Rasimu ya Katiba Mpya imeyanyong’onyeza makundi ya wanaowania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa muda mrefu kumekuwapo mjadala mkali wa nani anayestahili kuwania kiti hicho, lakini mbio hizo zimepunguzwa kasi na umaarufu wake, baada ya rasimu kupendekeza kuwapo kwa muundo wa Serikali Tatu – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Tanzania Bara (Tanganyika).

Habari kutoka ndani ya makundi hasimu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako ndiko kwenye msuguano mkali, zinasema wenye nia, pamoja na wapambe wao sasa wanakuna vichwa wakitafakari wajielekeze wapi kwenye kuwania urais.

 

Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaonekana bado kuwa na nguvu zinazotokana na ukweli kwamba rais huyo atakuwa kiongozi mkuu wa nchi, lakini ambaye kwa kimombo ni “ceremonial”. Endapo kilicho kwenye rasimu kitapita na kuwa Katiba, rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mambo makuu saba pekee kwenye Shirikisho.

 

Nafasi hiyo bado inaonekana kuwa na heshima, ingawa kwa utendaji kazi wa kila siku, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatakuwa na sauti ya moja kwa moja ya kuakisi mambo mazito ya upande wa Tanzania Bara.

 

Kwa kulitambua hilo, nguvu za kambi kadhaa za urais zimeelekezwa kwenye urais wa Tanzania Bara. Rais wa upande huo, licha ya kuwa hana nguvu kama Amiri Jeshi Mkuu, bado nguvu zake za kiuchumi zinaweza kumfanya akawa na sauti zaidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano.

 

Pengine ni kwa sababu hiyo, baadhi ya wananchi wanaotoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari, wanasema nguvu na uhalali wa rais wa Jamhuri ya Muungano, pamoja na ukweli kwamba zitakuwa zimeainishwa ndani ya Katiba ya Shirikisho, zitategemea zaidi busara, weledi na pengine ‘hisani’ kutoka kwa rais wa Tanzania Bara.

 

Kwa maneno mengine, baadhi ya wachangiaji wanasema uhai au kifo cha Muungano vinategemeana na msimamo na ushawishi wa rais wa Tanzania Bara, hasa ikizingatiwa kwamba ndiye mwenye nchi ‘tajiri’.

 

Hapatarajiwi kuwapo mvutano mkubwa Zanzibar kutokana na ukweli kwamba tayari kwa upande wao wameshajiwekea Katiba ambayo kimsingi itahitaji mabadiliko ya hapa na pale ili iendane na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Rasimu iliyozinduliwa wiki iliyopita chini ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, imezidi kuvunja nguvu za makundi baada ya kuwapo mapendekezo ya kipengele kinachoruhusu wagombea binafsi.

 

Wengi wanaona sasa hakuna sababu ya kugombana kwa sababu kama atakuwapo mwanachama wa chama chochote cha siasa anayeutaka urais kwa udi na uvumba, endapo jina lake litakatwa anaweza kusimama kama mgombea binafsi.

 

Kwa sababu hiyo, inatarajiwa kuwa mvurugano, vijembe, kashfa, matusi na makundi ni mambo yanayotarajiwa, ama kupotea, au kupungua kwa kiwango cha kustaajabisha wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.