Pluijm

Pluijm

Pazia la Ligi Kuu ya Vodacom nchini linatarajiwa kufunguliwa rasmi Agosti 22, mwaka huu kwa mechi ya Ngao ya Hisani kati ya Azam na Yanga, na Septemba 12 ndiyo mechi za msimu wa Ligi 2015/2016 zitaanza rasmi.

Mabadiliko mengi yamefanyika kwa timu mbalimbali za Ligi Kuu, hali inayoashiria kuwa na msimu wa ligi ngumu zaidi kuliko hata iliyopita msimu wa 2014/2015. 

Tumeshuhudia katika msimu uliopita timu zikipishana kwa idadi ndogo ya pointi kuanzia kwa timu zilizoshuka daraja, zilizonusurika kushuka daraja mpaka nafasi ya ubingwa.

Mbanano wa pointi au kupishana mabao tu ili kutofautisha nafasi kati ya timu moja na nyingine katika msimamo wa ligi, ni ishara ya ugumu wa ligi unaotokana na kuimarika kwa timu mbalimbali nchini. 

Kuimarika kwa timu hizo kumeondoa utawala wa Simba katika nafasi za kuwakilisha Taifa katika mashindano ya kimataifa kama ilivyozoeleka. Imepita misimu mitatu Simba haijapata nafasi kushiriki michuano ya kimataifa kwa kuambulia nafasi ya tatu na ya nne katika msimamo wa ligi huku Yanga na Azam zikibadilishana nafasi mbili za juu. 

Kuondolewa kwa Simba katika nafasi mbili za juu ni salamu tosha kwa Azam na Yanga kwamba ligi haina mwenyewe na yeyote anaweza kuwa bingwa kutegemeana na juhudi zake. Kutokana na maboresho na mabadiliko makubwa yanayoendelea kutoka katika Ligi Kuu ya Vodacom ni wazi Simba, Yanga na Azam zitakuwa katika wakati mgumu zaidi msimu huu. Yafuatayo ni mabadiliko ambayo yataifanya ligi ya msimu huu kuwa ya ushindani zaidi:

 

UZALENDO

Baada ya mashabiki wa Mbeya kuamua kushabikia timu za nyumbani hasa Mbeya City na kupata mafanikio makubwa katika ligi, mashabiki wa timu za mikoa mingine wamezinduka kuanza kushabikia timu za mikoani kwao kwa nguvu kubwa.

Simba na Yanga zinapata vipigo kiulaini zikienda Mbeya na Tanga, jambo ambalo linaamsha morali kwa mashabiki wa Shinyanga, Kagera, Songea, Mwanza na Mtwara kushabikia timu zao za nyumbani na kuzipa wakati mgumu timu kubwa nchini.

 

KUONGEZEKA KWA TIMU SHIRIKI

Kwa misimu mingi, Ligi Kuu hapa nchini imekuwa na timu shiriki 14 tu. Msimu huu timu zimeongezeka na kuwa 16, jambo linaloashiria kuwa na ligi ndefu na yenye changamoto zaidi kiushindani.

Ili kupata timu 16 zitakazoshiriki Ligi Kuu, TFF iliamua zishuke timu mbili na zipande timu nne. Timu zilizoshuka zilikuwa ni Polisi Morogoro na Ruvu Shooting huku timu zilizopanda daraja zikiwa ni Mwadui ya Shinyanga, African Sports ya Tanga, Toto African ya Mwanza na Majimaji ‘Wanalizombe’ wa mkoani Ruvuma. 

Katika misimu ya karibuni timu zinazopanda daraja huwa ni ngumu zaidi na mfano wa wazi ni Mgambo JKT, Mbeya City, Ndanda FC na Stand United ambazo kila moja zilitoa vipigo kwa timu vigogo za Simba na au Yanga na Azam bila huruma.  

 

UJIO WA MAKOCHA WA KIGENI

Iko wazi kuwa Wazungu ndiyo waliotawala soka la dunia na ujio wa makocha wa kigeni hususani kutoka Ulaya ni wazi kuwa timu nyingi zinataka kutawala soka hapa nchini. Kilichotokea kuhusu usajili wa makocha msimu huu imekuwa ni kama, “wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini?” Jambo hili hata kwa mashabiki linaleta morali kuwa timu zao zimedhamiria kuleta ushindani katika ligi. 

