Kasulu, Kigoma
MAAMBUKIZI ya viashiria vya ugonjwa wa Malaria Nchini Tanzania yame pungua kwa Watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015 na kufikia asilimia 7.3 kwa Mwaka 2017 hii ni kuzigatia harakati zinazo fanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Mashirika ya Marekani (USAID) pamoja na shirika la WHO kuhakikisha wanautokomeza ugonjwa huo.
Akizindua takwimu zilizo tolewa na Ofisi ya Takwimu ya Tanzania leo Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma Waziri wa Afya Maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Ummy Mwalimu , alisema Siku ya leo kupitia maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa Kigoma, atazindua rasmi Matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria kwa Mwaka 2017.
Kwa Mujibu wa Mkurugenzi mkuu ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Albina Chuwa alithibitisha Matokeo ya sasa ya utafiti huu, yanaonesha kuwa kiwango cha malaria kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini Tanzania kimeshuka kwa Zaidi ya nusu kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3. Hii ni kwa kutumia kipimo cha haraka cha utambuzi wa vimelea (mRDT).
Waziri Ummy alisema utafiti huo unaonesha Mikoa yenye kiwango kikubwa cha watoto wenye malaria ni, Kigoma (asilimia 24.4), Geita (asilimia 17.3), Kagera (asilimia 15.4) na Tabora (asilimia 14.8) ambapo Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Njombe, Songwe na Dodoma ina kiwango kidogo cha maambukizi chini ya asilimia moja.
“Takwimu hizi, zinaonesha kupungua kwa kiwango cha malaria kwa kiasi kikubwa, na hii ni habari njema kwetu sote na inaonesha ni jinsi gani Serikali yenu ipo tayari kutoa kipaumbele katika kuhakikisha kuwa malaria inadhibitiwa na hatimae tuweze kuitokomezwa kabisa Ili kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa, tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja katika kufikia malengo tuliyojiwekea ili jamii, hasa watoto chini ya umri wa miaka mitano na wanawake wajawazito ambao ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa wa malaria waweze kuepukana na ugonjwa huu”, alisema Waziri Mwalimu.
Alisema Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana, lakini bado kuna changamoto, ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi ili kwa pamoja tuweze kufikia malengo ya kutokomeza malaria nchini.
Changamoto hizo ni pamoja na Wanajamii kutotumia vyandarua ipasavyo katika kujikinga na ugonjwa wa malaria, kuwepo kwa mitazamo potofu juu afua za kupambana na malaria; mfano dhana ya kuwa viuatilifu-ukoko za kunyunyizia ukutani zinaleta kunguni na viroboto na kuwa vyandarua vinapunguza nguvu za kiume ni dhana potofu ambazo hazina ukweli wowote. Vilevile, Jamii kutoshiriki kikamilifu katika kutunza mazingira na kuharibu mazaliaya Mbu.
Kwa upande wake Mkurugenzi mwakilishi wa shirika la misaada na Maendeleo la Marekani USAID Andy Karas alisema kwa zaidi ya miaka 12 USAID imekuwa ikifanya kazi pamoja na serikali kupitia Wizara ya Afya kwaajili ya Kupambana na Malaria.
Alisema watoto wengi walio hai leo ni kwa juhudi za serikali, kwa kushirikiana na Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria kwa Muda wote wameweza kusambaza vyandarua zaidi ya milioni 10 na kununua viuwadudu zaidi ya milioni 20 na kupuliza dawa ya Mbu kwenye maeneo hatarishi vile vile wameweza kushirikiana na ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kufanya takwimu mbalimbali juu ya kupungua kwa ugonjwa wa Malaria.
Nae Balozi wa Usizwi Florence Tinguell aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kwa juhudi kubwa walizo zifanya katika kuhakikisha wanatokomeza Malaria ,imeweza kubuni mbinu. Kwa zaidi ya miaka 50 Ubalozi wa Uswizi umekuwa ukifadhili tafiti za malaria ambazo zimekuwa zikifanywa na taasisi ya Ifakara Health Institute.
Hata hivyo mjumbe wa kamati ya bunge ya kupambana na Malaria ( TAPAMA) na Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Iringa Rose Tweve alisema wao kama wabunge wanatoa wito kwa Wananchi wote kuwa jukumu la kupambana na Malaria na mapambano dhidi ya Malaria ni la Wananchi na wasiiachie serikali peke yake na kuomba nguvu kubwa ielekezwe kwenye kinga na wahudumu wa Afya na wakina mama kufika hospitali kwa wakati ilikuweza kupatiwa kinga ya Malaria.