Kundi la muziki wa zouk la Makoma lilikuwa na wanamuziki ambao walimudu kweli kuwachengua mashabiki waliokuwa wamefurika ukumbini walipofanya ziara nchini miaka kadhaa iliyopita. Wakati huo wengi wa mashabiki nchini walilikubali kundi hilo mwanzoni wakidhani kuwa ni kundi la muziki kama ilivyo Bongo Fleva.

Dhana hiyo ilinogeshwa na mabango ya matangazo kuhusiana na onyesho la kundi hilo. Wengi wakatamani kwenda kuwashuhudia vijana hao waliokuwa wakionekana kujipamba kisasa zaidi.

Picha zao ziliwaonyesha kama ni kina dada ‘washua’, wenye kujiremba kwa vipini puani, utengenezaji wa nywele na mavazi ya kisasa, hata jinsi ya ushambuliaji wa jukwaa.

Watu hao waliokuwa na shauku ya kuzisikiliza nyimbo zao, ndipo walibaini kuwa ni waimbaji wa muziki wa Injili, tofauti na mawazo yao walipodhani kuwa ni wasanii wa muziki wa kidunia.

Hata hivyo, vijana hao wa Makoma Troupe, usiku huo walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwaduwaza wapenzi kwa nyimbo zao za Injili, wakicheza kwa miondoko ya reggae.

Makoma Troupe ni kundi lililowahi kutamba katika tasnia hiyo, lililokuwa likiwakilishwa na ndugu sita; kaka wakiwa watatu na dada watatu, pamoja na rafiki wa familia yao.

Waliweza kuitikisa dunia hasa kwa wapenzi wa muziki wa Injili ambao waliuimba kwa miondoko ya muziki wa kisasa.

Kundi hilo la Makoma lililoundwa na wasanii ambao walikuwa wakiimba kwa kutumia mtindo wa Rumba, Pop na R&B kutoka Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baadaye walihamia nchini Uholanzi.

Kundi hilo la Makoma limekwisha kufanya kazi karibu nchi nyingi za Afrika.

Waimbaji wanaounda kundi hilo ni Nathalie Makoma, Annie Makoma, Pengani Makoma, Tutala Makoma, Duma Makoma, Martin Makoma na rafiki yao Patrick Badine.

Wakati wa kuimba hutumia lugha ya Lingala na Kiingereza lakini pia Kifaransa, Kireno na Kijerumani.

Waliweza kujihakikishia kuendelea kubaki katika tasnia hiyo kila wanapofyatua albamu.

Makoma Troupe walipata pigo mwaka 2004 baada ya mwimbaji wao nyota wa kundi hilo lililojipatia umaarufu barani Afrika na kwingineko duniani, Nathalie Makoma, kuamua kujiondoa.

Baada ya kulikacha kundi hilo, Nathalie aliamua kuimba muziki wa kidunia akiwa nje ya kanisa kutokana na kile alichodai kutaka kufanya kazi nyingine.

Wajuzi wa mambo walidai kuwa ugomvi baina yake na kaka yake mkubwa, ambao amekuwa akiuzungumza sana kwenye vyombo vya habari, ndiyo sababu kubwa ya mwimbaji huyo kuamua kuachana na kundi hilo.

Wapenzi na mashabiki walimshauri azingatie kuwa yeye alikuwa ni mwanzilishi  anayetegemewa na kundi hilo kwa takriban nyimbo zote. Wakampa mapendekezo kuwa yule ni kaka yake, wanatakiwa kuzungumza masuala yao kifamilia, si kuanika kwa kila mtu kuliko kujitoa kundini.

Nathalie ni mwimbaji aliyewahi kushika nafasi ya pili katika shindano la kutafuta mwimbaji maarufu lililoitwa Netherlands Idol mwaka 2008 na kupewa jina la Tina Turner.

Kwa leo tuishie hapa, wiki ijayo tutaangalia kwa undani Nathalie ni nani hasa.