Katika toleo lililopita mwandishi wa makala haya alieleza jinsi mfanyabiashara anayeanza kufanya biashara anavyoweza kulipa kodi yake ya mwaka sasa anatoa mfano jinsi ya utaratibu wa ulipaji wa kodi hiyo endelea
Ilipofika Juni 30, 2013 aliwasilisha TRA ritani yenye kuonesha mapato (faida) ya Sh 12,000,000. Ni kiasi gani cha kodi atalipa wakati wa kuwasilisha ritani yake ya mapato kwa mwaka wa mapato wa 2012?
Jibu: Iwapo viwango vya kodi vilivyoanza kutumika mwaka wa fedha wa 2012/13 Jedwali la kwanza kodi ya mwisho ya mwaka itakokotolewa kama ifuatavyo:-
1,350,000 + 30% (12,000,000 – 8640, 000) = 2,358,000
Hivyo kodi ya kulipa itakuwa ni Sh 2,358,000 – Sh 1,600,000= Sh 758,000
(iii) Riba inayotozwa kwa kuweka makadirio ya awali kidogo.
Walipakodi wanashauriwa kuwa waangalifu sana wanapojikadiria mapato na kodi ya awali ya kulipa. Kwa mujibu wa sheria inatakiwa isiwe pungufu ya asilimia 80 ya kodi halisi ambayo anastahili kulipwa. Kwa kutumia mfano hapo juu ni dhahiri Kambale atatozwa riba kwa kujikadiria chini ya asilimia 80 yaani Sh 1,600,000 ÷ Sh 2,358,000 x 100%= 68%. Kiwango cha riba ni kile ambacho kimeidhinishwa na Benki Kuu (BoT) mwanzoni mwa mwaka wa kalenda.
Je, ufanyaje kama umejikadiria kodi kidogo?
Iwapo mlipakodi atagundua kabla ya mwaka kuisha kuwa makadirio ya awali ni pungufu ukilinganisha na hali halisi inavyojionesha, anaruhusiwa kisheria kufanya marekebisho yanayostahili ili kuepukana na tatizo la kutozwa riba baadaye.
(iv) Kosa la kutokulipa kodi kwa muda unaotakiwa.
Kutokana na vyanzo kutoka katika wavuti ya TRA inaeleza kuwa mfanyabishara anayeshindwa kulipa Kodi ya Mapato kwa muda uliopangwa, hutozwa riba kwa kutumia kiwango kilichoidhinishwa na Benki Kuu mwanzoni mwa mwaka wa kalenda. Pia zipo njia nyingine za ukusanyaji kisheria pale ambapo mlipakodi anakuwa mgumu kulipa kwa hiari ikiwa ni pamoja na kuuzwa mali za mdaiwa.
Hasara katika biashara
Endapo wakati wa kutengeneza hesabu za biashara ili kupata mapato ya kutozwa kodi katika mwaka wa mapato, ikitokea kwamba hasara imepatikana, basi hasara hiyo inaruhusiwa kuhamishiwa katika miaka ya mapato inayofuata na kupunguzwa kutoka katika mapato ya miaka hiyo bila kuwa na kikomo.
Hata hivyo, hasara inayopatikana kutoka kwenye shughuli za kilimo au uwekezaji katika rasilimali hairuhusiwi kupunguzwa na mapato kutoka kwenye biashara nyingine.
Malalamiko juu ya makadirio ya kodi
Mojawapo ya haki za mlipakodi ambazo zimeainishwa katika Mkataba na Mlipakodi (Taxpayer’s Charter) ni kupanga makadirio ya kodi iwapo anaamini kuwa si sahihi.
Taratibu za kupinga makadirio ya kodi ni kama ifuatavyo: Kuandika barua kwa Kamishna ikieleza sababu za msingi zenye kuonesha makosa yaliyofanywa katika ukadiriaji. Barua ya kupinga makadirio ni lazima iwasilishwe katika muda wa siku 30 toka tarehe ya makadirio husika.
Mlipakodi anatakiwa kulipa kodi ambayo ni kubwa kati ya kodi ambayo haina malalamiko au 1/3 ya kodi yote iliyoliyokadiriwa.
Baada ya kupokea malalamiko, Kamishna anatakiwa kumtafuta mlalamikaji akikiri kupokea barua ya malalamiko na iwapo barua hiyo inakidhi matakwa ya sheria. Iwapo mlipa kodi hajaridhika na uamuzi wa TRA bado ana haki ya kukata rufaa kwenye vyombo vya kutoa haki, yaani Baraza la Rufaa za Kodi au Mahakama Kuu ya Rufaa za Kodi kwa uamuzi ya mwisho.
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) 1997
VAT ni kodi ya mlaji inayotozwa kwenye bidhaa na huduma zinazostahili kutozwa VAT zinazozalishwa hapa nchini na kwenye bidhaa au huduma zinazoingia Tanzania Bara kutoka nje ya nchi. VAT hutozwa kuanzia ngazi ya uzalishaji wa bidhaa, uuzaji wa jumla, reja reja mpaka bidhaa inapomfikia mlaji wa mwisho. Hii ina maana kuwa mlipaji wa kodi hii ni mlaji au mtumiaji wa bidhaa au huduma.
