2110Makontena 1,762 na magari 919 yametolewa katika Bandari Kavu jijini Dar es Salaam bila kulipiwa ushuru na kodi mbalimbali, JAMHURI limebaini.

Pamoja na upotevu huo, Serikali imepata hasara ya Sh milioni 914.136 ambazo hazikulipwa na meli za mafuta kwa miezi mitatu ya Septemba hadi Novemba, mwaka jana.

Ripoti ya Ukaguzi wa Ndani ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), inaonyesha kuwa magari hayo yametoweka katika Maghala ya Ushuru wa Forodha (CFS) yanayomilikiwa na kampuni za TALL, MASS, HESU na SILVER.

Mchanganuo wa upotevu huo na idadi ya magari kwenye mabano ni: TALL (347), MASS (184), HESU (328) na SILVER (60).

Makontena 1,762 yametoweka katika Bandari Kavu (ICD) za PMM (makontena 66), Azam (makontena 37), AMI (makontena 177), TRH (makontena 568), Al Lhushoom (makontena 19), DICD (makontena 161) na JEFAG makontena 734.

Meneja wa Ukaguzi wa Ndani wa TPA, A. Makoko, amebainisha baadhi ya sababu za ‘kupotea’ kwa makontena hayo, na kutoa mapendekezo kadhaa.

Miongoni mwa dosari hizo ni matumizi hafifu ya mfumo wa Teknolojia ya Mawasiliano katika kukusanya  mapato kwenye CFS na ICD.

Anasema udhaifu huo umesababishwa na baadhi ya watumishi kutokuwa na ujuzi wa matumizi ya kompyuta. Baadhi ya CFS na ICD hazina huduma za mtandao wa mawasiliano ya intaneti; na baadhi ya watumishi katika CFS na ICD hawana uwezekano wa kutumia mifumo ya Tancis na malipo kwa njia ya kiektroniki.

Kwenye mchanganuo wa fedha zilizopaswa kulipwa na meli, ripoti inaonyesha kuwa kiasi kilichoishia kwa ‘wanjanja’ Septemba mwaka jana ni Sh 484,010,868.86. Oktoba, fedha zilizopotea ni Sh 252,528,562.59; na Novemba kiasi kilichopotea ni Sh 117,597,143.22.

Kuhusu upotevu wa makontena na magari, uchunguzi imeonyesha kuwa kwa kipindi hicho hapakuwapo watumishi wa TPA katika malango yote ya ICD ambao wangepaswa kuhakiki nyaraka za shehena; na malipo ya tozo ya kuhifadhi mizigo.

 

Moto wa Serikali ya Awamu ya Nne

Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka kwa kushindwa kusimamia TPA na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Pamoja na Mwinjaka, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi Massawe. Pia alivunja Bodi ya Wakurugenzi ya TPA na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TPA Profesa Joseph Msambichaka.

Wajumbe wa Bodi walikuwa ni Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Haruna Masebu, Dk. Francis Michael, Mhandisi Gema Modu, Mhandisi Musa Ally, Nyamsingwa, Crescentius Magori, Flavian Kinunda na Donata Mugassa.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali haitavumilia kuona watu au kikundi chochote kilichojipanga kuhujumu mifumo au kuiba mapato ya Serikali.

“Ukaguzi wa ndani uliofanywa Julai 30, mwaka huu uligundua kuwapo kwa mianya mingi ya ukwepaji kodi yakiwamo makontena 2,387 yaliyopitishwa kati ya Machi na Septemba mwaka jana kinyume cha taratibu,” alisema.

Majaliwa akifanya ziara ya kushitukiza bandarini Dar es Salaam Novemba 27, mwaka huu. Alifichua mwanya wa ukwepaji kodi kwa makontena 329 yenye thamani ya mabilioni ya shilingi. Mara moja, aliwasimamisha kazi baadhi ya maofisa wa TRA; na muda mfupi baadaye Rais John Magufuli, akamsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade.

Watumishi watatu aliwahamisha kituo cha kazi, lakini siku iliyofuata nao walijumuishwa na wenzao sita na kutakiwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya uchunguzi.

Majaliwa alirejea Bandari Desemba 4 kufuatilia hatua za kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali kabla hajagundua makontena 2, 431 yaliyopita bila kulipiwa ushuru.

TRA iliwachukulia hatua watumishi 35 wa ngazi mbalimbali na kuwasimamisha kazi wengine wakiwamo 27 waliokamatwa gati namba 5 ambao wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano.

Kampuni na watu 43 waliohusika kwenye uingizaji wa makontena 329 ambayo yaliondolewa katika bandari kavu kinyume na taratibu, zilitangazwa.

Waliosimamishwa kutoka idara ya usimamizi wa ICD ni Happygod Naftari, Juma Zaar, Mkango Alli na Steven Mtui. Wengine ni Titi Ligalwike, Lyidia Kimaro, John Elisante na James Kimwomwa aliyehamishiwa Mwanza ambaye atalazimika kutekeleza agizo hilo akiwa huko.

Kwa upande wa viongozi waliotoa ruhusa kwa makontena hayo kuondoshwa bandarini nao wamesimamishwa. Hao ni aliyekuwa Meneja Mapato ambaye amehamishiwa Kitengo cha Fedha cha Makao Makuu, Shaaban Mngazija, aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandarikavu ambaye pia amehamishiwa Makao Makao Makuu kwa Naibu Mkurugenzi Huduma za Biashara, Rajab Mdoe.

 Wengine ni Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Ibin Masoud na Meneja Bandari Msaidizi Fedha, Apolonia Mosha.

Waziri Mkuu alisema Dk. Mwinjaka amewajibishwa kutokana na kushindwa kuzisimamia mamlaka mbili, TRL na TPA ambazo zipo chini ya wizara yake.

“Serikali ilitoa Sh bilioni 13 na TRL wenyewe wakakopa Sh bilioni 3 kutoka Benki ya TIB kwa ajili ya miradi, lakini fedha hizo hazikutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuisababishia serikali hasara. Rais ameagiza apishe uchunguzi wakati akisubiri kupangiwa majukumu mengine kama hatakutwa na hatia yoyote,” alisema Majaliwa.

 

Ufisadi TRL

 Februari 2013, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe alizundua Bodi ya Wakurugenzi na kuwataka kuhakikisha wanasaidia kuimarisha TRL ili mizigo mingi inayokwenda mikoani na nje ya nchi isafirishwe kwa njia ya reli kuokoa ubora wa barabara na kupunguza gharama za kuzikarabati.

Machi 2013, TRL ilisaini mkataba wa kununua mabehewa 25 aina ya Ballistic Hopper Bogie ya kubebea kokoto na kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries ya India. Mkataba huo ulikuwa na thamani ya Sh 4 bilioni.

Aprili 2013, TRL iliipatia mkataba mwingine kampuni hiyo ya India  wa kutengeneza mabehewa mengine 274 ya mizigo na Serikali ikalipa Sh 166 milioni kwa kila behewa.

Julai 2014, mabehewa hayo yaliingia nchini ila muda mfupi baada ya kuanza kutumika yaligunduliwa kuwa hayakuwa na viwango vilivyokusudiwa.

Desemba 2014, mabehewa 20 kati ya 25 yaliyoingia yaligundulika kuwa yanamong’onyoka, hivyo kumlazimu waziri huyo kuunda kamati ya uchunguzi dhidi ya watendaji waliokwenda India kuyakagua.

Mwezi huo,  pia Dk Mwakyembe aliwatimua kazi watumishi sita wa TRL kutokana na tuhuma za wizi na kuliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi.