Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amebaini upotevu wa fedha zaidi ya Sh bilioni 1. 3 katika shule ya Sekondari ya Wasichana Longido iliyopo wilayani Longido.

Fedha hizo zimepotea kutokana na ulipaji wa malipo bila kutoa risiti za mashine za kieletroniki, malipo holela ya wazabuni katika ujenzi wa shule hiyo kupitia ripoti ya awali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Makonda ameyasema hayo leo wilayani humo wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi wa shule hiyo iliyofanywa na Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa mara baada ya kutembelea shule hiyo na kubaini kutokamilika kwa bwalo la chakula pamoja na baadhi ya madarasa ya wanafunzi.

Makonda amesema katika ripoti hiyo ya Takukuru kwa mujibu wa taarifa za awali alizopitia alibaini upotevu wa fedha hizo ziliolipwa kiholela na pindi atakapokamilika kupitia taarifa yote ataiwasilisha kwa Waziri Mchengerwa kwa hatua stahiki zinazofuata.

“Nilipofika hapa shuleni nilihoji taarifa za Ujenzi wa shule hizi lakini ikanilazimu kuagiza Takukuru kuchunguza mradi huu na hayo ndio niliyobaini kwa mujibu wa taarifa za awali ambapo zaidi ya sh,milioni 300 zimelipwa lakini hazina nyaraka za kuonyesha zimelipwa lipwaje au zimeenda kwa nani lakini pia ripoti hiyo imebaini zaidi ya asilimia 71 ya fedha iliyotolewa kwaajali ya wazabuni imeongezwa kinyume na taratibu”

Amesema Sh bilioni 1 zilitumika pasipo kupitia mfumo wa kieletroniki wa EFDs lakini pia zaidi ya Sh milioni 300 zililipwa bila kuwa na nyaraka za udhibitisho wa kuonyesha zimelipwaje na zinaenda lwa nani ikiwemo ongezeko la asilimia 71 ya fedha iliyotolewa kulipwa wazabuni kulipwa kinyume na taratibu.