Na Daniel Limbe,Geita

“Samaki mkunje angali mbichi” ndivyo wasemavyo wahenga wakimaanisha mtoto mwema,mwenye hekima, busara na maarifa huandaliwa kingali mdogo.

Maneno hayo yanauweka bayana ukweli wa maisha ya mwanadamu katika malezi na makuzi ya mtoto hata anapokuwa mtu mzima.

Ukweli huo unaungwa mkono na kitabu kitakatifu cha Biblia katika Mithali 22:6 ambacho kinasema “Mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapo kuwa mzee”.

Kumbe tabia tulizonazo tukiwa watu wazima zinaakisi malezi na makuzi yetu ya utotoni, haijalishi ni tabia nzuri au mbaya.

Ndiyo maana upo msemo usemao” Huwezi kumnenepesha ng’ombe siku ya mnada” hakika uzuri wa kesho huandaliwa leo na nyota njema huonekana asubuhi.

Kwa lugha nyepesi ni kwamba matendo yasiyofaa kwa jamii ikiwemo ukatili,
mauaji,uchoyo,ufisadi,husuda,dhuruma na mengineyo mengi kwa kiwango kikubwa yanachangiwa na malezi na makuzi mabovu kutoka kwa wazazi au walezi.

Makala hii imejikita kuzungumzia tabia na mienendo mibovu itokanayo na malezi na makuzi yasiyofaa katika jamii,jinsi inavyosababisha madhara kwa jamii na taifa kwa ujumla.

WANANCHI WAELEZA MTAZAMO WAO

Siwema Samweli,mkazi wa Mkuyuni anasema mmomonyoko wa maadili katika jamii unachagizwa na baadhi ya wazazi kuwalea watoto wao kwa kuwadekeza kupita kiasi.

“Wazazi wengi wa sasa wanalea watoto wao kwa madeko makubwa wakiamini ndiyo malezi bora pasipo kutambua kuwa ndiyo wanawaharibia maisha yao ya baadaye”.

“Vilevile wapo wazazi na walezi ambao wanawanyanyasa na kuwatesa vibaya watoto kuliko kuwapatia upendo,faraja na amani,hali inayosababisha usugu na ukatili kwa watu wengine” anasema Siwema.

Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Walimu (CWT) wilayani Chato,Lucas Michael (Masai) anasema sheria ngeni za kuwalinda watoto zilizorithiwa na nchi yetu kutoka mataifa mengine pasipo kutazama mila na tamaduni zetu pia ni sababu ya kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili katika jamii.

“Ninaamini hatuwezi kuwa na malezi na makuzi mazuri iwapo tunaendelea na sheria za ovyo zilizopo,kwa sababu tulizipokea toka ng’ambo pasipo kuchuja mila na tamaduni zetu”anasema.

Anatoa mfano wa yeye alivyofikishwa kituo cha polisi baada ya kumwadhibu viboko mwanafunzi wake kwa lengo la kumuonya, na kwamba kutoka wakati huo hakutaka tena kusaidia malezi ya wanafunzi zaidi ya kuwafundisha masomo darasani.

“Nikiwa bado mwalimu wa sekondari(jina la shule na mwanafunzi tunavihifadhi) niliwahi kumwadhibu mwanafunzi wangu viboko nikiwa na lengo la kumwonya lakini ajabu nilishitakiwa polisi kuwa nimemtendea ukatili pasipo hata kuniuliza sababu za kutumia adhabu ya viboko, na kutoka kipindi hicho mpaka nilipostaafu sikutaka tena kuhangaika na malezi kwa wanafunzi wote.

Itambulike kuwa mwalimu ni Mzazi na mlezi, yapo makosa mengine tunatoa ushauri tu na inapotokea yanajirudia mara kwa mara bila mabadiliko yoyote tunalazimika kumwadhibu kwa fimbo.

“Kwahiyo nachoweza kusema uduni wa malezi kwa jamii yetu unasababishwa na sheria za ovyo ambazo zinamnyima mzazi haki ya kumwadhibu mtoto,ndiyo maana unaona mambo ya ajabu yanazidi kushamiri katika jamii ya sasa ukilinganisha na enzi wa Babu na Bibi zetu”anasema Mwl. Michael.

