Majira ya jioni leo Januari Mosi 2018 zimesambaa taarifa kupitia mitandao ya kijamii kwamba, mchora katuni maarufu Tanzania, Masoud Kipanya amekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya uchochezi.
Taarifa hizo zinadai kuwa, Masoud Kipanya ambaye pia ni mtangazaji wa Clouds FM, amekamatwa na Polisi baada ya kuchora katuni ambayo inajenga uhasama kati ya wananchi na serikali.
Baada ya kuibuka kwa utata huo, mwajiri wa Masoud Kipanya, Clouds Media Group (CMG), ilimtafuta Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya DMS, Lazaro Mambosasa ili athibitishe kama kweli amekamatwa
Lakini Lazaro Mambosasa alisema yeye hana taarifa ya kukamatwa na amesema kama kuna mtu anafahamu kituo gani amekamatwa atoe taarifa juu ya kituo hicho cha polisi alichokamatwa
“Uongozi wa Clouds Media Group (CMG) unawaomba wananchi wote nafasi ya utulivu wakati tukiendelea kuzifanyia kazi taarifa kamili wapi alipo Masoud Kipanya. Uongozi utaoa majibu ya kina.”
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam bado halijatoa taarifa kama linamshikilia mtangazaji huyo ama la.
Masoud amekuwa akichora katuni zinazoelezea masuala mbalimbali yanayoigusa jamii kuanzia kwenye uchumi, siasa, masuala ya kijamii na pia kitamaduni.