Usajili
Ili kuingia katika wigo wa kulipa VAT, mfanyabiashara anatakiwa kusajiliwa na kupata cheti cha usajili kinachotolewa na Kamishna kutoka TRA. Masharti ya kusajiliwa ni haya yafuatayo, Kuwa na Namba ya uthibitisho wa mlipa kodi (TIN); kuwa na kiwango cha mauzo yanayostahili kutozwa VAT kwa mwaka kinachozidi au kinachotarajia kuzidi Sh 40,000,000 kwa mwaka.
Pia kujaza fomu za maombi ya kusajiliwa kwa mujibu wa maelekezo, mfanyabiashara aliyesajiliwa na VAT anawajibika kununua na kutumia mashine maalum za kielektroniki za kutolea risiti (Electronic Fiscal Devices – EFDs).
Ni kosa kisheria kwa mfanyabiashara ambaye hatatumia mashine hizi. Ikumbukwe kuwa kwa mfanyabiashara ambaye amekidhi sharti la pili hapo juu atakuwa amevunja sheria kama hatasajiliwa katika kipindi cha siku 30 tangu alipogundua kuwa mauzo yake yanastahili kutozwa mauzo yake VAT yanazidi kiwango cha usajili na hivyo anaweza akatozwa faini, kifungo au vyote — faini na kifungo.
Pamoja na utaratibu huo wa kujisajili, Kamishna anayo madaraka ya kumsajili mtu yeyote iwapo ataona inafaa ili kulinda maslahi ya kiuchumi ya Taifa na kuzuia uvunjaji wa mapato ya Serikali.
Namna VAT inavyokokotolewa
Mfanyabiashara anapouza bidhaa au kutoa huduma inayostahili kutozwa VAT, anatakiwa kutoza VAT kwa kutumia kiwango kilichopo kwenye sheria.
Kiwango cha asilimia 18 ndicho kinachotumika kwa sasa. Kodi inayotozwa na mfanyabiashara anapouza inaitwa “kodi kwenye mauzo” (output tax), na kodi inayolipwa na mfanyabiashara kwenye manunuzi ya bidhaa au huduma inaitwa “kodi kwenye manunuzi” (input tax).
Baada ya mwezi kupita, kinachotakiwa kufanywa na mfanyabiashara ni kulinganisha kiasi cha kodi kwenye mauzo na kile cha kwenye manunuzi.
Iwapo kodi kwenye mauzo ni kubwa kuliko kwenye manunuzi basi mfanyabiashara atatakiwa kulipa TRA ile tofauti ya kodi. Lakini iwapo kodi kwenye manunuzi ni kubwa kuliko kwenye mauzo ina maana kuwa mfanyabiashara atakuwa anadai TRA.
Kiasi hicho kinachodaiwa kinaweza kikafidiwa na kodi ya miezi inayofuata au mfanyabiashara akaomba kurejeshewa kwa kuzingatia taratibu za marejesho ikiwa ni pamoja na kuwa na ankara za malipo (tax invoice) au risiti za kodi zinazotolewa na mashine za kutolea risiti za kielectroniki (fiscalized receipts).
Marejesho yanafanywa baada ya maombi ya mrejesho kukaguliwa na kuridhishwa na mhasibu aliyesajiliwa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi na pia amesajiliwa na TRA kama mtaalamu wa masuala ya kodi.
Mfano, Juma ni mfanyabiashara wa kuuza maji ya kunywa ya chupa kwa jumla na amesajiliwa na VAT. Iwapo Januari 2012 alinunua maji kiwandani kwa bei ya Sh 80,000,000 bila VAT, katika kipindi hicho aliuza maji yote bila VAT kwa bei ya Sh 120,000,000, Juma atatakiwa kulipa TRA kodi ya VAT kama ifuatavyo:-
Kodi kwenye mauzo
Sh 120,000,000 X 18%= Sh 21,600,000
Toa: Kodi kwenye manunuzi
Sh. 80,000,000 X 18%= Sh 14,400,000
Kodi ya kulipa ni Sh 7,200,000
Iwapo zipo gharama nyingine za kibiashara ambazo mfanyabiashara amelipa VAT kama umeme, usafirishaji na ana uthibitisho, itabidi kupunguza kodi ya kulipa TRA.
Kumbuka
VAT siyo mzigo kwa upande wa mfanyabiashara bali hulipwa na mlaji au mtumiaji wa mwisho. Mfanyabiashara ni wakala wa kutoza kodi na kuwasilisha TRA.