Zephania Malosha,kutoka taasisi ya “Uzao wetu” anasema tatizo la malezi na makuzi ya kitanzania lipo kwenye kupokezana kizazi kimoja kwenda kingine.

“Ukitaka kuelewa vizuri angalia ukoo wako,tazama Babu na Bibi zako walivyokuwa wakiwalea Baba au mama yako,kisha angalia Baba yako na Mama yako walivyokulea wewe,pia angalia malezi na makuzi ya wewe kwa watoto wako, utaliona hilo kwamba hakuna kizazi kinachoandaa kizazi kinachokuja mbeleni” anasema Malosha.

“Tumekuwa kama watoto wa Bata,ukizaliwa tu utajijua mwenyewe na hili linatokana na kinachoitwa maendeleo,ni muhimu tujue kuwa maendeleo ni mazuri lakini pia yanachangamoto zake mbaya kwa taifa letu”.

Askofu wa Kanisa la EAGT Jimbo la Chato,Kanda ya Geita, Mch. James Yugulwa, anasema wazazi wengi wapo katika majuto makubwa ya tabia za watoto wao na ukiangalia chimbuko ni msingi waliowawekea wao wenyewe toka wakiwa wadogo.

Anasema msingi ulio imara hujengwa katika neno la Mungu,mzazi ni lazima awe na juhudi kubwa ya kumlisha mtoto wake neno la Mungu tangu akiwa mdogo.

Mbali na hilo, anasema maendeleo ya mtoto yanahusiana na mtoto kuwa na kiwango kinachokidhi makuzi kimwili,kiakili,kiroho,kimaadili na kijamii.

“Ili mtoto aweze kukua vizuri anahitaji kutunzwa,kuongozwa na kulelewa katika misingi mizuri ya neno la Mungu”.anasema Askofu Yugulwa.

Mathalani, “Kuendelezwa kwa mtoto Kimwili ni kukua kimaumbile na uzito kwa uwiano wa mwili, aidha hali hiyo inategemea lishe na huduma bora za afya ikiwemo kupatiwa chanjo zote muhimu na upatikanaji wa viini lishe vyote muhimu”.

Kadhalika Maendeleo ya mtoto yanahitaji jitihada toka kwa wazazi,jamii na serikali kwa pamoja ikiwemo ulinzi dhidi ya unyanyasaji wa mtoto kama vile ubakaji, kukeketwa na kulazimishwa kuolewa au kuoa katika umri mdogo.

Ofisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Geita,Frenk Moshi,anasema mkoa huo tayari umezindua Programu ya malezi,makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto kwenye halmashauri sita za mkoa huo ili kuhakikisha elimu ya malezi bora inawafikia wananchi kwa karibu zaidi.

“Programu hiyo imeshaanza kwenye mkoa wetu na tumefanya uzinduzi kwenye halmashauri zote za mkoa wa Geita,ikiwemo halmashauri ya Geita mji,halmashauri ya wilaya ya Geita,Nyangh’wale,Mbogwe,Chato na Bukombe”.

“Kwa sasa mkoa wetu haujapata takwimu halisi za utekelezaji wa mpango huu, japo hivi karibuni tunatarajia kukutana na kupokea utekelezaji wa kila halmashauri,ispokuwa nachoweza kusema ni kwamba mkakati wetu ni kuhakikisha watoto wote wanapata huduma na malezi stahiki kutoka kwa serikali,jamii,wazazi na walezi”anasema Moshi.

Mbali na mkakati huo,kila halmashauri inaendelea na elimu kupitia makundi matano muhimu ikiwemo Afya,Ulinzi wa mama na moto,lishe,Malezi na ujifunzaji wa awali wa mtoto.

WASEMAVYO WASAIKOLOJIA TIBA

Mtaalamu wa saikolojia tiba,Deo Sukambi,akitoa mafunzo maalumu ya matunzo na malezi ya mtoto, anasema jamii kubwa haitambui tofauti ya malezi na matunzo,jambo linalodhoofisha kufikiwa kwa jitihada za maadili mema katika jamii.