Kuonesha kuwa fedha inaongea, Majimaji wamemleta kocha raia wa Finland, Mika Lonnstorm; raia wa Ujerumani, Martin Glerics, ametua Toto African, Stand United wamemvuta kocha wa zamani wa Simba, Patrick Liewig, huku Azam wakimrejesha Stewart Hall kama Yanga walivyofanya kwa Hans Der Pluijm na Simba wamemleta Mwingereza Dylan Kerr. Bila shaka kila kocha atataka kuonesha kuwa yeye ni kocha bora kutoka nje kwa matokeo ya uwanjani, lakini makocha wazawa kama Julio na Minziro nao watataka kuwakata ngebe.

 

MUDA WA KUTOSHA KUFANYA USAJILI

Dirisha la usajili lilitarajiwa kufungwa Agosti 6, mwaka huu lakini muda wa kufunga dirisha hilo umesogezwa mbele mpaka Agosti 20. Katika muda huo wa nyongeza timu zimesajili na kuacha baadhi ya wachezaji.

Muda mrefu katika usajili umetoa mwanya wa kufanya usajili kwa umakini na kuziba matundu ambayo kama dirisha lingefungwa tarehe ya awali matundu hayo yangeendelea kubaki wazi. 

 

KUONGEZEKA KWA UDHAMINI

Ligi imeanza kuwa na ushindani mkali hasa kutoka Azam TV walipoingia mkataba na TFF kwa ajili ya kuonesha michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom. Miaka ya nyuma timu nyingi zililia njaa na wakati mwingine hata chakula cha kula wachezaji wakiwa kambini ulikuwa ni mtihani mzito. Jambo la pili, timu zilikosa kabisa pesa za usajili hata wa bei chee na ilikuwa na suala la kupanda vijana wanaotaka kucheza ili kuonekana na si kutaka ushindi.

Mambo yamebadilika sana kwa sasa kwani kila timu ina uhakika wa milioni 100 toka Azam TV. Pesa hizo za udhamini zimeimarisha sana timu mbalimbali, jambo ambalo limeleta ushindani mkubwa katika ligi ya msimu uliopita. Msimu huu pesa hiyo ipo mezani lakini wadau wengi wamechomoza kudhamini timu mbalimbali za ligi kuu mbali na udhamini wa Azam TV. 

Kwa ujumla, timu nyingi hazilii ukata ukiacha Ndanda FC ambao wamekuwa wakiomba wadau kuidhamini timu hiyo. Kwa upande wa udhamini mkuu wa ligi Vodacom mambo yamezidi kunoga maana mkataba mpya wa udhamini umeboreshwa zaidi na kuleta afueni kwa wadau wote wa ligi. Udhamini huo wa Vodacom wenye thamani ya bilioni 6.6 kwa miaka mitatu unafanya ligi iendeshwe kwa bajeti ya bilioni 2.2 kutoka bajeti ya bilioni 1.6 kwa misimu iliyopita. 

Aidha, udhamini huo wa bilioni 2.2 kwa mwaka unalenga kupeleka bilioni 1.2 moja kwa moja katika timu zishiriki, jambo ambalo litasaidia timu kuwa na uhakika wa vifaa na mambo mengine. Udhamini huo umeboresha zawadi kwa washindi ambapo katika msimu mpya wa ligi timu mshindi wa kwanza itapata 80,401,160, mshindi wa pili 40,200,580, mshindi wa tatu 28,714,700 na mshindi wa nne 22,971,760. 

Kwa ujumla, ligi inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa sana na hivyo timu kubwa zijipange kisaikolojia kupokea matokeo watakayoyapata maana kila timu imejipanga kufanya vizuri. Huu ni msimu ambao tunaweza kushuhudia timu zikifukuza sana makocha kuliko misimu mingine kutokana na matokeo yasiyotarajiwa yatakayotokana na ushindani utakaokuwapo. 

Nitoe rai kwa Simba kujipima kama wamekuwa wamoja au bado kuna Simba Ukawa? Mbeya City wajitazame kama ile migawanyiko yao ipo au imemalizwa? Nasema haya ili kipenga kikilia kusiwe na malalamiko ya mwaka jana. Tunasubiri ligi itakayochangamshwa na maneno ya wasemaji kama Haji Manara, Jerry Muro, Thobias Kifaru na makocha kama Jamhuri Kihwelo Julio.

 

Baruapepe: [email protected]/Simu: 0715 36 60 10