KATIBU wa Halmashauri Kuu(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi, Uenezi,Siasa na Mafunzo CPA Amoss Makala amewahakikishia Watanzania kuwa wagombea wanaotokana na Chama hicho katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni wagombea wenye sifa na wako tayari kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo.

Amesisitiza kuwa wagombea wa CCM wamepatikana kwa utaratibu unaoeleweka na wamekabidhiwa tamko la Chama ambalo linaeleza kwa kina maelekezo ya wanayotokakiwa kuyatekeleza kwa ajili ya wananchi wakati wagombea wa vyama vingine wameokotwa okotwa tu.

Katibu wa Halmashauri Kuu(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi, Uenezi,Siasa na Mafunzo CPA Amoss Makala, Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Vijibweni wilayani Kigamboni Mkoani Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya mkutano wa kampeni za uchaguzi. (Picha na Fahadi CCM )

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Vijibweni wilayani Kigamboni Mkoani Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya mkutano wa kampeni za uchaguzi huo CPA Makala amesema uchaguzi huo ni muhimu na ndio maana CCM imeamua kuweka wagombea wenye sifa kwa ajili ya kuwatumia wananchi .

“Naomba niwahakikishie Watanzania kwamba Chama Cha Mapinduzi kimeleta wagombea safi ambao wako tayari kuwatumikia katika kuleta maendeleo.Mchakato wa kupata wagombea wa CCM wamepatikana katika utaratibu wa demokrasia na ukweli wagombea hao wanayo dhamana ya kuhakikisha wanakwenda kushirikiana na madiwani,Wabunge na Rais katika kuleta maendeleo,”alisema CPA Makala.

Aliongeza kuwa CCM wagombea wake wameandaliwa na Wana sifa za kutosha za kuwatumikia wananchi wakati wagombea wa CHADEMA hata utaratibu wa kupata wagombea wake haueleweki kwani wanapena tu.”Utasikia wanapambana Kamanda chukua Mtaa huo..Kwa CCM wagombea wetu wanapatikana kwa utaratibu mzuri kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.”

Akizungumza zaidi mbele ya mamia ya wananchi wa Wilaya ya Kigamboni,CPA Makala alisema baada ya Chama hicho kuzindua kampeni zake rasmi jana nchini kote tayari wapinzani wameingia ubaridi maana wanaona tayari wameshandindwa huku akisisitiza CCM inatofautiana na vyama vingine vya siasa na kufafanua Chama hicho ndicho kina Ilani ya Uchaguzi Mkuu inayotekelezeka na wengine hawana.

Hata hivyo alisisitiza ni muhimu wananchi kuchagua wagombea wa CCM kwasababu Chama hicho ndio kinatekeleza Ilani ya Uchaguzi mkuu 2020-2025 ,hivyo wagombea wa CCM wakishinda wataungana na madiwani , Wabunge na Rais katika kufanikisha utekelezaji wa Ilani.

Pia amesema CCM ndio Chama chenye dhamana ya kuwatumikia Watanzania nchi nzima na kwamba vyama vingine hawana wajibu huo na kazi yao ni kufanya maandamano.