Nadharia ya mabadiliko ya viumbe inatuambia kuwa viumbe wanabadilika, wanatoweka na kuja viumbe wapya kila baada ya kipindi fulani cha maisha.

Viumbe waliokuwapo huko mwanzo wa dunia si hawa waliopo leo, na kwa hakika viumbe watakaokuwapo mamilioni ya miaka baada ya leo si hawa tunaowajua.

Mabaki ya viumbe au visukuku (fossils) waliyoyapata wanasayansi chini ya ardhi yanaonyesha kuwa si tu kuwa viumbe wanabadilika, bali kila baada ya kipindi fulani huibuka spishi mpya. Kwa mtazamo wa kisayansi hii ni sawa na kusema uumbaji ni mchakato endelevu.

Kabla ya uwepo wa jamii hizi za mijusi iliyopo leo duniani kama mamba na kenge, huko nyuma takriban miaka milioni 240 hadi miaka milioni 65 iliyopita kulikuwa na mijusi mikubwa ya kutisha iliyoitwa dinosaur.

Wanasayansi wamewagawa dinosaurs katika makundi makubwa mawili kulingana na muundo wa mifupa ya paja na kiuno. Saurischian dinosaurs ni wale wenye mifupa ya kiuno inayofanana na ile ya reptilian. Wale wenye mifupa ya kiuno inayofanana na ndege hutambulika kama Ornithischian dinosaurs.

Licha ya mgawanyo huu bado dinosaurs walikuwa katika maumbo na hulka tofauti tofauti. Wapo wenye miguu minne waliokuwa wakila mimea (sauropods), wengine walikuwa na miguu miwili – wala nyama (theropods), wapo waliokuwa na pembe, ngao au hata magamba.

Mijusi hii ya dinosaur ilidumu na kuitawala dunia kwa takriban miaka milioni 175 na kisha iliangamia (extinction). Sababu halisi iliyosababisha kutoweka kwao bado ni mjadala kwa wataalamu wa visukuku, lakini wengi wanajenga nadharia kuwa kutoweka kwao duniani huenda kulitokana na kuanguka kwa kimondo kizito duniani kilichosababisha madhara.

Wanasayansi wengine wanaamini kutoweka kwa dinosaur kulitokana kama si mabadiliko ya tabia -nchi, basi ni kutokana na milipuko ya volkano.

Ugunduzi wa Tendaguru

Tendaguru ni eneo linalopatikana katika Wilaya ya Lindi Vijijini, takriban kilomita 60 kaskazini magharibi mwa mji wa Lindi. Tendaguru au Tendeguru ni neno la Kimwera, likiwa na maana ya kilima.

Mwaka 1906 wakati huo Tanganyika ikiwa koloni la Ujerumani, kwenye pitapita zake  chini ya mlima (Tendaguru) akienda Mto Mbwemkulu kwenye bonde la Mandawa, Lindi Vijijini, mwanasayansi na mhandisi wa madini, Bernhard Wilhelm Sattler, bila kutarajia aliona mifupa mingi iliyoonekana kama imefukuliwa na maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka mlimani. Jambo lile lilimshangaza na akatoa taarifa Ujerumani. Mwaka mmoja baadaye mtaalamu wa mabaki ya viumbe hai (paleontologist), Eberherd Fraas, akafika Tanganyika na kuchimbua mifupa miwili mikubwa ya dinosaurs.

Kuanzia mwaka 1909 taasisi ya Berlin Natural History Museum ikatuma wataalamu Tendaguru waliongozwa na Werner Janensch na Edwin Hennig. Kwa miaka minne, kuanzia mwaka 1909 hadi 1913 ukaanza uchimbaji na ufukuaji wa eneo la Mlima Tendaguru uliotumia vibarua zaidi ya 500.

Uchimbaji huo uliwezesha kupatikana mifupa na mabaki mengine ya wanyama yaliyofikia uzito wa tani 230. Uchimbaji huu wa Tendaguru unatajwa kama uchimbaji wenye mafanikio zaidi katika utafutaji wa mabaki ya dinosaur. Kuanzia mwaka 1913 mabaki hayo yalibebwa na Watanganyika kwa kilomita zaidi ya 60 kutoka Tendaguru mpaka pwani ya Lindi na kisha kupelekwa Ujerumani.

Museum Fur Naturkunde Berlin

Mabaki ya viumbe hao yalihifadhiwa katika makumbusho inayoitwa Naturkunde Museum nchini Ujerumani kwa madhumuni ya kuyafanyia utafiti na maonyesho ya kitalii. Kulingana na tovuti ya màkumbusho ya viumbe ya Naturkunde, baada ya uchambuzi na upembuzi wa kina wa wanasayansi waligundua kuwa mabaki hayo ya Tendaguru yanajumuisha masalia ya mimea na wanyama mbalimbali, lakini mengi yakiwa ni mabaki ya dinosaurs. Baadhi ya mabaki hayo ndiyo yanayofanywa sehemu ya maonyesho katika makumbusho hayo.

