Na Zulfa Mfinanga, Jamhuri Media, Arusha
Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda ameadhimisha siku ya Uhuru wa Tanganyika kwa kufanya matembezi ya maombi ya kuuombea mkoa huo pamoja na Taifa la Tanzania.
Akizungumza na mamia ya watu walihudhuria matembezi hayo ya maombi, Makonda amesema kupitia maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanganyika ameamua iwe siku ya kufanya matembezi ya maombi kwa kushirikisha madhehebu yote ya dini ndani ya mkoa wa Arusha.
Akiongoza matembezi hayo pamoja na viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini, Makonda amewataka wananchi wote walioshiriki kutumia mafundisho waliyotapata kutoka katika nyumba zao za ibada kuliombea Taifa, mkoa wa Arusha pamoja na familia zao.
“Leo tumeamua kuandika historia, hii siyo siku ya burudani, naomba kila mmoja wetu hapa atumie kila hatua yake kuomba ukombozi wetu, na tumuombe Mwenyezi Mungu aangalie nyoyo zetu za unyenyekevu kwake” amesema Makonda
Akiwa katika eneo mzunguko wa mnara wa saa eneo ambalo ni katikati ya bara la Afrika amesema kupitia eneo hilo lililobeba historia ya bara la Afrika wanaweka maombi yao hapo kwa ajili ya kuoanisha uhuru wa Tanganyika ili kuendelea kuwepo nchini na ndani ya familia za kila mwana Arusha.
Makonda amewataka wakazi wa mkoa huo kuzingatia maombi kila wakati kwani utukufu wa Mungu ukiwepo ndani ya familia zao utasaidia kuondoa maradhi, umasikini na shida mbalimbali.
Kwa upande wao viongozi wa dini Shekh wa mkoa wa Arusha Shaban Juma na Askofu Dkt. Israel Maasa wamewata wananchi wa mkoa wa Arusha kuendelea kuliombea Taifa, kumuombea Rais Dkt. Samia, mkoa wa Arusha pamoja familia zao na kuendelea kuishi kwa amani.
Baadhi ya wahudhuriaji waliozungumza na Jamhuri wameshukuru kuwepo kwa maombi hayo na kusema yataondoa changamoto mbalimbali zinazoukabili mkoa huo na kuomba yafanyike kila mara na kila mwaka katika maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika.
“Nina amini maombi haya yataenda kuinua uchumi wetu kupitia kazi na biashara tunazofanya, yataondoa ajali, maradhi na hata kuinua watoto wetu mashuleni” alisema Rose Julius mkazi wa Ngulelo.
Matembezi hayo yameanza kwenye mzunguko wa Impala kuelekea mzunguko wa mnara wa saa kupitia barabara ya Sokoine na kupandia mtaa wa Uswahilini (barabara ya St.Thomas Hospital) na kuishia mzunguko wa Mnara wa Mwenge (Makumbusho ya Azimio la Arusha).