Ikiwa ni miezi mitatu tangu Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Frank Msaki, asimamishwe kazi kutokana na tuhuma za kufanya malipo hewa ya posho za chakula kwa askari, JAMHURI imebaini yaliyojificha nyuma ya sakata hilo.
Tuhuma hizo zilimsukuma Rais, Dk. John Magufuli kuagiza kuondolewa kwa watumishi raia katika majeshi ya ulinzi na usalama nchini, jambo ambalo tayari limeshaanza kutekelezwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Vyanzo vyetu kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, vimesema malipo hewa yaligunduliwa na mmoja wa watumishi kitengo cha uhasibu ambaye alikuwa akipitia orodha ya askari wanaotakiwa kulipwa posho ya chakula, akakuta namba yake ya ajira katika orodha hiyo wakati yeye si askari na hakustahili kupata malipo hayo.
Taarifa zaidi zinasema, afisa huyo alilazimika kuhakiki namba hiyo na baada ya kujiridhisha na kufungua jina alikuta si lake huku namba iliyotumika ni yake, hivyo kutoa taarifa kwa mamlaka za juu za uhasibu ndani ya jeshi hilo.
“Viongozi wote wakubwa walikuwa Dodoma kwa ajili ya Bunge la Bajeti, walipigiwa simu na kuelezwa kilichopo kwenye orodha ya malipo, yalitoka maelekezo kwamba afanye uhakiki wa orodha nzima na kubaini watumishi hewa zaidi.
“Alihakiki na kugundua ya kuwa kuna udanganyifu zaidi katika orodha hiyo, Mhasibu Mkuu aliwafahamisha maafisa aliokuwa nao bungeni, hapa ofisini kuna askari anayehusika na kuandaa orodha ya askari wanaopaswa kulipwa posho, siku hiyo hakuwapo ofisini, hivyo aliitwa afisa mwingine ambaye ni raia afanye kazi hiyo, akagundua madudu haya,” anasema mtoa taarifa.
Inaelezwa kuwa uchunguzi uliofanywa na ofisi ya uhasibu ulibaini kuwa malipo hewa yamekuwa yakifanywa kupitia akaunti katika moja ya mabenki (jina tunalo) hapa nchini, huku wahusika wakiwa hawajabainika.
Taarifa iliyotolewa Julai, mwaka huu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, ilieleza kumsimisha kazi Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Frank Msaki, kutokana na tuhuma za kufanya malipo hewa ya posho ya chakula kwa watu ambao si askari.
“Frank Msaki amesimamishwa kazi kwa kufanya malipo ya kiasi cha shilingi milioni 305, kama posho ya chakula kwa watu ambao sio askari kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2015/2016,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu huyo amesema kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kijeshi, anayetakiwa kulipwa posho ya chakula yaani ‘ration allowance’ ni askari peke yake na si mtu mwingine yeyote.
Meja Jenerali Rwegasira alibainisha kuwa baada ya jalada la uchunguzi kufunguliwa na ukaguzi maalumu kufanywa na Mkaguzi wa Ndani wa Jeshi la Polisi, imebainika kuwa mbinu mbalimbali zimetumika ili kufanikisha malipo hayo hewa.
Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani, anasema kuwa ofisi yake inaendelea na uchunguzi wa suala hilo na kuwa unatakiwa kumalizika hivi karibuni.
“Sisi tunafanya upepelezi wetu, pia Mkurugenzi wa Mashtaka naye anafanya kazi yake kama wanavyotakiwa na kama kuna mashtaka naye atatimiza wajibu wake kama anavyotakiwa,” anasema DCI Athumani.
Utaratibu wa malipo ya posho za askari polisi nchini
Hati ya malipo ya posho ya chakula hupitia katika hatua mbalimbali ili kukamilika ambapo Mkuu wa kitengo cha mishahara pamoja na wafanyakazi waliopo chini yake, wamekuwa wakishirikiana na kitengo cha utawala kuandaa orodha ya askari wanaostahili kulipwa posho za kila mwezi.
Baada ya kukamilika kwa orodha hiyo, Mkuu wa kitengo cha fedha hutengewa fedha kwa ajili ya malipo ya posho za chakula kwa mwezi akiwa ameambatanisha orodha ya askari wanaotakiwa kulipwa posho hizo.
Kamishna wa Fedha hujiridhisha na usahihi wa orodha hiyo pamoja na kiasi cha fedha kinachopaswa kulipwa, na baadaye huandaa barua kwenda benki husika akiwaomba kuwalipa askari posho zao moja kwa moja kupitia akaunti zao binafsi.
