…………………………………………………………………….

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Wizara zote, Taasisi za Umma, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi, Watanzania wanaoishi Ughaibuni (Diaspora) na Wadau wote wa maendeleo kutoa ushirikiano wa kutoa maoni na taarifa kwa timu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili uchambuzi uwe halisia na toshelevu.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Mchakato wa Maandalizi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma leo tarehe 03 Aprili 2023. Amesema dira hiyo inatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii ili kufikia lengo la kuwa Taifa lenye ustawi.

Makamu wa Rais amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha katika maandalizi ya Dira hiyo, Watanzania kutoka pande zote za nchi, kutoka matabaka mbalimbali ya maisha, makundi mahsusi kama Bunge na Mahakama yatapata nafasi ya kuchangia mawazo yao.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango akiwasalimu viongozi na wananchi mbalimbali wakati alipowasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma kuzindua Mchakato wa Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Aprili 3, 2023. (Wengine pichani ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Zungu,Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu Kiongozi Dkt.Moses Kusiluka, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Daniel Chongolo na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu Mwamba

Makamu wa Rais ametoa wito wa mambo ya kuzingatia wakati wa maandalizi wa dira hiyo ikiwemo fursa ambazo hazijatumika ipasavyo hadi sasa na pamoja na kuzikamata fursa zinazochipukia, kuzingatia masuala ya elimu hususan sayansi, ufundi na ufundi stadi, utafiti na maendeleo, na ubunifu ili kukuza ujuzi na uwezo wa nguvukazi ya Taifa, namna ya kuvutia na kuasili teknolojia ili kukuza tija katika sekta zote za uzalishaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa pamoja na kuingia ubia wa kimkakati kuiwezesha Tanzania kuwapita washindani wake katika kipindi kifupi.

Ametaja mengine ya kuzingatia kama vile kubaini kiuhalisia rasilimali zote zinazohitajika kuwezesha utekelezaji makini wa Dira na mipango na kubainisha mfumo thabiti wa ufuatiliaji na tathmini kwa kuangalia vigezo mahususi vilivyowekwa pamoja na kujifunza kutoka katika nchi zilizofanikiwa kuendelea kwa kasi kuanzia miaka ya 1960 hususan zile za bara la Asia.

Makamu wa Rais ametaja hatua zilizopigwa na Tanzania hadi hivi sasa ikiwemo kujenga na kuimarisha utawala wa sheria, haki na demokrasia, Mhimili wa Mahakama kuimarisha kazi ya kutoa haki kwa wananchi pamoja na Serikali kuendelea kuzingatia sheria, mila na desturi za watanzania katika uendeshaji wa shughuli za kiserikali. Ameongeza kwamba uhuru wa vyama vya siasa na vyombo vya habari umeimarika pamoja na kupatikana mafanikio ya kuridhisha katika elimu ikiwemo kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi katika ngazi zote kuanzia shule za msingi hadi vyuo vya elimu ya juu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango akizindua rasmi Mchakato wa Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma leo tarehe 03 Aprili 2023 (Kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba)

Kwa Upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imeweza kufanikisha hatua mbalimbali za kimaendeleo kama vile uboreshaji wa miundombinu , ongezeko la shule, ukuaji wa sekta ya michezo pamoja na ukuaji wa uchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Awali akitoa taarifa ya Mchakato wa Maandalizi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu Mwamba amesema chimbuko la Maandalizi ya Dira 2050 imetokana na kuendeleza mafanikio yaliofikiwa kutokana na utekelezaji wa Dira 2025 pamoja na uhitaji wa mkakati utakaowezesha nchi kunufaika na maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia yanayoendelea kuibuka duniani.

Ameongeza kwamba Dira 2050 itahakikisha kuwa Tanzania inaendelea na mkakati utakaoainisha ajenda ya maendeleo ya nchi na mikakati mingine ya kikanda na kimataifa.

Uzinduzi wa Mchakato wa Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Viongozi wa vyama vya Siasa, Wabunge, Wadau wa Maendeleo, Sekta binafsi , Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, Viongozi wa dini pamoja na wananchi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango akihutubia Viongozi, Wadau wa Maendeleo pamoja na wananchi mbalimbali wakati wa Uzinduzi wa Mchakato wa Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango akiwakabidhi Waandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Dkt. Suzan Mlawi na Prof. Samuel Wangwe muongozo wa maandalizi ya dira hiyo mara baada ya kuzindua Mchakato wa Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050