“Usisahau unapolea mtoto wako jifunze kutofautisha matunzo na malezi, matunzo ni mtindo wa maisha unaompatia mtoto wako,shule unayompeleka,mavazi anayovaa,nyumba anayoishi, na chakula anachokula hayo siyo malezi bali ni matunzo, na kumpatia matunzo mazuri haimaanishi umemlea vizuri”.

“Malezi yanahusisha Mwongozo,maonyo,mafunzo,maelekezo, na kujibu maswali yake,uwepo wake kwenye maisha yake,kumhakikishia usalama wake na wakati mwingine kumpeleka kwenye mazingira ambayo anapaswa kujifunza namna gani anashiriki kwenye ulimwengu unaomzunguka”anasema Sukambi.

Anasema wazazi na walezi wengi ukisikia wanalalamika kuwa malezi ni magumu humaanisha gharama za matunzo ya mtoto, na siyo malezi.

Sukambi anaishauri jamii kutotumia gharama kubwa kusomesha watoto wao huku wakiacha nyuma suala la malezi bora jambo analodai ni hatari kubwa kwa mstakabali wa maisha ya baadaye.

“Sasa kipi bora wakati tukitumia muda mwingi kwenye haya matunzo,kilicho bora zaidi ni malezi na kama unaona kabisa Mungu hajakubariki kutoa matunzo mazuri usiweweseke,wala watoto hawahitaji chakula kizuri sana isipokuwa upendo tu wa Baba na mama”.

“Kwahiyo usijitese sana kutumia muda mwingi wa matunzo badala ya muda huo kuutumia katika malezi bora” anasema Sukambi.

Mwalimu George Sunzu(msaikolojia tiba) anasema baadhi ya watoto ambao hupitia malezi na makuzi mabovu,kwa kukosa ukaribu wa kihisia,kiwewe,na waliotelekezwa hupoteza uwezo wao wa huruma kwa watu wengine japo siyo wote.

Anasema kuwa maisha ya utotoni yanaunda tabia ya mwanadamu na kwamba ukatili hauzaliwi bali unatengenezwa.

Katika utafiti wa Daktari wa magonjwa ya akili nchini Uingereza,John Bowlby, ulioitwa “Maternal deprivation hypothesis” ulionyesha kuwa iwapo uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto utavunjwa,upo uwezekano mkubwa wa kuathirika maendeleo ya mtoto kihisia,kiakili na kisaikolojia.

Anasema ukosefu wa uhusiano mwema kati ya wazazi na mtoto ni zao la kile alichokiita kutokuwa na huruma kwa watu wengine(Affectionless psychopathy).

Aidha uwepo wa wauaji wa mfululizo,wahalifu,magaidi,jeuri na madikteta kuna uhusiano wa karibu wa tatizo la kiwewe, utakili, kutelekezwa, pamoja na kukosa ukaribu wa kihisia katika malezi na makuzi yao wakati wa utoto.

Wengine hukumbwa na tabia hizo kutokana na kufiwa na wazazi wao, ulevi wa kupindukia wa wazazi wao, uraibu wa dawa za kulevya pamoja na ugonjwa wa akili.

Utafiti mwingine uligundua kuwa aslimia 50 ya wauaji wa mfululizo walinyanyaswa kisaikolojia wakati wa utotoni, huku aslimia 36 ikionyesha walinyanyaswa kimwili na aslimia 26 walinyanyaswa kingono.

Katika historia ya wauaji wa mfululizo kama vile David Berkowitz, Ted Bundy na Joel Rifkin walikataliwa au kuachwa na mama zao.

Muuaji Edmund Kemper katika Malezi yake yeye aliteswa, na kunyanyaswa kisaikolojia na mama yake mzazi.

Vile vile muuaji wa kike Aileen Wuornos aliyeonyeshwa na Charlize Theron katika filamu ya Monster, aliachwa na mama yake akiwa na umri wa miaka minne tu na kulelewa na babu yake, ambaye alimnyanyasa kimwili na kingono.

Baba yake Adolf Hitler alikuwa mlevi na mwenye jeuri, huku mama yake akiwa amehuzunishwa na kupoteza watoto watatu wa awali hivyo hakuweza kumpa uangalizi na upendo.

