Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA

Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo ameongoza timu ya wataalam kutoka taasisi mbalimbali wanaoshiriki katika kampeni ya utoaji wa msaada na huduma za kisheria inayoitwa Mama Samia Legal Aid Campaign iliyotembelea maeneo ya vizuizi katika Wilaya za Kondoa na Chemba jana Tarehe 09/05/2023.

Akiambatana na wataalam kutoka Ofisi ya Mashtaka, Tume ya Haki za Binadamu, Dawati la jinsia la Polisi, Wanasheria na watumishi wengine kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Katibu Mkuu huyo alifika katika gereza la Kondoa na kufanikiwa kuongea na uongozi lakini pia na wafungwa na mahabusu waliokuwepo katika gereza hilo lengo likiwa ni kubaini changamoto za kisheria zikiwemo upatikanaji wa dhamana kwa wafungwa wanaostahili pamoja na namna kesi zao zinavyoendeshwa.

Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo akiwasili katika Gereza la Kondoa akiwa ameambatana na wataalamu wa Mama Samia Legal Aid Campaign kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa watu walio vizuizini.

Akitoa taarifa za ukaribisho kwa Katibu Mkuu na timu yake, Kaimu Mkuu wa Gereza la Kondoa SP Amry Ally Kibwana alisema moja ya changamoto waliyonayo ni wingi wa wafungwa na mahabusu walionao ambao unazidi uwezo wa Gereza hilo pamoja na changamoto ya usafiri wakati wa kuwapeleka mahabusu mahakamani.

Aidha wingi wa wafungwa katika gereza la Kondoa unachangiwa na kutokuwepo kwa Gereza katika Wilaya ya Chemba. Wafungwa ambao kesi zao zinasikilizwa Mahakama ya Chemba ambao wapo katika gereza la Kondoa hulazimika kupelekwa mahakamani mara mbili tu kwa wiki badala ya kila siku hali inayopelekea kucheleweshwa kwa kesi na mahabusu kukaa muda mrefu kizuizini.

Timu hiyo ya Mama Samia Legal Aid Campaign baada ya kuongea na uongozi wa Gereza iliingia ndani ya gereza na kuongea na mahabusu pamoja na wafungwa ambapo elimu ya sheria ilitolewa ikiwemo jinsi mtu anavyokamatwa kituoni mpaka anapelekwa gerezani vitu vinavyotakiwa kufuatwa, Lakini pia mtaalam kutoka haki za binadamu alielezea haki za msingi za wafungwa wakiwemo gerezani ikiwemo haki ya dhamana kwa makosa yenye dhamana na pia afisa kutoka Ofisi ya Mashtaka alifafanua namna kesi za watu walio vizuizini zinavyotakiwa kushughulikiwa na afisa mashtaka wa wilaya.


Kaimu Mkuu wa Gereza la Kondoa SP Amry Ally Kibwana akimkaribisha na kutoa taarifa ya awali kwa Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo na timu yake walipofika katika Grereza hilo Kwa lengo la kutoa Msaada wa Kisheria.

Aidha, Katibu Mkuu Makondo akatumia nafasi hiyo kuwaelezea Mama Samia Legal Aid Campaign na malengo mahsusi ya kampeni hii ya miaka mitatu kuwa ni kila mtanzania aliyepo nchini Tanzania Bara na Zanzibar kufikiwa na huduma hii ya msaada wa kisheria bila kujali mahali alipo lengo likiwa ni kuwezesha hata wale wasio na kipato waweze kupata haki wakiwemo walio vizuizini. 

Mahabusu na wafungwa pia walipewa nafasi ya kuuliza maswali baada ya elimu iliyotolewa huku wakitaja baadhi ya changamoto ambazo ni pamoja uchelewashwaji wa kesi hasa katika Mahakama ya Chemba ambapo Katibu Mkuu aliwaahidi kulishughulikia suala hilo lakini akawataka wale wote ambao wana makosa ambayo wanaweza kupata dhamana kujiorodhesha kwa Mkuu wa Gereza huku akiwaagiza watendaji kuhakikisha wanapatiwa dhamana kwa wakati.

Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya ya Chemba bwana Gelard Lomward Mongela (Kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Khamis Mkanachi (kushoto)



Pamoja na elimu na Msaada huo, Bi. Makondo alikabidhi msaada wa vifaa vya matumizi kwa ajili ya wafungwa ambavyo ni pamoja na sabuni, mafuta ya kupaka, dawa za meno, miswaki, mashine za ndevu pamoja na taulo za kike na vifaa vingine vya akina mama ikiwa ni sehemu ya mchango wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa watu hao walio Vizuizini.

Katika Kampeni hiyo Katibu Mkuu alikutana na Wakuu wa Wilaya za Chemba na Kondoa katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Chemba ambapo kwa pamoja walimshukuru Bi. Makondo kwa kuwa sehemu ya uendeshaji wa kampeni hiyo katika wilaya zao na wakimuahidi kutekeleza yale yote atakayoyaelekeza na kwamba wapo tayari kuunga mkono Mama Samia Legal Aid Campaign.