Giraffatitan brancai

Moja ya kivutio kikubwa katika makumbusho hayo ni kiunzi (skeleton) kilichokuwa cha dinosaur aliyefahamika kama Giraffatitan brancai. Dinosaur huyo ni jamii ya Sauropod dinosaur waliokuwa wakitembea kwa miguu minne na wanatambulika kwa shingo zao ndefu kama twiga na mikia mirefu mno. Kiunzi hiki kimetengenezwa katika umbile halisi la mnyama huyo (mounted) na kufikia urefu wa mita 13.7 na kuweka rekodi katika kitabu cha Guinness (Guinness World Records).

Wataalamu wengi wanaamini dinosaur huyu alikuwa na uzito kati ya tani 20 na tani 50. Ukifika katika makumbusho hayo Berlin, kwenye runinga inayotumia teknolojia ya kisasa ya picha na video unapata fursa ya kutazama jinsi kiunzi hiki kinavyoweza kubadilika na kuwa katika umbo halisi la dinosaur anayetembea na kutoa mlio.

Allosaurs

Mabaki mengine yanayoonyeshwa katika makumbusho haya ni Allosaur dinosaur. Aina hii ya mijusi inatambulika kwa uwezo wao wa kutembea kwa miguu miwili na chakula chao kikuu kikiwa ni wanyama. Jamii hii inatambulika pia kama mazimwi (beasts).

Pterosaurs

Hii ni aina ya dinosaur waliokuwa na mbawa na walijaliwa uwezo wa kuruka kama ndege (winged lizards). Mbali na Pterosaurs, mabaki ya Kentrosaurus kutoka Tendaguru pia yanapatika Naturkunde Museum. Kentrosaurus ni jamii ya Stegosaurus, na wanafahamika zaidi kama dinosaur wenye miili ya manundu yalichongoka kuanzia mgongoni hadi mkiani.

Ni muhimu kutambua kuwa kiingilio katika jumba hili la Naturkunde Museum ni Euro 8 (takriban Sh 21,000) na kwa mwaka wanapokea wateja zaidi ya 800,000. Hii ni kusema kuwa makumbusho haya yanaingiza Sh zaidi ya bilioni 16 kwa mwaka mmoja kupitia mabaki ya dinosaur wa Tendaguru; ilhali Watanzania wenye hii rasilimali wakiwa hawaambulii hata senti moja.

Mara kadhaa wabunge wakiongozwa na wabunge kutoka Lindi, akiwamo Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali, wamepaza sauti kuiomba Serikali ya Tanzania iitake Serikali ya Ujerumani iyarejeshe mabaki ya mijusi ya Tendaguru kwa kuwa kama taifa hatunufaiki na urithi huu.

Majibu ya serikali ni kwamba kuyarejesha si tu kutaambatana na gharama kubwa za usafirishaji, bali pia ni jambo lisilo na tija kwa Tanzania kwa kuwa Ujerumani imekubali kufadhili shunguli za utafiti Tendaguru na kusomesha Watanzania kwenye eneo hilo la utafiti wa mabaki ya viumbe hai!

Ni jambo la ajabu sana kwa serikali kuamini kuwa kuyarejesha nyumbani mabaki haya yanayoliingizia Jiji la Berlin mabilioni ya pesa kuliita jambo lisilo na tija na badala yake tunapaswa kupumbazwa kwa ‘misaada’ ya ada kwa wananafunzi na ufadhili usiosemwa wala kujulikana utatekelezwa lini.

Kama serikali ikiamua kwa nguvu ya kidiplomasia, tunaweza kuyarudisha nyumbani mabaki ya mijusi wetu na kupelekwa tena eneo la Tendaguru yalikotolewa na kutengenezewa makumbusho mkoani Lindi na kuwa kivutio kwa watalii.

Fedha zitakazopatikana zitasaidia, pamoja na mambo mengine, uhifadhi wa msitu wa Tendaguru ambao umeanza kuharibiwa na wafugaji na majangili wa mbao.

Mwanamazingira na mkereketwa wa wanyamapori ambaye pia ni Mbunge kutoka Mkoa wa Lindi, Riziki Lulida (Mama Mjusi), amesema ni muhimu kwa serikali yetu ikaweka juhudi kubwa ya kuzungumza na Ujerumani ili mabaki haya yarudi Tanzania na kuyatengenezea makumbusho.

Amesema kama hilo haliwezekani, basi Ujerumani ikubali kutoa sehemu ya fedha ya mapato kutoka Naturkunde Museum kila mwaka kwa Serikali ya Tanzania na Mkoa wa Lindi ili zisaidie maendeleo na uhifadhi wa Pori la Tendaguru.

Mwandishi wa makala hii, Juma Salum, ni mwanachama wa Taasisi ya Waandishi Marafiki wa Mazingira na Wanyamapori (JFW – NH). Anapatikana kwa simu: 0657972723.