Benito Mussolini na Francisco Franco walikuwa watoto wa baba walevi na wajeuri, ambapo wakingali na umri mdogo, Mussolini na Franco wote walionyesha uwepo wa dalili za ukatili wa kisaikolojia na kutojali kabisa hisia za wengine.

Kingali akiwa mdogo, Mussolini alikuwa jambazi mwenye jeuri ambaye alifukuzwa shuleni kwa kumchoma kisu mwanafunzi mwenzake.

Kadhalika Baba yake Saddam Hussein na kaka yake mkubwa wote walikufa muda mfupi kabla ya kuzaliwa kwake, na kumwacha mama yake akiwa na kiwewe kiasi kwamba alimkataa Saddam, kisha kuchukuliwa na mjomba wake.

Saddam Hussein akiwa mtoto pekee wa mama asiye na mwenza, alionewa kila mara na kupigwa akiwa mtoto na alijifunza jeuri ili kujitetea.

Itambulike wazi kuwa mtoto asipopewa malezi bora yenye huruma na mapenzi mema katika miaka yake ya mapema tangu kuzaliwa kwake, upo uwezekano mkubwa wa kuharibu uwezo wake wa huruma.

PROGRAMU YA MALEZI NA MAKUZI NCHINI

Tanzania inaendelea na utekelezaji wa Programu jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) huku jamii ikitakiwa kushirikiana katika mpango huo.

Mei 17,2024 Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu,Dkt. Dorothy Gwajima, akiwasilisha Bajeti ya makadilio ya mapato na matumizi ya Wizara yake Bungeni akasema kuwa migogoro ya ndoa katika jamii imekuwa ikichangia sana watoto kukosa malezi na makuzi jambo linalosababisha baadhi yao kukimbilia mitaani.

Kwamba hapa nchini kumekuwa na ongezeko la mashauri ya migogoro ya ndoa ambapo kufikia Aprili mwaka huu jumla ya mashauri 31,380 yalishughulikiwa ikilinganishwa na 28,773 yaliyoshughulikiwa kwa kipindi cha 2022/2023 ambalo ni ongezeko la mashauri 2,607 sawa na aslimia 8.3.

“Katika kipindi cha Julai 2023 hadi April mwaka huu,Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI tumewatambua watoto takribani 8,372 wanaoishi na kufanya kazi mbalimbali mtaani kutoka halmashauri zote nchini ukilinganisha na watoto 5,728 waliotambuliwa Julai 2022 hadi Aprili 2023” anasema Dkt. Gwajima.

Hata hivyo anasema utekelezaji wa Programu jumuishi ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto inafungua milango kwa sekta zote hapa nchini katika kumuandaa Mtanzania wa kesho na kwamba programu hii inakusudia kuona mtoto anaandaliwa vizuri.

“Ili MMMAM iweze kuwa na tija kwa taifa inahitaji kuwanufaisha watoto wote kwa usawa hasa wale wanaoishi na kufanya kazi mitaani,hii itawasaidia kuwarudisha kwenye mfumo rasmi ili waandaliwe kwa usalama wa taifa letu”.anasema Dkt.Gwajima.

Aidha Takwimu zinaonyesha kuwa vitendo vya ukatili vimepungua kutoka matukio 41,416 wanaume ikiwa ni 13,471 na wanawake 27,945 kwa kipindi cha mwaka 2017/18 hadi kufikia 29,373 wanaume wakiwa 8,476 na wanawake 20,897 mwaka 2021.

Kwa mujibu wa utafiti wa masuala ya Jinsia,Mila,Desturi,Tamaduni na sheria za Tanzania, (SIGI. 2022) inaonyesha kuwa aslimia 38 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukatili.

Aidha masuala yanayosababisha kuongezeka kwa ukatili ni pamoja na hofu ya kutengwa na jamii baada ya kutoa taarifa za ukatili,ucheleweshaji wa kesi mahakamani,uwepo wa mfumo dume na upatikanaji duni wa huduma za kijamii na afya kwa manusura wa ukatili.

