Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

OPARESHENI maalumu iliyofanywa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama imefanikisha kukamatwa magunia ya kufungia tumbaku maarufu kama majafafa yenye thamani ya zaidi ya sh bil 1.4.

Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Hussein Bashe amethibitisha kukamatwa marobota ya mali hizo na watuhumiwa 15 waliohusika na wizi huo wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Hussein Bashe akitoa taarifa za kukamatwa kwa mali za wakulima zenye thamani ya zaidi ya sh bil 1.4 kwa Wawakilishi wa Vyombo mbalimbali vya habari leo katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na kuonesha baadhi ya mali zilizokamatwa. Picha na Allan Kitwe.

Waziri Bashe ametaja baadhi ya watu waliohusika katika wizi huo wa mali za wakulima kuwa ni makampuni yanayonunua zao la tumbaku, taasisi za fedha, viongozi wa vyama vya Ushirika na viongozi wa kuchaguliwa na wananchi.

Amemwagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kuchukua hatua mara moja kwa kuwasimamisha kazi Viongozi wote wa vyama vya msingi (Amcos) na vyama vikuu vya ushirika (Union) waliohusika katika wizi huo wa mali za wakulima.

Amesisistiza kuwa kwa miaka 2 Wizara yake imekuwa ikifanya jitihada za kubaini mianya ya wizi wa mali za wakulima, juhudi hizo sasa zimezaa matunda baada ya kunaswa wezi na marobota ya magunia ambayo ni mali ya wakulima.

‘Majafafa ni mali ya wakulima, mnunuzi yeyote anaponunua tumbaku anapaswa kurudisha magunia hayo kwa mkulima ili ayatumie kufungia tumbaku yake msimu unaofuata na sio kumuuzia tena mara ya pili, huu ni wizi,’, ameeleza.

Waziri Bashe ameonya kuwa ni marufuku kwa kampuni yoyote, mabenki au viongozi wa ushirika kuwauzia majafafa kwa kuwa tayari waliyanunua msimu uliopita na wanaweza kuyatumia kwa miaka 2 au 3 kwa kuwa ni mali yao.

Amebainisha kuwa katika oparesheni hiyo iliyofanyika katika Mikoa ya Tabora na Shinyanga wamekamata malori yaliyokuwa yanasafirisha marobota ya magunia hayo, wahusika waliokuwa wakiyasafirisha na wamiliki wa magodauni.

‘Tutafanya uchunguzi wa kina kwa makampuni ya tumbaku, viongozi wa vyama vya ushirika, taasisi za fedha na wafanyabiashara wote, yeyote atakayebainika kufanya uhujumu huu atakiona cha moto na maghala yote yakamatwe’, ameeleza.

Amempongeza Mkuu wa Mkoa huo na timu yake iliyofanya oparesheni hiyo ikihusisha Afisa wa Takukuru, Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi na Idara ya Usalama na kubainisha kuwa oparesheni hiyo itaendelea katika mazao yote.

Waziri Bashe amemwagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku (TTB) kuhakikisha wakulima hawakatwi fedha yoyote ya magunia katika msimu huu wa kilimo na kuelekeza wanunuzi na vyama vya ushirika kugawa majafafa kwa wakulima bure.