Ulipaji wa VAT
Mfanyabiashara aliyesajiliwa anatakiwa kujaza ritani ya kila mwezi husika kwa njia ya mtandao au kwa kuwasilisha kwenye ofisi za TRA mnamo au kabla ya siku ya mwisho ya kati ya mwezi unaofuata. Ritani inatakiwa iambatane na malipo ya kodi au ushahidi wa kuonesha kuwa kodi imelipwa. Mfano, iwapo ritani inayotakiwa kuwasilishwa ni ya mwezi wa Agosti, basi tarehe ya mwisho ya kuwasilisha ritani na kulipa kodi itakuwa tarehe ya siku ya mwisho ya kati ya mwezi Septemba.
Bidhaa zilizosamehewa VAT
Kutokana na sababu mbalimbali za kijamii na kiuchumi, Tanzania haina utaratibu wa kutoza kodi ya VAT kwenye kila kitu. Baadhi ya bidhaa hutozwa VAT kwa kiwango cha asilimia 0 na nyingine zimesamehewa kabisa.
Baadhi ya bidhaa ambazo hazitozwi kodi ya ongezeko la thamani ni kama vyakula ambavyo havijasindikwa: Kama mahindi, ngano, unga wa mahindi na ngano na nafaka nyingine, matunda yasiyosindikwa, mbogamboga na karanga, nyama ya kuku, ng’ombe, samaki na mayai.
Bidhaa na huduma nyingine zilizosamehewa ni dawa za binadamu zilizotajwa na Wizara ya Afya, huduma za tiba kama meno na magonjwa mbalimbali, magazeti, majarida na vitabu, mbolea na dawa za kilimo, usafirishaji wa abiria kwa kutumia basi, treni, ndege, meli na vyombo vingine vya usafiri isipokuwa biashara ya taksi, gari za kukodi, boti na ndege za kukodi.
Huduma za elimu zinazotolewa na taasisi yoyote iliyosajiliwa na Serikali, uuzaji au upangishaji wa nyumba za kuishi au ardhi, huduma za mazishi na: huduma za fedha bidhaa zinazotozwa kwa kiwango cha asilimia 0 ni bidhaa zinazokwenda nje ya nchi na kuuzwa huko. Kwa hiyo, mfanyabiashara ambaye amesajiliwa VAT na akauza bidhaa zake nje ataruhusiwa kupata marejesho ya kodi aliyolipa kwenye manunuzi ingawa hakuna kodi aliyokusanya kutoka kwenye mauzo yake.
Sheria ya Ushuru wa stempu 1972
Sheria ya ushuru wa stempu ya mwaka 1972 haijafutwa, bali yamefanyika mabadiliko kwa kufuta ushuru wa stempu kwenye risiti za mauzo ya bidhaa au huduma inayohusu biashara. Baadhi ya walipakodi wanafikiri kuwa sheria yote imefutwa, la hasha, ni mabadiliko tu yalifanyika katika sheria husika.
Ushuru wa stempu
Ushuru wa stempu bado unatozwa kwenye hati za kisheria au mikataba mbalimbali kama mikataba ya kuuziana nyumba, viwanja, mashamba au vyombo vya moto. Kiwango cha ushuru wa stempu ni asilimia 1 au kiasi chochote kisichozidi asilimia 1.
Muda wa kulipa ushuru w stempu
Ushuru wa stempu unatakiwa kulipwa ndani ya siku 30 baada ya kusaini hati au mkataba.
Utunzaji wa kumbukumbu za biashara
Sheria zote za kodi zinasisitiza suala la utoaji wa risiti na utunzaji wa kumbukumbu sahihi. Pamoja na kwamba ni matakwa ya kisheria pia utunzaji wa kumbukumbu una faida kubwa kwa mfanyabiashara kama ifuatavyo:-
Kujua mwenendo na maendeleo ya biashara iwapo kuna faida au kuna haja ya kuboresha zaidi, ili makadirio ya kodi yawe bora na sahihi, wafanyabiashara wote wanatakiwa kuwa na kumbukumbu sahihi za biashara ili ziwe kigezo sahihi cha makadirio ya kodi. Pale mlipakodi anapokuwa na tatizo au malalamiko kuhusu kodi aliyokadiriwa na Kamishna, kumbukumbu sahihi zitasaidia sana katika kutatua malalamiko na kuepukana na usumbufu.
Kuhalalisha unayofanya endapo kumbukumbu inazohusika na biashara yako zitakuwepo, utumiaji wa Mashine za Kodi za Kielekroniki za Kutolea Risiti (FEDs). Biashara yoyote ile ni lazima iende na wakati na iwe ya kisasa ili iweze kukua na kuwa na mwonekano kiuchumi kwa wadau. Serikali iliamua kuanzisha mfumo wa utoaji risiti kwa kutumia mashine za kielektroniki za kodi. Utaratibu huu ulianza rasmi Julai 1, 2010 kwa wafanyabiashara waliosajiliwa na VAT ikiwa ni awamu ya kwanza.
Awamu ya pili, kuanzia Julai 2013, Serikali imeamua kwamba biashara yoyote yenye mauzo zaidi ya Sh milioni 14 kwa mwaka, lazima iwe na mashine za kodi za kutolea risiti za kielektroniki.
Ni mashine bora zitakazoboresha kumbukumbu na biashara zako.
Itaendelea wiki Ijayo