Baada ya benki kulipa posho hizo, maandalizi ya hati ya malipo zilizotolewa awali, huandaliwa na kitengo cha mishahara mara baada ya kupokea hundi ya posho kutoka Hazina. Hati hiyo huambatanishwa na orodha ya askari wanaostahili posho za chakula.
Hati hiyo ya malipo hufanyiwa kazi na kitengo cha ukaguzi wa awali (Examination) ili kuhakiki usahihi wake ikiwa ni pamoja na kujiridhisha iwapo malipo hayo yameidhinishwa na mkuu wa kitengo cha fedha.
Baada ya kitengo cha ukaguzi kujiridhisha, hati ya malipo hukabidhiwa kwenye kitengo cha uhasibu ili iingizwe katika mtandao wa kompyuta na baada ya hapo hupelekwa na kukabidhiwa kwa Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kitengo cha mishahara pamoja na kitengo cha utawala, ndiyo wanaoshirikiana kuandaa orodha ya askari wanaostahili kulipwa posho ya chakula.
Mkuu wa kitengo cha fedha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Ndallo Shihango, amekataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa yeye si msemaji wa Jeshi la Polisi.
“Umesema wewe ni nani? Humjui msemaji wa Jeshi la Polisi? hapa tuna utaratibu wa kuwa na msemaji mmoja. Mimi si msemaji, mtafute msemaji atakujibu unalotaka kulifahamu,” anasema SACP Ndallo.
Alipotafutwa kuzungumzia sakata hilo, Mkaguzi wa Ndani wa Jeshi la Polisi, Saisita Makanda, amesema taarifa yoyote ya Jeshi la Polisi hutolewa kwa kufuata taratibu.
“Nakuomba uwasiliane na wasemaji wa Jeshi la Polisi ndiyo wanaoweza kukupatia taarifa maana ndiyo kazi yao,” anasema Makanda.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Advera Bulimba, katika mahojiano na gazeti hili amesema kwamba jambo la aina hilo hawezi kuliongelea kwenye simu kwa kuwa ni mambo ya ndani yanayohitaji kuzungumzwa kwa kina.
Hata hivyo, mwandishi wa JAMHURI alipomuomba aende kumuona ofisini kwake, alisema kuwa muda wa kazi umekwisha hivyo itakuwa vigumu kuruhusiwa kuingia ofisini kwake.
“Unajua haya mambo huwezi kuongea kwenye simu, lazima nijue wewe una nini nami niweze kufuatilia kwa kina, siwezi kukujibu lolote kwa sasa, wewe njoo wiki ijayo unieleze nifuatilie nikujibu,” anasema Advera.
Rais Magufuli alihoji sababu za kuwapo watumishi raia katika majeshi ikiwa ni pamoja na polisi na kuagiza watumishi watakaoajiriwa wawe ni askari, akilenga kupeleka nidhamu ya jeshi kwenye idara ya uhasibu.
“Hao watumishi ambao ni raia muwapeleke Utumishi, kwani hakuna polisi ambao wamesomea uhasibu, uhandisi na masuala ya utawala? Matatizo ya wizi wizi pamoja na yale ya watumishi hewa, kama yataletwa na raia, IGP kaorodheshe majina yao wote watoke,” alinukuliwa Rais Magufuli.
Baada ya kutoa agizo hilo, Jeshi la Polisi lilianza kuangalia njia za kutekeleza agizo hilo. Kada ya uhasibu ilionekana kulengwa zaidi kutokana na kuwa waajiriwa wa Hazina.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinaeleza baada ya tafakuri, iliamuriwa wahasibu wote ambao ni raia wapelekwe kwenye mafunzo katika Chuo cha Polisi Moshi.
Wahusika wote walipewa taarifa wakitakiwa wajiandae kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi. Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea, viongozi waandamizi wa Polisi walipitia miongozo mbalimbali na kubaini kuwa na wahasibu ambao ni askari kungeleta mtanziko mkubwa kwenye kazi za kihasibu.
“Mwongozo wa kwanza kabisa wa askari ni utii, akiwa mhasibu askari kama koplo hawezi kukataa au kuhoji amri ya mkuu wake inayomtaka atoe fedha. Mhasibu askari anapokaidi maagizo au anaadhibiwa kijeshi, lakini kwa raia hiyo haiwezekani,” anasema mtoa taarifa wetu.