Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewaomba viongozi wa dini kuhubiri amani na utulivu ikiwemo wanasiasa kufanya kampeni za kistaarabu tunapoelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotaraji kufanyika Novemba 27 mwaka huu nchi mzima.

Aidha amewaomba viongozi wa dini kuunda kamati maalum kwaajili ya kujiandaa siku ya Uhuru Desemba 9 ,mwaka huu kwa kuadhimishwa kwa maombi maalum ya kuliombea Taifa , familia,biashara,watoto kwakubeba bendera 100,000 ndogo na bendera kubwa 10000.

Makonda ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati alipokutana na viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini ,wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa wa Arusha kwa ajili ya kutafakari mambo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha.

Ameaema uchaguzi huo unalenga kupata viongozi bora na kusisitiza kuwa watu washindane kwa hoja na sera na si matusi badala yake washindane kwa kuongelea changamoto za kwenye mitaa na kuziainisha ili kusaidia serikali kuzitatua.

“Nawaomba viongozi wa dini tuhubiri amani na utulivu uliopo nchini, wanasiasa wafanye kampeni za kistaarabu na pia lazima tujue Arusha ni Mkoa wa pekee wenye kubeba hadhi ya utalii hivyo tushikamane katika kuhakikikisha tunafanya kampeni za kistaarabu na tuhamasishe waumini wetu kuchagua viongozi bora wanaowataka wao”