DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Mjadala kuhusu hitaji la Katiba mpya bado haujakufa miongoni mwa wananchi, wanaharakati, wasomi na wanasiasa.
Lipo kundi la wale wanaodhani sasa ni muda mwafaka kwa Tanzania kuwa nayo. Pia wapo wale wanaoamini kwamba waraka huo si muhimu kuliko upatikanaji wa haki za msingi za kijamii.
Wapo wadau wanaobainisha kwamba tatizo wala si Katiba mpya, bali namna ya kuyatekeleza yaliyomo katika Katiba kwa kitaalamu wanaita ukatiba.
Makundi haya yanaendelea kunyukana katika majukwaa mbalimbali ikiwamo mitandao ya kijamii. Binafsi sitaki kujihusisha na kundi lolote kati ya haya matatu. Ningependa kuibua hoja nyingine ambayo hadi sasa sijaona ikijadiliwa kwa mapana na marefu licha ya umuhimu wake.
Hoja yangu inajikita katika dhana ya Katiba kama uwanja wa mapambano ya kitabaka kati ya walionacho na wasionacho. Dhana hii kuhusu Katiba inajengwa na ukweli kwamba katika jamii yapo makundi yenye masilahi tofauti na muda mwingine kinzani.
Tabaka la wasionacho, au kama wanavyojulikana hapa Tanzania, walalahoi, linawajumuisha wafanyakazi, wakulima, wavuvi, wamachinga, bodaboda na kadhalika.
Hawa wanahitaji Katiba ili kujikomboa. Wakati huo huo wale walionacho, au walalaheri, wakiwamo watu wenye mitaji na wanasiasa wa pande zote mbili, upinzani na chama tawala, wanahitaji Katiba kuhakikisha masilahi yao yanadumishwa kwa kuhakikisha mfumo uliopo wa kiuchumi – siasa unaendelezwa.
Kwa maoni yangu, mjadala kuhusu Katiba mpya hauwezi kuachwa kuathiriwa na mgongano wa kitabaka niliougusia hapo juu. Hivyo, ni muhimu kutambua haya madai ni kwa masilahi ya kundi gani, wasionacho au walionacho?
Masilahi ya walalahoi yanaweza kuonekana kupitia hofu zao kuhusu mfumo wa uchumi unaowafukarisha wakati kwa walalaheri masilahi yao ni kuona nafasi yao kisiasa – kiuchumi inaendelea kudumishwa kupitia mfumo uliopo wa kibepari.
Huu mvutano wa kimasilahi baina ya matabaka haya mawili katika jamii ni vema ukawekwa wazi katika mjadala huu wa Katiba. Je, kwa hali iliyopo ni tabaka lipi litashinda?
Kwa vyovyote vile, tabaka tawala – linalojumuisha watawala waliopo madarakani na wapinzani wanaouwania utawala – litafanikiwa, kwa kuwa mawazo na nguvu za tabaka hilo ndizo zinatawala jamii kwa sasa.
Kwa hiyo, walalahoi na hata walalahai wanaweza wakawa kama daraja tu la kufikia Katiba mpya. Na hii inatukumbusha zaidi kuwa katiba ni mapambano ya kitabaka, si kitu huru tu, hivyo tunapaswa kuwa makini katika kujadili.
Kama nilivyosema katika hoja iliyopita, Katiba ni mapambano ya kitabaka. Katika mapambano hayo kundi la walalaheri linatumia mbinu mbalimbali za kuweza kuwafanya walalahoi wasiweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Katiba.
Mbinu mojawapo ni elimu na nyingine ni ile mlalahoi akihitaji huduma ya maji au umeme, walalaheri wanamwambia hilo si suala la Katiba, bali ni suala la wizara au halmashauri.
Kwa mfano, wapo watu wanaodhani kuwa katika mchakato wa Katiba mpya sharti kwanza ‘wananchi wa kawaida’ – yaani walalahoi wapewe elimu kuhusu Katiba. Wanaona walalahoi wapo kimya na hawajui uzito na maana ya Katiba.
Lakini wanasahau kuwa kwa mwananchi mlalahoi kufahamu Katiba si lazima awe amekariri vifungu au misamiati ya kisheria inayopatikana humo.
Profesa Issa Shivji amewahi kusema mwananchi akisema hana barabara, hapati matibabu hospitalini, na hana masoko ya mazao yake, hapo maana yake anazungumzia Katiba, si lazima aonyeshe kuwa ibara fulani mimi siipendi au ibadilishwe.
Suala la kubadilisha au kutengeneza hivyo vifungu si la mwananchi moja kwa moja. Ni jukumu la waliopewa dhamana ya kutengeneza au kuyaweka maoni hayo ya wananchi katika Katiba.
Hivyo, kwa makundi yote yaliyo mstari wa mbele katika mjadala huo ni muhimu watambue kwamba hoja ya elimu inapaswa kutafakariwa zaidi ya watu kujua ibara au maandishi ya Katiba.
Je, Katiba ni mwarobaini? Katika kujadili hili ninakubaliana na Profesa Shivji ambaye amewahi kutolea mfano wa nchi kadhaa zinazoaminika kuwa na Katiba bora zaidi Afrika lakini ukitazama hali ya ndani katika nchi hizo ni ya kusikitisha.
Hii inatupa picha kwamba haitoshi tu kuitazama Katiba pekee kama chombo kinachoweza kuleta mabadiliko ya mfumo wa maisha katika jamii.
Hii inatukumbusha kwamba ni lazima tutazame mgongano wa kitabaka uliopo na uhusiano wa uzalishaji mali kiujumla, maana ndipo kilipo kiini cha matatizo ya kijamii.
Kwa mfano, Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 katika ibara ya 11 inaeleza kuhusu haki ya kufanya kazi, elimu na nyinginezo. Lakini ukija katika mfumo wa uchumi katika jamii ambao una matabaka ya walalahoi na walalaheri, elimu bora inauzwa kwa wachache wenye uwezo wa kifedha. Elimu imekuwa biashara.
Kwa hiyo, si suala tu la Katiba inasemaje, lakini lazima tutazame hiyo Katiba ipo ndani ya tabaka lipi?
Ni nini kinahitajika? Wapo wanaofikiri kwamba Katiba ni zao la siasa tu, lakini ukweli ni kwamba Katiba nayo ni zao la mfumo wa uchumi unaotawala, unaotokana na mgongano wa kitabaka.
Kwa maana nyingine, ni zao la siasa – uchumi. Ndiyo maana tukitaka kuangalia utekelezaji wa Katiba hatuna budi kutazama pia mfumo wa uchumi unaoongoza.
Mwandishi ni Mhadhiri Msaidizi katika Kitengo cha Sosholojia na Ustawi wa Jamii Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).
+255683961891/+255659639808