Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar, ambaye pia ni kiongozi wa chama cha upinzani cha SPLM-IO, amekataa uteuzi wa Jenerali Chol Thon Balok kuwa waziri mpya wa ulinzi.
Jenerali huyo anatoka chama cha Rais Salva Kiir na anachukua nafasi ya Angelina Teny, mke wa Machar, ambaye alifutwa kazi wiki chache zilizopita.
Mkataba wa amani uliomaliza vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano unagawanya nyadhifa za baraza la mawaziri kati ya vyama vya Bw Kiir na vya Machar.
SPLM-IO imemtaka Kiir kubatilisha uteuzi wa Jenerali Thon, kikisema rais hapaswi kuchukua maamuzi hayo ya upande mmoja hadi pale mzozo wa kufutwa kazi utakapotatuliwa na naibu wake.
Matukio hayo yanatishia makubaliano yaliyotiwa saini mwaka 2018 ambayo yananuiwa kuandaa njia ya uchaguzi mwaka ujao.