha demokrasia

Katika mkutano uliofanywa na baadhi ya vyama vya upinzani na chama tawala jijini Dodoma, Desemba 15 na 17, ulitoka na azimio la kuundwa kwa kikosi kazi cha demokrasia cha watu 23. 

Pia, Januari 10, 2022 huko Zanzibar, Rais Dk. Hussein Mwinyi, alizindua kikosi kazi cha kuratibu na kuchakata maoni yaliyotolewa na vyama hivyo, na madai yaliyotolewa ni kutaka kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi, kurejesha majukwaa na mikutano ya kisiasa pamoja na kutungwa tena kwa sheria ya vyama vya siasa ili kutoa uhuru wa vyama kufanya shughuli zake za kisiasa. 

Kikosi kazi hiki kitafanya kazi zake Tanzania Bara na Zanzibar katika kuchakata maoni ya vyama vingi vya siasa, lakini madai yenyewe ndiyo baadhi nimeyataja hapo juu, lakini hamna hata moja linalozungumzia uhuru wa wananchi katika maisha yao ya kupata uchumi wao. 

Yote kwa yote, ni malalamiko ya wanasiasa katika kuangalia uchaguzi, zaidi mjadala umeibuka kwenue Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba mpya. 

Maridhiano ya kisiasa hayagusi masuala haya

Ukirejea hapo juu, hoja za wanasiasa wa upinzani na chama tawala wanayatazama maridhiano kama sehemu ya kisiasa tu, yaani wanasiasa kukaa pamoja kwenye meza na kukubaliana masuala yao yanayohusu masuala ya vyeo na uhuru wao wa kufanya kazi. 

Lakini nafikiri haya ni makosa tunayafanya, kwa sababu maridhiano ni mchakato ambao unapaswa uanzie kwa wananchi wenyewe. Lakini ukitazama madai ya wanasiasa kuhitaji maridhiano hayatokani na hoja za wananchi juu ya hali zao za maisha ya kila kitu. 

Maridhiano haya hayagusi kabisa hali ya wananchi wanaondokana vipi na umaskini waliokuwa nao, wanapata vipi huduma zao za msingi za kila siku, lakini maridhiano ya siasa zetu hizi za kutafuta kula zenyewe zinajielekeza kwenye ugatuzi wa kisiasa na vyeo kuliko ugatuzi wa uchumi. 

Wananchi wanahitaji maridhaino, na maana kwao ya maridhiano ni kupata ardhi, maji na afya. Mchimbaji wa madini anahitaji leseni ya uchimbaji na kitalu. Hata mjadala wa wamachinga, wanahitaji maridhiano ya kupata maeneo ya kufanya biashara zao. 

Lakini ukitazama maoni ya wanasiasa juu ya hicho kikosi kazi kilichoundwa cha kuratibu madai ya wanasiasa, wao wanalilia uhuru wa vyama vya siasa tu na si uhuru wa mmachinga kufanya biashara zake. 

Wanasiasa wanalilia uhuru wao wa kufanya mikutano na kuwa huru kupata vyeo lakini wamachinga wanahitaji uhuru wa biashara zao, sawa na wakulima, ndio kundi lenye umaskini mkubwa na ndivyo tafiti zetu zinaonyesha hivyo, lakini madai yao si ajenda za wanasiasa, siasa zetu hazijadili tena mkulima kwa nini ni maskini? 

Kwa nini mazao yake hayamnufaishi yeye mwenyewe? Sera zipi zitakazowajali wakulima? Mambo haya si kipaumbele kwenye yanayoitwa maridhiano ya wanasiasa.

Wavuvi wanatoa hoja ya kuona kuna sera zinazowabana wasivue na kila kukicha wanaondolewa kwenye maeneo yao ya uvuvi. 

Lakini pia hata kundi la wavuvi kuwa maskini, kunyonywa mali zao, mazao yao ya uvuvi wanayoyavua na wanaojiita wajasiriamali wa uvuvi, lakini ukiwasikiliza wanasiasa na wanaodai maridhiano ya nchi, masuala haya ya wananchi hayaonekani kama sehemu ambayo yalipaswa kujadiliwa kwenye hayo maridhiano. 

Kwa bahati mbaya masuala haya huwa hayapewi kipaumbele na uzito mkubwa kwenye hayo yanayoitwa maridhiano ya wanasiasa, kwa sababu mwanasiasa anawaza atashinda vipi Uchaguzi Mkuu ujao, lakini si mwananchi ananufaika vipi baada ya uchaguzi ujao. 

Uzoefu katika Bara la Afrika

Uzoefu unaonyesha hivyo, siasa zetu katika kinachoitwa maridhiano barani Afrika na ulimwengu kwa ujumla wake, bado tunaendelea kufanya makosa tunadhani wanasiasa kukubaliana kugawana vyeo ndiyo tumefikia maridhiano. Kumbe si kweli. 

Ipo mifano ya uundwaji wa serikali za mpito na za umoja wa kitaifa, ambazo shabaha yake ni kwenda kwenye uchaguzi na kuwaita wadau pamoja wa kisiasa na kugawana vyeo, lakini njia hiyo imekuwa na matatizo makubwa sana na kuleta hali ya uvunjifu wa amani na watu kutoelewana. 

Mfano mzuri wa nchi ya Sudan baada ya kumuondoa Omar Ali Bashir, mpaka sasa kuna mvutano wa madaraka baina ya jeshi na serikali ya kiraia pamoja na wananchi wenyewe. 

