Ziara iliyofanywa na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, mkoani Njombe hivi karibuni imesaidia kurejeshwa kwa mali za ushirika zilizokuwa zimeporwa na viongozi wasio waaminifu wa ushirika wa eneo la Lupembe, mkoani humo.

Kaimu Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Charles Malunde, amesema hivi karibuni kuwa kutokana na maelekezo ya Bashe, Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na vyombo vya dola wamefanikiwa kurejesha mali mbalimbali za wanaushirika zilizokuwa zimechukuliwa na wajanja wachache kwa kushirikiana na viongozi wa ushirika wa eneo hilo.

Taarifa ya Malunde imezitaja mali zilizopatikana ni pamoja na magari sita yakijumuisha Mitsubishi Canter matatu, Toyota Land Cruiser, Escudo na Rock. 

Pia zimo injini za magari mbili; jenereta; mashine nne za kuvunia chai; shamba moja la chai lenye ukubwa wa ekari 215 na nyumba moja ambayo iko jirani na shamba hilo la chai katika Kitongoji cha Mbingu, Kata ya Lupembe.

Malunde anasema zoezi la urejeshaji wa mali za wanaushirika wa Njombe pamoja na mali za vyama vya ushirika vingine bado linaendelea ili kuhakikisha mali zote za vyama vya ushirika zinarejeshwa na kuwekwa katika mikono salama.

“Huu ni mfano dhahiri kuwa tusipokuwa na viongozi waaminifu na waadilifu hakika juhudi za kufufua na kuimarisha ushirika hazitazaa matunda yoyote. Ni imani yangu kuwa kila mdau akisimamia sehemu yake husika na kuisimamia kwa uaminifu tutarejesha heshima ya ushirika iliyopotea kwa muda sasa. Wanachama wa vyama vya ushirika wana mchango mkubwa katika kufanikisha hili,” anasema.

Wakati huo huo, Malunde amewataka warajisi wasaidizi wa vyama vya ushirika wa mikoa kuwashirikisha viongozi wa vyombo vya usalama wanapolazimika kufanya upekuzi kwa wanachama wanaoomba kugombea uongozi katika vyama vya ushirika.

“Kutekelezwa kwa jambo hilo ipasavyo kutasaidia kuwapata viongozi wenye sifa,” anasema Malunde.

Kupitia taarifa hiyo, Malunde pia amewataka warajisi wasaidizi kuhakikisha kuwa hakuna ubaguzi kwa wanachama wanaotaka kuwania nafasi za uongozi.

“Warajisi wasaidizi na maofisa ushirika walioko katika ngazi za wilaya wahakikishe kuwa viongozi wa vyombo vya usalama katika ngazi ya wilaya wanashirikishwa katika hatua ya upekuzi. Ushirikiano huu utatusaidia kuwapata viongozi waaminifu na waadilifu. Viongozi walioko katika ngazi za vijiji na kata nao wana mchango mkubwa katika kuwapata viongozi wenye sifa zinazotakiwa; hivyo nao washirikishwe katika zoezi la upekuzi,” anasema Malunde.

Anabainisha kuwa ni vema jambo hilo likapewa umuhimu, ikizingatiwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi katika vyama vya ushirika na ametoa rai kwa wanachama kuhakikisha wanawachagua viongozi wenye sifa stahiki watakaowezesha kulinda na kuendeleza mali na masilahi ya wanaushirika.

“Katika kuhakikisha kuwa vyama vya ushirika vinapata viongozi ambao watakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya ushirika nchini, hatuna budi kushirikiana sote katika kuwapata viongozi hao,” anasema Malunde.

Anaonya kuwa kuchaguliwa kwa viongozi wasio waaminifu na waadilifu katika vyama vya ushirika ndiyo chanzo cha mali za wanaushirika kuibwa na hatimaye vyama hivyo kufilisika.

“Mwanachama wa kawaida anaweza kuilaumu serikali bila kujua kuwa viongozi wanaoiba mali za chama chake aliwachagua yeye mwenyewe,” anasema.