Taasisi na watu binafsi wameendelea kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwasaidia watoto wenye matatizo ya ugonjwa wa moyo.

Wiki iliyopita Ubalozi wa nchi za Falme za Kiarabu (UAE) ulitoa Sh milioni 27 ambazo zitatumika kuwakatia bima ya afya watoto 500 wanaosumbuliwa na tatizo la moyo.

Akizungumza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kupokea hundi ya fedha hizo, Makonda aliwataka watu na taasisi nyingine zenye uwezo kuwasaidia watoto hao wahitaji.

Ameushukuru ubalozi huo kwa kuwasaidia watoto hao na kubainisha kuwa iwapo Watanzania wataamua, wana uwezo wa kutatua matatizo mengi katika jamii kupitia michango.

“Fedha hizi zitasaidia kuwakatia bima za afya watoto 500 ambao ka sasa wamelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Bima watakazokatiwa zitawahakikishia kupata matibabu bila shida,” amesema Makonda.

Amesema bima hizo zitazipunguzia mizigo familia za watoto hao, kwani zitawawezesha kupata matibabu si ya moyo tu, bali hata maradhi mengine yatakayowakabili.

Amesema watoto wengi kati ya hao waliopatiwa msaada huo wanatokea katika familia maskini.

Amemshukuru Balozi Khalifa Abdulrahman Almarzooqi kwa kuendelea kumuunga mkono katika suala hilo, kwani hapo awali ubalozi huo ulisaidia gharama za masomo kwa wasichana 100 wa kidato cha tano na sita, kuleta madaktari bingwa 10 ambao wamesaidia kuwafanyia upasuaji watoto 60 wenye tatizo la moyo, kusaidia futari kwa maimamu wa misikiti 800 na kutoa wito kwa watu wengine kuwa na moyo wa kujitolea kama balozi huyo.

Kwa upande wa Balozi Almarzooqi, ameonyesha kufurahishwa kwake na utendaji kazi mzuri wa Makonda katika kuwasaidia wananchi wenye mahitaji na hilo ni jambo lililousukuma ubalozi huo kumuunga mkono na kushirikiana naye.

Amesema ni jambo la kuleta faraja kuwa kila msaada ambao wanautoa kupitia kwa mkuu huyo wa mkoa unawafikia walengwa bila shida.

Makonda amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuwasaidia watoto hao, kwani wapo ambao wamo katika hali mbaya na jitihada zinatakiwa kuokoa maisha yao.