Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefanya Mkutano Mkuu katika Hoteli ya Regal Naivera jijini Tanga. Pamoja na mambo mengine, Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi, amezungumza na JAMHURI mambo mengi, lakini kwa leo anazungumzia mtazamo wake wa soka la Tanzania. Endelea na mahojiano…
Swali: Mashabiki wa soka wana kiu ya mafanikio katika mchezo huu, nini malengo yenu TFF.
Jibu: Kwa kweli azma yetu ni ile ile, kuhakikisha mpira wa Tanzania unakua na sisi tunafikia lengo la kutoa upinzani wa kutosha katika hatua za kimataifa kuanzia ukanda wetu wa CECAFA, Afrika na hatimaye kung’ara duniani.
Swali: Kama malengo ndiyo hayo, kwanini timu za Taifa hazifanyi vema?
Jibu: Naam, baada ya timu yetu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kutofanya vizuri katika michuano ya COSAFA huko Afrika Kusini Mei, mwaka jana, na baadaye kufanya vibaya katika mchezo wa kwanza katika mtoano wa mashindano ya CHAN, Kamati ya Utendaji ya TFF ilichukua uamuzi wa kusimamisha ajira ya kocha wa kigeni, Martin Nooj.
Badala yake kuingia mkataba na makocha wazawa Boniface Charles Mkwasa akisaidiana na Hemed Morocco. Tangu walimu hawa wemechukua timu ya Taifa imekuwa bora na hadi sasa tumefungwa mechi mbili tu za mashindano dhidi ya Algeria na Malawi ugenini, tumetoka sare mbili nyumbani dhidi ya Nigeria na Algeria na kuifunga Malawi nyumbani.
Swali: Vipi kuhusu timu ya Kilimanjaro Stars?
Jibu: Timu ya Kilimanjaro Stars chini ya Kocha Abdallah Kibadeni na msaidizi wake, Juma Mgunda, katika mashindano ya CECAFA Challenge katika mechi nne ilizocheza Ethiopia haikufungwa hata mechi moja katika ‘Open Play’ ingawa ilitolewa kwa penalti tano tano katika hatua ya nusu fainali.
Kipindi chote ambacho tumekuwa na makocha wazawa kiwango cha Tanzania FIFA kimekuwa kikipanda mara zote. Tunawapongeza sana makocha wetu hawa na benchi la ufundi.
Kwa sasa tunajiandaa na mechi za kufuzu kucheza fainali za Afrika AFCON 2017 nchini Gabon. Mechi hizi ni dhidi ya Chad Machi 23, mwaka huu ambako tutacheza ugenini na mechi ya marudiano Dar es Salaam Machi 28, 2016.
Imani yetu ni kuwa timu yetu itaendeleza wimbi la ushindi. Katika kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Nigeria, Taifa Stars iliweka kambi nchini Uturuki na pia timu iliweka kambi Afrika Kusini kujiandaa na mechi dhidi ya Algeria. Kambi hizi zimesaidia sana kuimarisha timu yetu kabla ya mechi hizi kubwa mbili.
Swali: Na ni vipi kuhusu timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars?’
Jibu: Timu yetu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars chini ya Kocha Rogasian Kaijage ilifanikiwa kuitoa Zambia na hivyo kufuzu kucheza fainali za michezo ya Afrika nchini Kongo Brazzaville. Katika fainali hizi, Tanzania ilifungwa na Ivory Coast na Nigeria na kutoka sare na Congo, hivyo kutolewa katika hatua za makundi.
Uzoefu uliopatikana katika mashindano hayo umempa fursa Kocha mpya wa Timu ya Twiga stars, Nasra, kuweza kuunda kikosi kipya kichanga ambacho majuzi kilitoa changamoto kwa timu ya Zimbabwe, imani yetu ni kwamba hii timu itafanya vizuri mechi ya marudiano mjini Harare. Aidha, timu ya Twiga Stars ilipata mechi moja ya majaribio dhidi ya Malawi.
Swali: Vipi kuhusu soka la vijana?
Jibu: Kikosi chetu cha Taifa cha vijana chini ya umri wa miaka 17 (U17) kinachojiandaa na hatua za mtoano Juni, 2016 kilikuwa kifanye ziara ya kimichezo nchini Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya.
Lengo lilikuwa ni kukipatia kikosi hiki uzoefu wa kimataifa. Wakati tayari kikosi kimejiandaa na kukabidhiwa bendera, akaunti za TFF zilifungiwa na TRA na hivyo safari kuvunjika kwa ukosefu wa fedha.
Pamoja na changamoto hiyo, mpango mkakati umefanyika na sasa kikosi hiki kitacheza mchezo mmoja wa kirafiki wa kimataifa hapa Tanzania mwezi ujao, na baadaye kwa hisani ya Chama cha Mpira cha India timu itakwenda India kuweka kambi ya wiki tatu tayari kwa kuikabili Seychelles mwezi Juni. Tunakishukuru Chama cha Mpira cha India pamoja na serikali ya India kwa kutupatia sapoti hii.
Fainali za Afrika U17 mwaka 2019
Maandalizi ya fainali hizi ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji, yanaendelea vizuri na vikao na wizara tayari vimeanza kwa ajili ya kufanya maandalizi muhimu ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Pia maandalizi ya timu itakayoshiriki fainali hizi yameanza kwa vijana umri chini ya miaka 13 (U13) kujumuisha pamoja katika shule ya Alliance mjini Mwanza.
Kocha Kim Poulsen tumemleta mahsusi ili, pamoja na majukumu mengine, atuandalie kikosi cha ushindi cha vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Imani yetu ni kuwa Tanzania tutafanikiwa kuandaa mashindano mazuri mwaka 2019 na pia kunyakua kombe hili.