Mkuu wa Mauzo na Mtandao wa Matawi wa benki ya NMB, Donatus Richard akifurahi pamoja na mashabiki WA Yanga waliojitokeza kupiga picha na Makombe ya Yanga. Benki ya NMB imeingia makubaliono na Yanga kurahisisha wanachama kujisajili kwenye Matawi yote ya NMB kuanzia tarehe 10 Julai.
Mashabiki wa timu ya Yanga wakiwa ameshikilia jezi mpya za timu hiyo katika Banda la Benki ya NMB kwenye viwanja vya Sabasaba
 
Shabiki wa Yanga, Mary Jakobo akifurahi na mtoto wake kwa kupiga picha na makombe ya timu hiyo

Na Mwandishi Wetu

Benki ya NMB kwa kushirikiana na Klabu ya Yanga imewaomba wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuchangamkia fursa ya kujisajili ili  kupata kadi za uanachama ambazo zitawasaidia kutambulika na klabu hiyo pamoja kupata kwa urahisi huduma za kibenki.

Hayo wameyaeleza jana walipokuwa kwenye viwanja vya maonesho ya kibiashara ya Sabasaba ambapo pia mashabiki wa timu hiyo walipata fursa ya kupiga picha na makombe matatu ambayo walibebwa na timu hiyo msimu uliopita wa 2022/23.

Wiki iliyopita Taasisi hizo mbili ziliingia makubaliano ya ushirikiano wa kusajili Wanachama kwa Benki hiyo kuanzisha kadi maalumu kwa ajili ya wanachama wa timu hiyo ambazo mbali na uanachama wao pia zitawasaidia katika huduma nyingine za kifedha.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkuu wa Mauzo na  Mtandao wa Matawi  wa benki hiyo, Donatus Richard alisema pamoja na mambo mengine lakini maamuzi yao yametokana na ubora na mafanikio ya timu ya Yanga ambayo imeyapata msimu uliopita.

“Benki Bora ya NMB na timu bora ya Yanga tumeungana ili kurahisisha usajili wa Wanachama na mchakato wa kuanza kujiandikisha utaanza jumatatu tarehe 10 Julai” alisema Richard.

Alisema wao kama washiriki wenza katika mpango huo tayari wamejipanga mikoa yote nchini kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa urahisi katika kila tawi la NMB na amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.

Aidha alisema kwa wale mashabiki wa Yanga nawenyewe wanaruhusiwa kwenda kwenye matawi ya NMB kupata kadi zao .

Wakati huo huo shabiki wa yanga Mary Jakobo amesema kuwa amefurahi kupigapicha na makombe hayo na kudai msimu ujao lazima waya bebe kwa mara nyingine.

“Nimefurahi kupata nafasi ya kupiga picha makombe yetu msimu ujao naamini tutaendeleza ushindani wetu,alisema Jakobo.
Naye Doto Kapela amesema msimu huu timu yao inafanya usajili mzuri ambao utawapa mafanikio makubwa msimu ujao utakaoanza mwezi Agosti mwaka huu.

Yanga inatarajia kusajili zaidi ya wanachama milioni nane kwa miaka miwili ya mkataba huo na Benki hiyo ya NMB.