Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Tabora
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia mwanamke mmoja kwa tuhuma za kuwaua watoto wawili wa familia moja kwa kuwanywesha sumu.
Kamanda wa Polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Richard Abwao, amethibitisha kutokea tukio na kubainisha chanzo cha mauaji hayo ni baada ya kutokea ugomvi kati ya baba wa watoto hao Zakaria Dotto na mtuhumiwa mbaye alikuwa ni mama wa kambo.
Kamanda amewataja watoto waliouawa kuwa ni Dickson Zakaria (5) na Goodluck Zakaria (4) ambao walikuwa wanaishi na baba yao mzazi na kulelewa na mama huyo.
Kamanda amesema kuwa mtuhumiwa aliwanyweshwa sumu watoto hao aina ya super feed NPK na bens attack 344se inayotumika kuulia wadudu kwenye mazao.
Akizungumzia chanzo cha tukio hilo kama amebainisha kuwa ugomvi huo ulisababishwa na baba wa watoto hao kutotoa huduma za kifamilia ambapo baada ya kuona mzozo unazidi baba mzazi wa watoto hao aliamua kuondoka na kuacha watoto na mama yao huyo wa kambo.
Kamanda ameeleza kuwa mama huyo aliamua kuchukua sumu hiyo iliyokuwemo ndani akaikoroga kwenye kikombe na kuwanywesha watoto hao na yeye mwenyewe akanywa.
Ameongeza kuwa baba wa watoto aliporudi alikuta mke wake huyo akitapika sana na watoto wamelala ambapo aliamua kumpeleka hospitalini bila kujua kilichotokea kwa watoto pia.
Amefafanua kuwa aliporudi nyumbani kwenda kuangalia watoto akakuta wameshafariki na alipokwenda kumuuliza mke wake kuhusu watoto akamjibu kuwa amewanywesha sumu ya kuulia wadudu.
Kamanda Abwao amesema kuwa mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Polisi na atafikishwa mahakamani muda wowote ili kujibu tuhuma za mauaji zinazomkabili.