Mkataba wa ajira ni sawa na mikataba mingine. Huingiwa kwa hiari ya wahusika na wahusika hao hao waweza kuondoka katika mkataba huo kwa hiari zao. Tuzungumzie mwajiri kuamua kujitoa katika mkataba wa ajira.
Mwajiri anaweza kujitoa katika mkataba wa ajira. Mwajiri kujitoa katika mkataba wa ajira maana yake ni kumsimamisha kazi mwajiriwa. Si kosa kumsimamisha kazi mwajiriwa, bali ni kosa kumsimamisha kazi mwajiriwa bila kufuata utaratibu wa sheria.
Hapa chini tutaona mambo muhimu ambayo ni haki kwa mwajiriwa japo wote mwajiriwa na mwajiri wanatakiwa kuyajua ili haki na wajibu viweze kutimizwa.
Taarifa ya kuvunja mkataba (Notice)
Notisi hubeba taarifa za kusudio la kuvunja mkataba na sababu za kuvunja mkataba.
Mambo ya kuzingatia ni haya:
(a) Kwa mkataba wa ajira ambao malipo yake ni ya kila mwisho wa mwezi (monthly pay contract) notisi yake inatakiwa kutolewa ndani ya siku 28 kabla ya siku ambayo mkataba unatarajiwa kuvunjwa.
(b) Kwa mikataba ambayo ni ya siku moja moja au wiki kwa wiki, basi mwajiriwa anatakiwa kutoa notisi ya ya siku 4 kabla ya siku ya kuvunja mkataba.
(c) Kwa mkataba wa ajira ambao unatakiwa kuvunjwa ndani ya mwezi mmoja tokea kuingiwa kwake, basi notisi ya siku saba kabla inatakiwa kutolewa na mwajiriwa.
(d) Ikiwa mkataba unacho kipengele kinachoongelea notisi na muda wake, basi muda huo hivyohivyo ulivyo katika kipengele hicho unatakiwa kufuatwa.
Gharama za kumrudisha mwajiriwa alikotolewa (repatriation expenses)
Sehemu ulikofanyia usaili na kusaini mkataba ndiyo sehemu inayohesabika kuwa eneo lako la kazi la asili. Ukihamishwa kutoka hapo kwenda wilaya, mkoa au nchi nyingine, basi hili litakuwa ni eneo jingine la kazi.
Na ikiwa mkataba utavunjwa ukiwa eneo jingine la kazi, basi unastahili kupata gharama za kurejeshwa eneo lako la kazi la asili.
Mosi, unaweza kupatiwa posho na kujisafirisha mwenyewe.
Pili, unaweza kupatiwa usafiri wa kukusafirisha badala ya posho.
Usafirishaji unakuhusu wewe mwenyewe mwajiriwa, mizigo yako na familia kama unayo. Gharama za chakula na sehemu ya kulala njiani zinajumuishwa kama zipo.
Cheti cha utumishi/huduma (Certificate of Service)
Ni cheti ambacho huwa kinathibitisha kuwa fulani alihudumu sehemu fulani, kwa cheo fulani, ndani ya muda fulani na huduma yake ilikuwa nzuri kwa kiwango fulani. Cheti hiki humsaidia mwajiriwa kupata ajira katika eneo jipya kwa wepesi na uaminifu.
Lakini pia hukuza wasifu wa mwajiriwa na huondoa dhana kuwa yawezekana mwajiriwa aliondolewa kwenye kazi husika kwa makosa ya kinidhamu nk.
Malipo ya kisheria na kimkataba
Malipo yote ya kisheria na kimkataba yalipwe kwa mwajiriwa kabla ya mkataba kusitishwa. Haya ni pamoja na mishahara anayodai kama ipo, posho zake zote, overtime kama zipo, likizo kama zipo, kifuta chozi (severance pay), na malipo yote ambayo anastahili na yapo kimkataba.