Ukitazama wakati inaundwa serikali ya mpito haikuyazingatia maoni ya wananchi, mvutano umekuwa namna ya nafasi na madaraka. 

Pia nchi ya Mali baada ya kupinduliwa kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Ibrahim Boubacar Keita, katika kutafuta maridhiano ikaundwa serikali ya mpito ambayo nayo ilijikita kwenye kugawana vyeo na kutazama uchaguzi, lakini si mjadala wa sera gani zitakazowawezesha wananchi kupiga hatua kimaisha, mambo haya hayakuwa kipaumbele. Mpaka sasa nchi ya Mali bado haijatulia chini ya Asimi Goita. 

Pia jirani zetu DR Congo, mpasuko wa serikali ya Tshisekedi na chama kinachoongozwa na aliyekuwa Rais, Joseph Kabila, juu ya kugawanywa kwa nafasi za uwaziri. 

Hii ilikuwa kama sehemu ya maridhiano ya kisiasa ili kuweka taifa pamoja. Lakini kilichotokea ni mpasuko katika taifa, wanasiasa wanaona vyeo havitoshi. 

Lakini pia makubaliano haya ya kisiasa hayakugusa hata kidogo shida za wananchi wa Congo, bado Wacongo walikuwa katika shida mbali na maridhiano yale ya kisiasa. 

Na hata kinachoendelea Kenya, kwa kile walichokiita maridhiano ya ‘handshaking’ Uhuru na Odinga. Lakini kushikana mkono huku, hakuangalii na kugusa kabisa maisha ya watu, ni wanasiasa tu kupata mwafaka wa maisha yao. 

Na baadaye tuliona ujio wa BBI (Build Bridge Initiatives) nao ulitafsiri kuleta mwafaka katika nchi lakini kilichoonekana si hicho, ni wanasiasa kujitengenezea fursa za uongozi na kujiwekea ulinzi wa mali zao. 

Kwa mifano hii, kwa ufupi hii inatuonyesha kuwa tunafanya makosa kufikia maridhiano. Hatufuati maridhiano ya kweli, mara zote tumekuwa tunadhani wadau wa kisiasa wakipewa nafasi kwenye serikali, basi tumemaliza migogoro na matatizo, kumbe tunaacha sehemu kubwa ya wananchi ambao wana ajenda zao na maoni yao juu ya maisha yao ya kila siku. 

Na ili uweze kuyazungumza ya wananchi na kupata mwafaka, lazima kuwe na mjadala wa kujadili ni sera zipi ambazo zinaweza kuwapeleka mbele wananchi.

Ni nini maridhianao yanapaswa kugusa?

Swali hili ni muhimu hasa katika hoja niliyoitoa, kuwa maridhiano yetu yanaacha sehemu muhimu sana ya kujadili sera gani zinazowavusha wananchi? Je, ni sera zinazojali wengi? Au ni sera za wachache? 

Maswali haya yanapaswa kuongoza majadiliano yetu juu ya maridhiano. Hatupaswi kuishia kwenye uhuru wa wanasiasa na kuhubiri amani, ipo haja ya kupanua mjadala juu ya maridhiano, ionekane pia mwananchi akisema nimekosa huduma hospitali, pia ijadiliwe kwenye maridhiano kwamba mwananchi huyo anahitaji afya na ndiyo maridhiano ya kweli katika jamii. 

Maridhiano lazima yatambue sababu gani kuna kuwa na pengo kubwa kati ya maskini na matajiri? Nini kinasababisha haya; kuwe na walalahoi na walalaheri? Je, sera zipi zinaweza kuondoa tatizo hili? Si tu kuishia kwenye Tume Huru ya Uchaguzi, kama vile uchaguzi ndiyo njia pekee itakayowapa watu maisha mazuri, la! 

Lazima tutafute maridhiano juu ya kuja na sera zitakazojali walio wengi katika nchi, si sera zinazojali wachache zinazowafanya wananchi kutengwa na uchumi wao ambazo zinawapa shaka wavuvi kuondoka baharini, wamachinga kuacha biashara au wakulima kuacha kilimo. 

Tunahitaji maridhiano ambayo yatatufanya tuwe na sera ambazo zitainua hali ya makundi mbalimbali katika jamii katika kuzalisha mali. 

Rai yangu

Ni muhimu sana kuyapa umuhimu masuala ambayo wananchi wanayadai, na si makubaliano ya wanasiasa. Hivyo, maridhiano yajikite kwenye sera ambazo zitakazowajali walio wengi na si vinginevyo. 

Lazima tufikiri upya dhana ya maridhiano na kutaka mazungumzo ya kisiasa, si Tanzania tu bali Afrika na dunia kwa ujumla, kuwa kutafuta mwafaka si wanasiasa kukaa kwenye meza na kugawana vyakula, bali ni kujadili namna gani mwananchi wa kawaida atapata ardhi yake? Uchumi wake? 

Mkulima atauzaje mazao yake na kadhalika. Lakini kama tutaendelea kudhani kuwa na utitiri wa vyama na wanasiasa kuweka vikao na kuzungumzia masuala yao ndio mwafaka na maridhiano, tutakuwa hatulengi kuleta ukombozi wa jamii, bali kikundi kidogo cha wanasiasa kunufaika.

Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa namba za simu: 0683 961891/0659 639808 na barua pepe: [email protected]