NA CHRISTOPHER MSEKENA

Wiki iliyopita Staa wa Bongo Fleva, Rayvanny, ameteka mitandao ya kijamii baada ya kutangaza kuachana na Lebo ya WCB inayomilikiwa na Diamond Platnumz.

Hatua hiyo imekuja baada ya Rayvanny kuwa mkubwa kiasi cha kuona sasa anaweza kujisimamia yeye mwenyewe akiwa katika lebo yake ya Next Level Music aliyoitambulisha mwaka jana.

Rayvanny ndiye alikuwa msanii mwenye mafanikio makubwa zaidi katika tasnia ya muziki kutoka WCB, kuanzia kwenye namba za mauzo ya muziki hadi kupata tuzo kubwa duniani ya BET.

Makala hii inaangazia mambo matano muhimu ambayo Rayvanny anapaswa kuzingatia akiwa nje ya WCB ili azidi kufanikiwa, asipotee kama walivyopotea kina Rich Mavoko, Q Boy Msafi na wengine waliojiondoa katika lebo hiyo yenye wafuasi na mashabiki wengi.

Alinde uhusiano wake na Diamond

Uhusiano wa Rayvanny na Diamond haupaswi kufa kwa namna yoyote ile. Rayvanny analazimika kuulinda huo uhusiano kwa kuendelea kumheshimu Diamond na kumpa nafasi ya baba ili wafuasi wao waendelee kumpa sapoti hata kama ametoka WCB.

Wasanii wote waliopotea punde baada ya kutoka WCB, walitengeneza kitu kama ‘bifu’ na Diamond, jambo lililoibua vita iliyoishia kuwapoteza na kuwafanya wawe wasanii wa kawaida na wasiwe juu kama walivyokuwa chini ya WCB.

Kitendo cha Rayvanny kuaga kwa heshima kimemuongezea nafasi ya kupendwa zaidi na mashabiki wa Diamond na pengine ataendelea kupewa sapoti kubwa kama aliyokuwa akipewa kipindi alichokuwapo WCB.

Atengeneze wafuasi wake binafsi

Hadi sasa asilimia kubwa ya mashabiki wa Rayvanny ni wale wale wa WCB, kwa hiyo anakabiliwa na changamoto ya kuumba wafuasi wake binafsi watakaokuwa nguzo ya muziki wake.

Wafuasi hao wapya watakuwa na nguvu ya kumpigania yeye na muziki wake hata ikitokea siku mashabiki wa WCB wakaacha kumsapoti, asitetereke.

Asiridhike na mashabiki wa WCB wanaoendelea kumpa sapoti, kwa sababu tu ameondoka vizuri WCB, tunafahamu kwamba huko mbeleni chochote kinaweza kutokea baina yake na mashabiki hao wa Diamond, hivyo ni muhimu sasa Rayvanny akawa na wafuasi wake binafsi.

Achukue uzoefu kwa Harmonize

Harmonize anaweza kuwa somo zuri kwa Rayvanny kwa sababu ndiye msanii aliyeweza kuvumilia mikikimikiki ya mashabiki wa WCB hadi amefanikiwa kujenga ufalme wake wa Konde Gang.

Si jambo baya kwa Rayvanny kujifunza kwa Harmonize mbinu alizotumia ili kuweza kubaki katika chati, kiasi kwamba ukiwatazama wasanii watatu wakubwa Bongo ni Diamond, Alikiba na Harmonize.

Uzuri ni kwamba tangu walipokuwa WCB walikuwa ni marafiki, hivyo si jambo baya Rayvanny akimtafuta Harmonize ili apewe mbinu nyingine za kuishi vizuri nje ya Wasafi.

Asawazishe bifu zote, awe huru

Akitaka aendelee kuwa katika chati baada ya kuondoka WCB ni lazima asawazishe bifu na migogoro yote ambayo WCB waliingia na wadau wa muziki.

Inafahamika kwamba ukiwa msanii wa WCB kuna redio haziwezi kucheza muziki wako. Huwezi kufanya mahojiano na vyombo fulani vya habari, kwa muktadha huo Rayvanny anapaswa kuweka mambo sawa ili awe msanii huru kufanya kazi na kila mdau.

Akijidai kuendeleza bifu za Wasafi na wadau wa muziki, awe na uhakika kwamba hataweza kustahimili, na hilo ndilo litakuwa anguko lake. Muhimu aweke mambo sawa, awe rafiki wa kila mtu ili azidi kuvuma.

Asiache kuwekeza katika biashara ya muziki

Ukiangalia wasanii wote waliopotea punde baada ya kutoka WCB walipunguza uwekezaji katika muziki. Walikuwa wanafanya uwekezaji wa kawaida tofauti na walivyokuwa kwenye lebo.

Rayvanny atazidi kustawi endapo ataendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika muziki wake, kwa kufanya video za gharama sambamba na ubunifu kwenye kazi ili azidi kutoboa kwa kipindi hiki ambacho kila mtu anamtazama kama ataweza kustawi akiwa nje ya WCB.

Akipunguza ubunifu katika kazi zake atafanya mashabiki wa muziki wamuone kuwa ni msanii wa kawaida, tofauti na alivyokuwa WCB, kwa kuwa tuliona uwekezaji mkubwa ukifanyika katika kazi za audio na video zake.

[email protected]