Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ametoa onyo kwa wananchi wenye tabia ya kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo ya hifadhi, akiwataka waache mara moja na wale watakaoendelea wasije kuilaumu serikali kwa hatua itakazochukua dhidi yao.

Ameyasema hayo wakati akizindua rasmi Jeshi Usu ambalo limepewa jukumu la kulinda maliasili za nchi, ikiwemo wanyamapori na misitu, Fort Ikoma, Serengeti mkoani Mara, mwishoni mwa wiki.

Uzinduzi huo umehusisha taasisi tatu za Wizara ya Maliasili na Utalii za Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Kuanzishwa kwa Jeshi Usu hilo ni utekelezaji wa Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 iliyoelekeza kubadili mfumo wa uendeshaji kutoka wa kiraia kuwa wa kijeshi.

Makamu wa Rais ametoa mwito kwa wananchi kutovamia hifadhi na kutofanya ujangili, akisema kipenga kimepulizwa.

Amewataka wanachi wanaoishi eneo linalozunguka hifadhi washirikiane na Jeshi Usu kulinda usalama wao na wa watalii. Pia amelitaka jeshi hilo lishiriki kutambua na kudhibiti vitendo vya kigaidi, kwani wapo magaidi wanaoweza kuingia nchini kwa kutumia kivuli cha kutalii.

Amesema ujio wa jeshi hilo utasaidia kupambana na majangili ambao wamekuwa wakitumia silaha za kivita.

Amezitaja changamoto zinazoukabili uhifadhi kuwa ni pamoja na ujangili, uvamizi wa mifugo kwenye hifadhi, uvamizi wa mipaka, mmomonyoko wa maadili miongoni mwa watumishi, wanunuzi haramu wa mazao ya misitu na uchomaji moto.

Taarifa za kiintelijensia zinaonyesha kuwa silaha nyingi na risasi zinaingizwa kutoka nchi jirani. Majangili hao wamekuwa na mtandao ndani na nje ya nchi.

Makamu wa Rais anaamini kuanzishwa kwa Jeshi Usu si tu kutapunguza, bali kutamaliza ujangili nchini.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa usalama katika hifadhi, hata sura za bodi za taasisi za uhifadhi kwa sasa ni za kijeshi. Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA ni Jenerali mstaafu George Waitara; Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA ni Meja Jenerali mstaafu Hamis Semfuko; na kwenye Bodi ya NCAA kuna mjumbe ambaye ni Brigedia Jenerali (mstaafu) Aloyce Damian Mwanjile.

“Hii ni kuonyesha kuwa serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa ujangili wa wanyamapori nchini unakwisha na si kupungua tu, bali pia maeneo yaliyohifadhiwa hayatumiki kama maficho ya magaidi na waharibifu wa mazingira,” amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Nape Nnauye, amezitaka operesheni za Jeshi Usu ziendeshwe kwa kuzingatia haki za binadamu ili wananchi waone thamani ya uhifadhi.

Awali, Waziri wa Malisili na Utalii, Hamis Kigwangalla, amempongeza Rais John Magufuli kwa kuridhia uanzishwaji wa jeshi hilo, huku akiwataka Watanzania kuwa wazalendo na wenye uchungu na maliasili zilizomo nchini.

Ameongeza kuwa, Jeshi Usu litachangia kuongeza nidhamu pamoja na uwajibikaji kwa askari hao.