Malawi imetangaza siku 21 za maombolezo kufuatia kifo cha Makamu wa Rais wa nchi hiyo Saulos Chilima na watu wengine nane kilichosababishwa na ajali ya ndege.
Siku ya Jumatatu, Chilima na ujumbe wake walikuwa safarini kuelekea kaskazini mwa nchi hiyo kabla ndege ya kijeshi waliyoabiri kupoteza mawasiliano na rada kutokana na hali mbaya ya hewa.
Mabaki ya ndege hiyo yalipatikana siku ya Jumanne, ndani ya msitu mnene na wenye vilima vikali karibu na mji wa Mzuzu.
Kipindi cha maombolezo kinaanza Juni 11 mpaka Julai 1, Baraza la Mawaziri la nchi hiyo limesema katika taarifa yake ya Jumanne.
Bendera kupepea nusu mlingoti
Rais Lazarus Chakwera ameelekeza bendera zote kupepea nusu mlingoti wakati wote wa maombolezo, iliongeza taarifa hiyo.
Kulingana na baraza hilo, taratibu za mazishi zitatangazwa hapo baadaye.
Mabaki ya miili ya Chilima na waathirika wengine ilisafirishwa kwa ndege kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo, Lilongwe.
Rais Chakwera aliambatana na viongozi wengine wa serikali kuipokea miili hiyo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kamuzu, jumanne jioni.
Baadhi ya viongozi mbalimbali ulimwenguni wameendelea kutuma salamu zao za rambirambi kwa familia na serikali ya Malawi.