Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali zote mbili chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi zimedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Michezo kwa kujenga miundombinu ya kisasa ya michezo mbalimbali pamoja na kufundisha wataalamu wa michezo ili kuibua vipaji na kuinua viwango vya michezo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Hafla ya Uwekaji Jiwe la Msingi Ujenzi wa Viwanja vya Michezo vya Priz katika eneo la Kilimani Unguja Zanzibar leo tarehe 24 Aprili 2025 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano.
Amesema jiwe la msingi la ujenzi wa viwanja hivyo vya michezo ni mwendelezo wa uwekezaji katika sekta ya michezo ambayo ni miongoni mwa sekta za kimkakati zinazokua kwa kasi na inayotarajiwa kutoa hamasa na kuvutia mashindano ya michezo mbalimbali katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Amesema Serikali kupitia Wizara zinazohusika na Michezo itaendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika michezo yote ikiwemo michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete riadha, bao, drafti, karata, mieleka, mchezo wa ngombe, mbio za baskeli na mbio za ngalawa. Makamu wa Rais ameongeza kwamba ni dhamira ya Serikali kuendelea kutoa fursa kwa watoto, vijana, wanafunzi, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki katika michezo mbalimbali kwenye mazingira rafiki na yenye usalama zaidi.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema viwanja vinavyojengwa hivi sasa vimezingatia kwa kiasi kikubwa utatuzi wa changamoto mbalimbali ambazo zinazoyakumba makundi maalum katika kushiriki michezo kama vile udhalilishaji, umbali mrefu wa kufuata viwanja na miundombinu isiyowezeshi kwa wachezaji wenye mahitaji maalumu na wanawake.
Makamu wa Rais amesisitiza maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano yaende sambamba na shughuli ya kuhifadhi mazingira, kama upandaji miti katika maeneo ya viwanja vya michezo, maeneo ya kupumzikia na maeneo mengine pamoja na kuhimiza usafi wa mazingira, ikiwemo kutumia nishati safi ya kupikia.
Vilevile, Makamu wa Rais amesema ili kuimarisha sekta ya michezo nchini, ni muhimu kufanya jitihada za kuvutia timu mbalimbali kutoka nje ya nchi kufanya ziara za michezo hapa nchini na kuendelea kuvutia mashindano ya kimataifa. Amesema Serikali inahitaji kushirikiana na wadau katika kutekeleza programu mbalimbali ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Makamu wa Rais amewasihi wadau wa sekta binafsi kuunga mkono jitihada za kuinua sekta ya michezo kwa kuanzisha maeneo ya kijani ambayo yanaweza kutumika pia kwa ajili ya michezo na burudani (Green parks), kuanzisha timu/klabu mbalimbali za michezo, kuanzisha na kuendesha shule maalum za michezo pamoja na kushiriki katika jitihada mbalimbali za kuwashirikisha wenye mahitaji maalum katika michezo.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imevuka malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 kwa kuwekeza zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya michezo katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.
Amesema Viwanja hivyo ni fursa kwa vijana kupata ajira pamoja na kujiepusha na tabia hatarishi ikiwemo matumizi ya za kulevya.