Hata hivyo kupitia Dawati la Jinsia la polisi kwa wanawake na watoto, jitihada za makusudi zinaendelea kuonekana baada ya serikali kufuatilia na kudhibiti makosa ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji,ulawiti,kutupa watoto,ukeketaji pamoja na vipigo.

Machi 11, 2023 katika ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto kwa nchi za ukanda wa Afrika mashariki,
mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani(WHO) hapa nchini,Dkt. Charles Moses,akasema zaidi ya miaka 40 shirika hilo pamoja na washirika wengine wamekuwa wakihamasisha ajenda ya malezi kwa watoto.

“Lengo la maendeleo endelevu la 4.2 ni kuhakikisha wavulana na wasichana wote wanapata maendeleo bora ya utotoni(ECD) ifikapo mwaka 2030″anasema Moses.

Pia inakadiliwa kuwa zaidi ya watoto milioni 250 duniani kote hasa kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati wapo katika hatari ya kutofikia ukuaji wao kamili kutokana na sababu mbalimbali.

SHERIA YA MTOTO .

Kwa mujibu wa Ibara ya 13 kifungu cha kidogo(1) Mtu yeyote haruhusiwi kumtesa mtoto au kumfanyia vitendo vingine vya ukatili,kumpa adhabu za kinyama au kumdhalilisha ikiwa ni pamoja na kumfanyia mambo ya kimila yanayoondoa utu wake au yenye madhara katika ustawi wake kimwili au kiakili.

Kifungu kidogo cha (2) Hakuna adhabu kwa mtoto itakayokubalika kama adhabu hiyo ni ya kupindukia kwa namna na jinsi ilivyotolewa kwa kuzingatia umri,hali yake ya kimwili na kiakili na, hakuna adhabu itakayokubalika kama mtoto huyo kwa sababu ya umri wake mdogo au vinginevyo hawezi kuelewa lengo la adhabu hiyo.

Aidha Ibara ya 14 inatamka kuwa “Mtu yeyote atakayekiuka kifungu chochote katika sehemu hii atakuwa ametenda kosa la jinai na mahakama ikimwona kuwa ana hatia, atalipa faini isiyozidi shilingi milioni 5 au kwenda jela kwa kipindi kisichozidi miezi sita au kutumikia adhabu zote mbili kwa pamoja.

NINI KIFANYIKE?

Baadhi ya wananchi wanapendekeza jamii kurejea upya kwenye malezi na makuzi ya zamani ikiwa ni pamoja na kuwafundisha watoto michezo na nyimbo za asili ili kulinda na kuenzi tamaduni za kitanzania.

Jamii ielimishwe madhara ya ndoa na mimba za utotoni ambazo zimekuwa zikichangia watoto kutupwa mitaani kutokana na wazazi kushindwa kumudu gharama za matunzo ya mtoto.

Viongozi wa dini watimize wajibu wao kwa kuwafundisha watoto njia ziwapasayo kuenenda katika maonyo na maelekezo ya Mwenyezi Mungu ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu Baba,Mama na watu wengine.

Halmashauri kupitia idara zake za Ustawi na Maendeleo ya Jamii wayafikie makundi yaliyoko chini na kuwaelimisha namna bora ya malezi na makuzi ya watoto badala ya kuwaacha na kukua wapendavyo.

Vituo vya malezi na makuzi ya watoto wapewe ruzuku na serikali ili waweze kuwahudumia kikamilifu watoto wote walio katika hatari ya kukimbilia mitaani.

Serikali itenge fedha za kutosha kuwawezesha wasaikolojia tiba na madaktari wa afya ya akili kwenda kwenye vituo vya malezi,shule za msingi na sekondari kwaajili ya kutoa elimu na msaada wa tiba kwa watoto watakaotambuliwa.

Serikali iajiri walimu wa saikolojia na ushauri nasaha ( psychology, guidance & counselling teachers) kwa shule zote za msingi na sekondari kwa sababu ndipo lilipo kundi kubwa la watoto na vijana ikizingatiwa kundi hilo hutumia muda mwingi wakiwa shuleni kuliko nyumbani.

                  
Please follow and like us:
Pin Share